NGUVU imeongezeka Yanga baada ya mastaa baadhi kurejea kikosini na kati yao wanaweza wakawa sehemu ya mechi dhidi ya Tanzania Prisons, inayotarajiwa kupigwa Aprili 4, kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji Prince Dube mwenye mabao sita na beki wa kati Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’, waliumia mechi dhidi ya Azam FC iliyomalizika kwa suluhu, Uwanja wa Benjamin Mkapa na sasa wamepona na wataanza kuendelea kuitumikia timu hiyo pale ligi itakaporejea.
Wakati huohuo, Chadrack Boka na Edmund John ambao walikaa nje kwa muda mrefu na wenyewe wataungana na wenzao katika mazoezi ya timu yanayotarajia kuanza Machi 30, 2026.
Mechi mbili za Yanga dhidi ya Mtibwa 1-1 Yanga Machi 21, Uwanja wa Jamhuri Dodoma na TRA United 0-0 Yanga iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, mastaa hao wote walikosekana.
Kurejea kwao kumeonekana kuwa na umuhimu mbele ya mastaa wa zamani wa klabu hiyo, kuona nguvu inaenda kuongezeka hasa mechi za mwisho zinazokwenda kuamua ubingwa wa msimu huu.
Yanga bado inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza michezo 16, wakiwa pointi saba mbele ya Simba ambao wamecheza michezo miwili nyuma.
Mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Chambua amesema:”Wanapocheza pamoja Laurindo Dilson Depu akae eneo la kufunga na Dube awe huru wa kuzunguka uwanjani mabao lazima yatapatikana mengi.
Aliongeza kuwa, “Dube na Depu kila mmoja ana mabao sita, hivyo kuumia kwao mabao 12 yalikuwa nje. Hilo ni pigo kitendo cha kurejea Dube kina maana ya kwenda kupata mabao mengi.”
Kwa upande wa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Said Bahanuzi amesema: “Mechi za mzunguko wa pili zinakwenda kuamua nani atakuwa bingwa wa msimu huu, hivyo kurejea kwa kwa Dube, Depu, Bacca na wachezaji wengine kikosi kinakwenda kuwa na nguvu.”
Ukiachana na mastaa waliopona majeraha, wengine watakao kuwa nje muda mrefu ni Job aliyekuwa panga pangua kikosi cha kwanza na alitengeneza kombinesheni nzuri na Bacca, ambapo walishirikiana kuipa Yanga ubingwa kwenye misimu minne mfululizo.
Pia, mchezaji mwingine staa wa Yanga aliyepo nje ni Clement Mzize ambaye ndani ya misimu miwili nyuma alifunga mabao 20 na asisti 11 (2024/25) mabao 14, asisti nne na 2023/24 mabao sita, asisti saba. Hata hivyo taarifa zinasema kuwa kwa upande wa Depu anaweza kurejea uwanjani muda wowote kuanzia sasa.
