WALIMU 150 wa amali kwenye shule za serikali wanaondoka Jumapili kwenda nchini India kwa mafunzo maalum ya amali ambayo yatawawezesha kuongeza ujuzi kwenye taaluma hiyo.
Walimu hao kutoka mikoa mbalimbali nchini waliagwa rasmi jana kwenye hafla maalum iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali.
Waliagwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe na Mkurugenzi Mkuu wa Global Education Link, (GEL) Abdulmalik Mollel.
Akizungumzawakati wa hafla ya kuwaaga walimu hao, Profesa Mkenda alisema safari hiyo ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza kuboreshwa kwa elimu ya amali.
Profesa Mkenda alisema kwa kuwa wameanza kutoa mafunzo hayo ya amali ikiwemo kwenda kujifunza kwenye mataifa mbalimbali duniani hakutakuwa na kurudi nyuma.
“Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza mara kadhaa kuhusu mafunzo ya amali, anataka kuona tunakwenda mbali zaidi namimi nasema kwa kuwa tumeanza basi hatutarudi nyuma, tutakwenda India na mataifa mbalimbali kujifunza wenzetu wamefanyanini kwenye mafunzo ya amali,” alisema
Aidha, aliwataka walimu hao kujifunza kwa bidii wakiwa nchini India ili watakaporudi wawe mfano kwa walimu wengine ambao hawajapata nafasi hiyo.
“Tunataka kuona mabadiliko makubwa, mtakaporudi watu waone kabisa kwamba kuna watu walikuwa nchini India kwa masomo, mhakikishe shule zinavifaa vya kufundishia masomo ya amali katika ngazi zote,” alisema
“Tunatambua maono makubwa ya rais wetu kwenye masomo ya amali kwa hiyo kazi yetu sisi wasaidizi wake ni kuyatafsiri kwa vitendo kwa kufanya kazi kuhakikisha tunatimiza ndoto hizo kwa kutoa elimu bora na siyo bora elimu,” alisema
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe alisema kuzingatia nidhamu na maadili watakayofundishwa nchini India kwaajili ya kuja kuleta matokeo chanya kwenye maeneo yao.
“Tunataka mkirudi muwe chachu kwa wengine kutaka nao kwenda India kujifunza, mtushauri tufanye nini ili tuweze kutoa matokeo chanya kwenye maono ya rais Samia,” alisema
Aidha, alisema safari ya walimu hao ni matokeo ya mabadiliko ya mitaala ya elimu yaliyoanza muda mrefu na kuja kutekelezwa na Rais wa awamu ya sita, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mageuzi ya elimu utekelezaji wake ni wa muda mrefu,unamilima na mabonde kwa hiyo ingawa kuna changamoto nyingi lakini sisitutapambana mpaka mwisho hakutakuwa na kurudi nyuma hata siku moja,” alisema Waziri Shemdoe





