Kutoka urembo hadi siasa: Safari ya Dorcas Francis isiyoyumba

Dar es Salaam. Wakati wengi wakiamini tasnia ya urembo ni lango la umaarufu na mitindo pekee, kwa Dorcas Francis imekuwa zaidi ya hapo.

Ni safari iliyomtoa kwenye majukwaa ya mitindo hadi kwenye medani za siasa na diplomasia, akibeba ndoto ya kuhamasisha wanawake kusimama imara na kupigania nafasi zao bila kuyumba.

Dorcas siyo jina jipya kwa wale wanaofuatilia tasnia ya urembo nchini. Lakini nyuma ya umaarufu huo kuna simulizi ya mwanamke aliyethubutu kuvuka mipaka ya ndoto zake za awali na kujitengenezea njia katika ulimwengu unaochanganya ubunifu, uongozi na siasa.

Safari yake inaanzia katika utoto uliojaa ndoto na hamasa ya ubunifu. Anakumbuka akiwa msichana mdogo aliyependa sana mitindo na urembo, jambo lililomfanya kuvutiwa na mavazi na namna watu wanavyojipamba.

“Tangu nikiwa mdogo nilijua ninachotaka,” anasema Dorcas kwa kujiamini, akisimulia kumbukumbu ya utotoni alipokataa kuvaa viatu alivyonunuliwa na baba yake kwa sababu moyo wake ulikuwa kwenye viatu vyeupe alivyovitamani.

Kwa wengi, tukio hilo lingeonekana dogo, lakini kwake lilikuwa ishara ya mwanzo wa msimamo wa kuamini kile anachokitaka.

Katika familia yao, majarida na magazeti yalikuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Baba yake alipenda kununua magazeti na majarida mbalimbali, na humo ndipo Dorcas alipokutana kwa mara ya kwanza na ulimwengu wa mitindo.

Anasema alipenda kuangalia mitindo aliyokuwa akiiona katika majarida ya kimataifa, hasa Vogue Magazine, jambo lililomfanya kuanza kuota ndoto za kuwa sehemu ya tasnia hiyo.

Hakubaki kuota tu. Alianza kuchora michoro ya mavazi, kubuni mitindo na kujifunza taratibu za tasnia ya urembo kwa kufuatilia wabunifu na wanamitindo waliokuwa wakifanya vizuri.

Shuleni na hata alipofika chuo kikuu, Dorcas alianza kujijengea mtindo uliomtofautisha na wengine. Wengi walimwona kama mwanamitindo hata kabla hajaanza rasmi safari hiyo.

Hata hivyo, kusimama mbele ya watu haikuwa rahisi kwake mwanzoni. Alikuwa na hofu ya majukwaa na kuonekana hadharani.

Lakini hatua moja ilibadili mwelekeo wa maisha yake. Alipopata nafasi ya kushiriki mashindano ya urembo yaliyofanyika katika eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, aliamua kujaribu bahati yake. Ajabu ni kwamba aliibuka mshindi, ushindi uliompa ujasiri mpya na kumfungulia milango katika tasnia ya urembo.

Baada ya hapo, Dorcas aliingia zaidi katika ubunifu wa mavazi na mitindo, akianza kushirikiana na washiriki wa mashindano mbalimbali ya urembo nchini.

Miongoni mwa mafanikio yake ya awali ni kushiriki katika ubunifu wa mitindo kwa washiriki wa mashindano ya Miss Tanzania, akiwemo mshindi wa mwaka 2007. Hatua hiyo ilianza kujenga jina lake taratibu katika tasnia ya urembo.

Kuunganisha urembo na maisha halisi

Licha ya mafanikio katika tasnia hiyo, Dorcas hakutaka ndoto zake ziishie kwenye majukwaa ya mitindo pekee.

Akiwa msomi wa Mahusiano ya Umma na Utangazaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na taaluma ya uchumi na biashara ya kimataifa, aliamua kupanua upeo wake katika maeneo mengine ya maisha.

Baada ya kupata ajira mkoani Mtwara, alijikuta akilazimika kusawazisha kazi yake rasmi na wito wake wa ubunifu.

Ingawa majukumu yalikuwa mengi, hakuwahi kuacha shughuli za ubunifu. Aliendelea kubuni mavazi, kushiriki matukio ya urembo na kujenga mtandao wa watu ndani na nje ya tasnia hiyo.

