Iringa. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuongoza maziko ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi.
Maziko hayo yatafanyika Machi 31, 2026, katika Kijiji cha Idodi, Wilaya ya Iringa, na yatahudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jumamosi, Machi 27, 2026, nyumbani kwa marehemu, eneo la Gangilonga, Manispaa ya Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema mwili wa Lukuvi utawasili mkoani Iringa kesho, Jumapili, Machi 29, 2026, na utapelekwa nyumbani kwake Gangilonga kwa ajili ya kulala.
Amesema Jumatatu, Machi 30, 2026, asubuhi, mwili huo utatolewa nyumbani na kupelekwa katika Kanisa Katoliki Kihesa, lililopo katika Manispaa ya Iringa, kwa ajili ya misa, na wananchi watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.
“Baada ya ibada na shughuli ya kuaga mwili, msafara utaanza safari kuelekea Kijiji cha Idodi kwa maandalizi ya mwisho ya mazishi,” amesema Kheri James.
Ameongeza kuwa maziko rasmi yatafanyika Jumanne, Machi 31, 2026, katika Kijiji cha Idodi, yakiongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Mkoa wa Iringa, pamoja na Watanzania kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli hizo za kitaifa, ili kumuenzi marehemu kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa.
Sambamba na hilo, maandalizi ya eneo la maziko yanaendelea katika Kijiji cha Idodi, ikiwamo kazi ya kuandaa kaburi atakapopumzishwa kiongozi huyo.
