KOCHA wa zamani wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema hakuna mchawi yeyote kwenye kikosi cha Yanga bali timu hiyo ilichemka kwenye usajili wa msimu huu.
Hivi karibuni kumekuwa na mjadala kuhusiana na kiwango cha Yanga ambao timu hiyo pamoja na kwamba inaongoza ligi lakini imeshatoka sare kwenye michezo minne hadi sasa baada ya kucheza mechi 16.
Kuanzia usajili mkubwa uliofunguliwa Agosti mwaka jana na dirisha dogo la Januari Yanga imefanya usajili wa wachezaji 15 lakini Mbrazili huyo anasema ni watatu tu walistahili kuwa kwenye kikosi hicho.
Katika dirisha kubwa Yanga iliwashusha mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Nizar Abubakar ‘Ninju’; viungo wakiwa Moussa Bala Conte, Offen Chikola, Mamadou Doumbia, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’, Lassine Kouma na Celestin Ecua wakati mshambuliaji akiwa Andy Boyeli ambao wote ukiacha Tshabalala wameshindwa kuwika.
Dirisha la Januari ikawaongeza wengine sita ambao ni kipa Hussein Masalanga; viungo ni Buba Jammeh, Mohammed Damaro, Allan Okello huku washambuliaji ni Emmanuel Mwanengo na Laurindo Aurelio ‘Depu’.
Hapo ndipo alipoanzia kocha Roberto ambaye aliwahi kuifundisha Simba akisema Yanga kwenye kundi hilo la wachezaji 15 ilipata watatu pekee ambao waliingia kwa haraka kwenye kikosi cha kwanza ambao ni Tshabalala, Depu na Okello.
Robertinho ambaye aliwahi kuwindwa na Yanga amesema hatua ya wachezaji 12 wa timu hiyo kushindwa kutoa ushindani wa haraka kwa wale ambao waliwakuta lazima itaitingisha timu, akisema ni lazima uongozi wa klabu hiyo urudi chini na kujiuliza wapi ilikosea.
“Nilikuwa hapo wakati wote timu ambayo ilikuwa inatishia mafanikio ya Simba, ilikuwa ni Yanga ambao kitu kikubwa ilikuwa ni namna walivyokuwa wanaboresha kikosi chao wakati wanapofika dirisha la usajili, ilikuwa inaonekana kuna hesabu nzuri zinafanyika lakini sasa mambo ni tofauti,” amesema Robertinho.
“Nimeangalia msimu huu nimeshangaa sana kuona kwenye wachezaji wengi ambao waliwasajili kuna watatu tu ndio wameingia kikosi cha kwanza, namuona Tshabalala, yule mshambuliaji kutoka Angola (Depu) na Okello (ambaye hata hivyo bado hana nafasi ya kudumu).
“Wengine viwango vyao vimeshindwa kuwapa ushindani wale ambao waliwakuta, unajua iko hivi kwenye timu unapoleta mchezaji mpya anatakiwa kumpa ushindani yule anayemkuta kwenye nafasi watakayokuwa wanashindania sasa unapoona wale wanaokuja wanashindwa kufanya hivyo hapo lazima uongozi wao ukae chini ujiulize kitu gani kimesababisha amesema kocha huyo wa zamani wa Vipers ya Uganda.
Katika wachezaji 15 ambao waliwasajili dirisha hili imeshawatema watano ambao wanne iliwatoa kwa mkopo ambao ni Conte, Doumbia, Chikola na Ecua huku Boyeli ambaye alikuja kwa mkopo akirudishwa kwenye klabu yake kuitokana na kiwango chake kushindwa kukubalika.
Robertinho amesema licha ya Yanga kukumbana na changamoto hiyo ya kutosajili sawasawa, lakini bado timu hiyo ina kikosi imara ambacho kimeendelea kulinda kiwango chao ikiwa juu ya msimamo huku ikiwa haijapoteza.
“Huwezi kusema Yanga wameshuka ubora moja kwa moja, angalia bado wanaongoza ligi lakini pia ni moja kati ya timu mbili ambazo hazijapoteza mchezo wowote, hii ina maana kwamba wana kikosi imara, ilitakiwa timu zingine inazokutana na Yanga ziifunge ili uonyeshe kushuka kwao lakini hilo limeshindikana.”
