Maswa. Ongezeko la shule binafsi za mchepuo wa Kiingereza katika maeneo mbalimbali nchini limeleta fursa mpya za elimu kwa watoto, lakini pia limeibua wasiwasi kuhusu usalama wa wanafunzi wanaosafirishwa na mabasi ya shule.
Baadhi ya wazazi, wadau wa elimu na wadau wa usalama barabarani katika wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wanasema kumekuwa na tabia ya baadhi ya mabasi ya shule kubeba wanafunzi kupita uwezo wake, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya watoto endapo ajali itatokea.
Wakizungumza leo Machi 27, 2026 na Mwananchi Digital wadau wa usalama barabarani wamesema kubeba abiria kupita kiwango kilichoruhusiwa ni moja ya sababu zinazoweza kuongeza madhara makubwa wakati wa ajali.
Caroline Shayo ambaye ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa amesema mabasi ya shule yanapaswa kuzingatia idadi halisi ya viti vilivyopo ili kulinda usalama wa wanafunzi.
“Gari likijazwa kupita uwezo wake, hata mfumo wa usalama kama mikanda ya viti hauwezi kufanya kazi ipasavyo. Hii inaongeza hatari kwa abiria, hasa watoto,” amesema.
Amesema watoto ni kundi linalohitaji ulinzi maalumu barabarani, hivyo ni muhimu kwa shule na madereva wa mabasi kuhakikisha wanazingatia kikamilifu kanuni za usalama.
Kwa upande wake, Neema Kessy ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu amesema shule zina wajibu wa kuhakikisha usalama wa wanafunzi wao tangu wanapotoka nyumbani hadi wanaporejea.
“Elimu bora haiishii darasani pekee. Usalama wa mwanafunzi ni sehemu muhimu ya malezi na ustawi wa mtoto. Shule zinapaswa kuhakikisha usafiri wa wanafunzi ni salama na unazingatia taratibu zote,” amesema.
Ameongeza kuwa shule zitakapopuuzia suala la usalama wa wanafunzi zinaweza kupoteza imani ya wazazi pamoja na jamii.
Baadhi ya wazazi mjini Maswa wamesema wamekuwa wakishuhudia mabasi ya shule yakibeba wanafunzi wengi kupita uwezo wake hasa wakati wa asubuhi na jioni.
Japhet John ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma katika Shule ya St Bakhita iliyopo mjini Maswa amesema hali hiyo inawatia wasiwasi wazazi wengi.
“Tunawaona watoto wanajazwa wengi kwenye basi moja. Ikitokea ajali madhara yanaweza kuwa makubwa sana,” amesema.
Naye, Elias Mabula ambaye ni mlezi wa mwanafunzi anayesoma Shule ya Dekapoli amesema kuwa utekelezaji wa sheria unapaswa kuwa mkali ili kuzuia uzembe unaoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.
“Sheria zipo kinachohitajika ni usimamizi madhubuti,mabasi ya shule yanapaswa kubeba wanafunzi kulingana na uwezo wakena kuhakikisha watoto wanakaa kwenye viti kwa usalama,”amesema.
Mtaalamu wa usalama wa watoto, Basila Bruno amesema utekelezaji wa sheria ni muhimu ili kuzuia uzembe unaoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.
“Sheria zipo, kinachohitajika ni usimamizi madhubuti. Mabasi ya shule yanapaswa kubeba wanafunzi kulingana na uwezo wake na kuhakikisha watoto wanakaa kwenye viti kwa usalama,” amesema.
Akizungumzia suala hilo makamu mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani wilayani Maswa, Mercy Emanuel amesema kuwa kutokana na hali hiyo amezitaka mamlaka husika, likiwemo Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani pamoja na wasimamizi wa elimu, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mabasi ya shule.
“Kwa kuzingatia usalama wa wanafunzi katika usafirishaji ni jukumu la pamoja la shule, wazazi na mamlaka za usimamizi wa barabara, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira salama,”amesema.
Waonya kujaza wanafunzi kupita uwezo kwenye mabasi ya shule