Morogoro. Serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa maziwa nchini, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje unaogharimu zaidi ya Sh23 bilioni kila mwaka.
Takwimu zinaonyesha Tanzania huagiza wastani wa lita milioni 11.6 za maziwa, licha ya kuwa na idadi kubwa ya mifugo. Changamoto ya ubora wa maziwa yanayozalishwa ndani imekuwa miongoni mwa sababu kuu.
Akizungumza na Mwananchi baada ya mafunzo ya tasnia ya maziwa kwa wakaguzi yaliyofanyika Morogoro, Msajili wa TDB, Profesa Msalya amesema Serikali imejipanga kuhakikisha maziwa yanayozalishwa yanakuwa bora na salama kwa matumizi ya binadamu.
Amesema changamoto za ubora zinatokana na kuchanganya maziwa na maji, matumizi ya vyombo visivyo salama na ukosefu wa mifumo rasmi ya ukusanyaji na usindikaji.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa maziwa yanayozalishwa hapa nchini yanakidhi viwango vya ubora ili kurejesha imani ya watumiaji na kupunguza utegemezi wa maziwa kutoka nje,” amesema Profesa Msalya.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Profesa George Msalya akizungumza jambo katika mafunzo ya wakaguzi wa tasnia ya maziwa iliyofanyika Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Ameeleza mikakati hiyo inahusisha kuongeza uzalishaji, kuimarisha ukusanyaji na usindikaji, pamoja na kutoa elimu kwa wadau wote wa mnyororo wa thamani.
Profesa Msalya amesema uzalishaji nchini umeongezeka kutoka lita bilioni 3.9 mwaka 2025 hadi bilioni 4.01 mwaka 2026. Hata hivyo, kati ya ng’ombe zaidi ya milioni 39 waliopo nchini, asilimia 90 ni wa asili wenye uzalishaji mdogo, hivyo jitihada zinafanyika kuboresha mifugo.
Serikali pia imetenga Sh216 bilioni kwa kampeni ya chanjo ya mifugo (2025-2030) ili kupunguza magonjwa na kuongeza uzalishaji.
Katika kuimarisha miundombinu, Profesa Msalya amesema Serikali imehamasisha ujenzi wa viwanda 188 vya kusindika maziwa na kuongeza vituo vya kukusanyia kutoka 200 hadi 269 katika miaka sita iliyopita. Aidha, imeondoa baadhi ya kodi ikiwemo ushuru wa forodha na VAT kwa vifaa vya tasnia hiyo.
Ameongeza kuwa kuna mradi wa miaka 10 (2025-2035) wenye thamani ya Sh520 bilioni wa kuboresha tasnia ya maziwa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unahusisha ununuzi wa ng’ombe bora 17,200, ujenzi wa vituo 150 vya kukusanyia maziwa na uwekezaji katika maji na malisho.
Kupitia mradi huo, wafugaji watanufaika na mikopo nafuu, mafunzo ya kisasa na pembejeo bora. Pia, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetenga zaidi ya Sh30 bilioni kwa kuwawezesha wafugaji na wawekezaji.
Katika sekta ya elimu, mpango wa unywaji maziwa shuleni unatarajiwa kufikia shule 5,000 ifikapo 2030 ili kukuza lishe na kuongeza soko la ndani.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mteule wa Maziwa kutoka Siha, Hawa Rajabu amesema mafunzo yaliyotolewa Morogoro kwa washiriki zaidi ya 120 yamelenga kuimarisha usimamizi wa ubora kuanzia uzalishaji hadi usambazaji.
“Tumepata mbinu za kuwafundisha wafugaji kuhusu usafi wa kukamua, lishe bora ya mifugo na matumizi sahihi ya vifaa ili kuhakikisha maziwa yanakuwa salama kwa matumizi,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya changamoto ni uchafuzi wakati wa kukamua, ikiwemo kutumia mikono isiyo safi badala ya mafuta maalumu.
Mkazi wa Morogoro, Sophia Mapunda amesema aliwahi kupata hasara baada ya kununua maziwa yaliyoharibika. “Niliwahi kununua maziwa lakini yaliharibika baada ya kuchemsha,” amesema.
Naye Thadei Hafigwa amesema elimu kwa wafugaji ni muhimu kubadili mtazamo wa wananchi wanaokimbilia maziwa ya nje.
Kwa mujibu wa Profesa Msalya, utekelezaji wa mikakati hiyo unalenga kufikia uzalishaji wa lita bilioni 5 ifikapo 2035 na kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa maziwa kutoka nje.
