Mbeya. Zaidi ya Watu 1, 000, waishio katika mazingira magumu wakiwepo wazee walemavu ,yatima kupatiwa mahitaji mbalimbali ikiwepo vyakula ili kuwawezesha kuungana na watanzania wengine kusherehekea Sikukuu ya Pasaka.
Machi 26, 2026, ikiwa ni siku pili baada ya kuzinduliwa rasmi kampeni maarufu ” Bendera ya Upendo” msimu wa tatu yenye lengo ya kubaini wahitaji na kuwarejesha tabasamu hususani waishio makazi hatarishi kujengewa nyumba za kisasa.
Hatua hiyo imepelekea kugeuka kilio cha furaha kwa baadhi wa wahitaji ambao wamefunguka kueleza magumu wanayo pitia kwa kukosa mahitaji kikiwepo chakula.
Mratibu Kiongozi wa Kampeni hiyo kupitia Taasisi ya Tulia Trust, Lugano Mwangosi amesema lengo la kugusa makundi hayo ni sehemu ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi sambamba na msimu wa tatu kukimbiza bendera hiyo.
’Mwaka huu tuna kauli mbiu ‘Tunataka kukuza, kueneza upendo, umoja na mshikamano “kwa lengo la kuhamasisha matendo ya huruma kwa jamii kujitolea kuwasaidia watu wenye uhitaji kabla na baada ya kuwabaini,” amesema.
Amesema msimu huu wamewekea malengo kuyafikia makundi mbalimbali ya wahitaji zaidi1,000,pasipo kuacha wazee,walemavu, yatima kwa kuzifikia Kata 13, na mitaa 60,sambamba na kugawa mchele kilo 10 kwa kila mmoja .
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo amesema kwa siku ya jana Machi 24, mwaka huu kampeni hiyo imewafikia wahitaji 200 ,huku baadhi yao kubainika kuishi katika makazi hatarishi.
Mwakanolo amesema huu ni mwendelezo wa Taasisi hiyo kugusa wahitaji ikiwa ni mpango mkakati kupitia “Tulia Trust mtaani kwetu” wenye lengo la kurejesha tabasamu kwa walengwa kuwa kama jamii nyingine.
“Baada ya kuhitimisha kampeni ya bendera ya upendo,Tutarejea kwa ajili ya kufanya tathimini za makazi ya wazee ili kutoa mrejesho kwa Mkurugenzi wetu Dk Tulia kwa ajili ya taratibu za kuanza ujenzi wa makazi bora ya kisasa, “amesema.
Awali akipokea msaada qa chakula, Mwanamke Ester Kisole (80), amejikuta akiangua kilio cha furaha na kumshukuru Dk Tulia kugusa makundi yaliyo sahaulika kupitia bendera ya upendo.
“Nalia kwa furaha namshuku sana kwa msaada huu wa chakula mimi na familia yangu,lakini kikubwa namuombea kwa Mungu Dk,Tulia na tumbo lililo mzaa kwa ajili ya kutushika mkono wahitaji,”amesema.
Naye, Lotina Mwambani, Mkazi wa Mtaa wa viwandani, Kata ya Mwakibete ameshukuru kwa msaada wa mchele kilo 10 ,na kubainisha utawezesha kula na familia yake katika kusherehekea sikuu ya Pasaka Aprili 5,mwaka huu,
“Hatuna ya kusema ni mengi ametufanyia kuhakikisha tunakuwa na tabasamu kama jamii nyingine pasipo kuchagua dini ya mtu wala kabila,”amesema.
Diwani Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki amesema kitendo cha kutoa misaada kwa familia zisizo jiweza ni ishara tosha ya kiongozi mwenye hofu ya Mungu kugusa wengine katika kutimiza maandiko ya biblia ,”amesema.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa Kata yangu wahitaji kuguswa hivi karibuni mmoja kukabidhiwa nyumba ya kisasa jambo ambalo kama jamii tunaishiwa maneno ya kusema zaidi ya kumuombea kwa Mungu ampe maisha marefu,”amesema.
