TIMU ya Uhamiaji, imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Black Sailors katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo Ijumaa Machi 27, 2026 kwenye Uwanja wa Mao Zedong B, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu hizo kuelekea mashindano yaliyo mbele yao.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani wa hali ya juu, Uhamiaji ilionesha kiwango kizuri hadi kufanikiwa kutumia vyema nafasi ilizozipata, jambo lililozaa matunda ya ushindi huo.
Black Sailors ilijitahidi kurudi mchezoni kwa kutengeneza mashambulizi kadhaa langoni mwa Uhamiaji lakini uimara wa safu ya ulinzi ya wapinzani wao iliwafanya ishindwe kubadili matokeo licha ya kupata bao moja.
Matokeo hayo yanaifanya Black Sailors inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar kuendelea kuwa na wakati mgumu katika michezo yao ya maandalizi, baada ya kupoteza mara ya tatu mfululizo kwa idadi hiyo hiyo ya mabao 2-1 kwenye kujipima kwao.
Licha ya matokeo hayo, michezo ya kirafiki imekuwa na umuhimu mkubwa kwa timu hizo kwani inawapa makocha nafasi ya kujaribu mbinu mbalimbali, kuwapa nafasi wachezaji tofauti na kufanya tathmini ya kikosi kabla ya kuingia katika mashindano rasmi.
Kwa upande wa Uhamiaji inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, ushindi huo unaonekana kuongeza morali kwa wachezaji huku ukiwa na ishara ya maandalizi mazuri kuelekea michezo ijayo ya ligi hiyo inayoendelea kesho Jumamosi.
