Ufaulu wa awali, msingi washuka Kishapu

Kishapu. Wakati juhudi zikiongezwa kuboresha elimu nchini, takwimu mpya zimeibua wasiwasi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga baada ya kiwango cha ufaulu katika elimu ya awali na msingi kushuka kwa asilimia 10 ndani ya mwaka mmoja, huku ukosefu wa chakula shuleni na changamoto za ufundishaji ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu.

Taarifa hiyo imebainishwa katika kikao cha wadau wa elimu cha tathmini ya matokeo ya mwaka 2026 kuanzia shule za awali, msingi hadi sekondari, kilichofanyika leo Machi 27, 2026 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kishapu.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wilayani humo, Boas Mafuru, amesema kiwango cha ufaulu kimeshuka kutoka asilimia 71 mwaka 2025 hadi asilimia 61 mwaka 2026.

Amesema changamoto kadhaa zimechangia hali hiyo, ikiwamo ukosefu wa chakula katika baadhi ya shule, ufundishaji usio na viwango kwa baadhi ya walimu pamoja na usimamizi dhaifu katika baadhi ya shule.

“Ukosefu wa chakula kwa baadhi ya shule, ufundishaji usio wa kiwango kwa baadhi ya walimu, usimamizi dhaifu kwa baadhi ya viongozi wa shule, pamoja na ukosefu wa hamasa ya elimu kwa baadhi ya wazazi na utoro wa wanafunzi, ni miongoni mwa sababu zilizosababisha kushuka kwa ufaulu,” amesema Mafuru.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, divisheni ya elimu imeweka mikakati mbalimbali ikiwamo kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya chakula katika shule zote 128 za awali na msingi wilayani humo ili wanafunzi waweze kupata lishe wanapokuwa shuleni.

“Tumekubaliana kuhamasisha kilimo cha mazao ya chakula katika shule zote ili kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe. Pia tutaimarisha usimamizi wa ufundishaji na kufanya tathmini za mara kwa mara kwa wanafunzi ili kuongeza kiwango cha ufaulu,” ameongeza.

Wakati juhudi zikiongezwa kuboresha elimu nchini, takwimu mpya zimeibua wasiwasi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga baada ya kiwango cha ufaulu katika elimu ya awali na msingi kushuka kwa asilimia 10 ndani ya mwaka mmoja, huku ukosefu wa chakula shuleni na changamoto za ufundishaji ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amemtaka Ofisa Elimu wilayani humo kusimamia kikamilifu majukumu yake, akisisitiza kuwa uzembe katika usimamizi wa elimu unaweza kuchangia kushuka kwa ufaulu.

Masindi amesema Serikali haitavumilia kushuka kwa kiwango cha ufaulu, akisisitiza kuwa watendaji wote wanaohusika na usimamizi wa elimu wanapaswa kuwajibika ipasavyo.

“Afisa elimu anapaswa kusimamia majukumu yake ipasavyo. Uzembe katika nafasi hiyo ni chanzo kikuu cha kushuka kwa ufaulu. Serikali haiko tayari kuvumilia hali hiyo, na wale watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao wanapaswa kujitathmini au kupisha wengine wenye uwezo,” amesema Masindi.

Aidha, amewaelekeza wadhibiti ubora wa elimu pamoja na waratibu wa elimu kuhakikisha wanafika mashuleni mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na hali ya ufundishaji.

Amesisitiza pia umuhimu wa kujenga msingi imara wa elimu kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari, akieleza kuwa hatua hiyo ndiyo itakayosaidia kuboresha matokeo ya wanafunzi katika ngazi za juu.

Masindi pia amesisitiza umuhimu wa lishe kwa wanafunzi, akionya kuwa yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa mpango wa chakula shuleni atachukuliwa hatua kali.

“Walimu wenye weledi na bidii wanapaswa kupewa nafasi za uongozi ili wasimamie kwa nguvu suala la ufaulu na lishe mashuleni. Pia kuna umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu, wazazi na walezi katika kupambana na utoro na kuboresha mazingira ya ujifunzaji,” amesema.

Katika kikao hicho, wadau mbalimbali wa elimu wakiwamo taasisi za dini, taasisi zisizo za kiserikali na sekta ya fedha, zikiwamo TCRS, benki za CRDB na NMB, wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu wilayani humo.

Wadau hao wameahidi kusaidia kuboresha miundombinu ya shule ikiwamo ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na vyoo, pamoja na kutumia majukwaa yao kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu na lishe kwa watoto.

Katika hatua ya kuhamasisha ushindani wa kitaaluma, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fadhili Mvanga, amekabidhi vyeti vya pongezi kwa shule 10 zilizofanya vizuri katika mitihani ya mwaka 2026.

Hata hivyo, shule zilizofanya vibaya zimepewa vinyago kama ishara ya kuhamasisha kuongeza juhudi katika kuboresha ufaulu.

Pamoja na changamoto hizo katika elimu ya awali na msingi, takwimu zinaonyesha kuwa hali ya ufaulu katika shule za sekondari wilayani humo imeendelea kuwa nzuri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiwango cha ufaulu wa kidato cha pili kimeendelea kubaki asilimia 86 kwa mwaka 2025 na 2026, huku ufaulu wa kidato cha nne ukiongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2025 hadi asilimia 93 mwaka 2026.