Kadiri muda ulivyopita, aligundua kuwa urembo unaweza kuwa jukwaa la kuleta mabadiliko katika jamii, hasa kwa wasichana na wanawake vijana.

Mwaka 2022 ulikuwa hatua nyingine muhimu katika safari yake. Alishiriki katika majukwaa ya kimataifa ya urembo na hapo ndipo alipoanza kutambua pengo kubwa la majukwaa ya kuwawezesha wasichana nchini.

Kutokana na hilo, aliamua kuanzisha mfumo wa kusaidia kukuza vipaji vya wasichana.

Kwa sasa, Dorcas ni mkurugenzi wa Miss Tanzania kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo anasimamia na kuandaa washiriki wanaokwenda kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Anasema jukumu hilo linahitaji uvumilivu, ubunifu na rasilimali, lakini ameamua kulisimamia kwa dhamira ya kuona wasichana wengi wakipata fursa.

“Changamoto zipo nyingi, ikiwemo mtaji, lakini ninachoamini ni kuanza na wazo na kulisimamia,” anasema.

Kwa Dorcas, maisha si ya kusubiri mazingira kuwa mazuri, bali ni ya kuanza na kile kilichopo.

Hatua kuelekea kwenye siasa

Safari yake haikuishia kwenye tasnia ya urembo. Kadiri alivyozidi kujijenga kijamii, aligundua kuwa masuala ya maendeleo ya jamii, wanawake na vijana yanahitaji sauti katika ngazi za maamuzi.

Hapo ndipo alipoanza kuingia katika siasa. Katika safari yake ya kisiasa, amewahi kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufikia hatua ya kuwania ujumbe wa Kamati Kuu katika uchaguzi uliofanyika Januari 2025, ingawa hakufanikiwa.

Baada ya wimbi la wanachama wengi wa Chadema kutimkia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), naye alikuwa miongoni mwao, na Chaumma kilimteua kugombea ubunge katika Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, hakufanikiwa.

Ingawa hatua hiyo iliwashangaza baadhi ya watu waliomzoea kwenye tasnia ya urembo, kwake ilikuwa hatua ya kawaida katika safari yake ya uongozi.

Anaamini wanawake wanaweza kufanya vizuri katika siasa bila kuacha utambulisho wao katika nyanja nyingine.

Katika safari yake yote, Dorcas anasema jambo moja linalomuhusu zaidi ni kuwainua wanawake.

Anatumia majukwaa yake kuhamasisha wanawake vijana kujiamini, kuthamini utu wao na kupigania ndoto zao kwa njia halali.

Anapinga tabia ya baadhi ya wanawake kutumia miili yao kama njia ya kufanikisha malengo.

“Usifanye hivyo. Inakushusha heshima yako,” anasema kwa msisitizo.

Dorcas anaamini mwanamke ana uwezo wa kufanikiwa kwa kutumia akili, bidii na ubunifu bila kujidhalilisha.

Pia anaamini imani ya kiroho ni nguzo muhimu katika maisha yake.

“Mungu ndiye nguvu yangu. Naamini ukiwa na wazo na ukalifanyia kazi, Mungu hufungua njia,” anasema.

Leo, Dorcas Francis anaendelea kujenga daraja kati ya urembo, ujasiriamali na siasa.

Maisha yake ni simulizi ya mwanamke aliyekataa kufungwa na mipaka ya jamii na badala yake kuchagua kuandika hadithi yake mwenyewe, huku akitamani kuona wanawake wengi zaidi wakisimama imara na kuamini uwezo wao.

Safari yake ni kielelezo cha ujasiri na uthabiti wa mwanamke anayethubutu kuvunja minyororo ya dhana potofu na vikwazo vilivyowekwa na jamii kwa muda mrefu.

Badala ya kukubali kuongozwa na matarajio ya wengine, aliamua kusimama imara na kutengeneza njia yake mwenyewe, akiamini kuwa kila mwanamke ana haki ya kuishi ndoto zake bila hofu wala kusitasita.

Kupitia mapambano, mafanikio na changamoto alizokutana nazo, simulizi yake inatoa mwanga wa matumaini kwa wanawake wengi wanaotafuta sauti na nafasi yao katika jamii. Ni hadithi inayohamasisha ujasiri, kujithamini na dhamira ya kubadilisha simulizi la maisha yao.