Mpina: Umafia wa Lukuvi uliniokoa

Dodoma. Wakati mwili wa William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) ukiagwa bungeni Dodoma, Mbunge wa zamani wa Kisesa, Luhaga Mpina amesimulia kumbukumbu juu yake kuwa mnadhimu huyo wa Bunge alimnusuru kutimuliwa au kuvuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi huo ungefikiwa na CCM endapo Mpina angetimiza azma yake ya kuipigia kura ya Hapana, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12 iliyokuwa imewasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango wa wakati huo, marehemu Dk William Mgimwa.

Wakati Mpina, ambaye sasa ni mwanachama wa ACT-Wazalendo, akieleza hayo, Mbunge mwingine wa zamani wa Kawe na Viti Maalumu, Halima Mdee, yeye ametoboa siri za bajeti za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Lukuvi kuungwa mkono na upinzani.

Mdee amesema Lukuvi alikuwa akichukua ushauri na mapendekezo ya hotuba za kambi ya upinzani bungeni na kwenda kuvifanyia kazi kwa vitendo.

Familia ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Marehemu, William Lukuvi wakati wa kuaga mwili wa mpendwa wao leo Ijumaa Machi 27, 2026 katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Pia, alishughulikia migogoro mbalimbali ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mpina na Mdee wametoa simulizi hizo kwa nyakati tofauti katika kipindi ambacho Taifa linaomboleza kifo cha Lukuvi (70), aliyefariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mshtuko wa moyo.

Hadi anafariki dunia, Lukuvi alikuwa mbunge wa Ismani, Mkoa wa Iringa, nafasi aliyoishikilia kwa miaka 31 tangu alipochaguliwa mara ya kwanza mwaka 1995 katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi.

Leo Ijumaa, Machi 27, 2026, Mpina ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi akizungumza na Mwananchi amesimulia sababu iliyotaka kumfanya kuikataa bajeti hiyo, kwamba Mpango wa Maendeleo ulikuwa unaeleza Serikali itatenga asilimia 35 ya bajeti kutelekezwa kwenye maendeleo lakini yenyewe ikatenga asilimia 22.

“Kwa kuona vile mimi nilitaka kupiga kura ya Hapana,” amesema Mpina.

Amesema huenda angeweza kushughulikiwa ndani ya chama kwa kuikataa bajeti ya Serikali, lakini kilichomuokoa asifukuzwe ubunge ni busara na maarifa aliyokuwa nayo Lukuvi ambaye alikuwa mnadhimu wa Bunge.

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Marehemu, William Lukuvi likiwasili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

“Pale kilichofanyika ulikuwa ni umafia lakini ambao ulikuwa na matokeo mazuri kwangu. Kumbuka Mzee aliniita nje wakati nimeshajiandaa kusema Hapana. Niligoma nikitaka anipe muda kwanza nipige kura lakini akasema tuongee dakika chache,” anasema Mpina.

“Tulipotoka kuzungumza, mara milango ya Bunge ikafungwa ghafla na nilipotaka kuingia walinizuia kabisa, lakini yeye akaingia. Kwa wakati ule niliumia sana, lakini baadaye nilimshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi na leo nina maumivu kwamba tumempoteza mtu,” amesema.

Mpina amesema kipindi hicho alikuwa mbunge kama wengine, hakuwa amepata nafasi ya naibu waziri wala waziri, hivyo angefukuzwa ubunge wasifu wake usingekuwa kama sasa.

“Kumbuka Lukuvi alishakuwa mbunge mzoefu na waziri wa muda mrefu, kama angekuwa mwenye moyo wa korosho huenda angemwacha kijana aangamie, lakini busara zilipomuishia akatumia upande wa pili na kupata matokeo aliyotarajia.

“Kweli siyo kila kisu kinabebwa kwa ajili kuumiza watu, wakati mwingine kinaweza kukusaidia kukata kamba zilizojifunga miguuni mwako kwa bahati mbaya na kama zikiachwa usingeendelea na safari yako.

“Ndiyo hapo unajiuliza, hivi hawa wanasiasa unawaelewa kweli, ukiwakuta wanararuana kwenye majukwaa, we nunua maji kisha kaa pale ukunje mguu na kuanza kunywa, wakimaliza waombe lifti muondoke.

Mpina amemuombea malalo yenye heri Lukuvi ambaye amemaliza mwendo kabla ya kushuhudia ndoto zake (Mpina) zikitimia.

Kwa upande wake Mdee, amesema uwezo wa Lukuvi ndani na nje ya Bunge ulikuwa mkubwa na ndiye waziri pekee ambaye alikuwa akichukua maoni na ushauri wa hotuba za upinzani na kuzifanyia kazi.

Mdee amesema wakati anaingia Wizara ya Ardhi alikuta migogoro mingi maeneo mbalimbali nchini ya wakulima na wafugaji, wawekezaji kuhodhi maeneo na alitumia uzoefu wake na uchapakazi wake kuishughulikia na kwa sehemu kubwa alifanikiwa.

“Kwa kweli watu wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, basi huyo ni Lukuvi. Ni mawaziri wachache sana waliokuwa wanachukua mawazo ya upinzani na kuyafanyia kazi na naweza kusema tangu aondoke wizara ya ardhi, hakuna waziri aliyeweza kuvaa viatu vyake kwa vitendo hata kwa asilimia 30.”

Viongozi mbalimbali wakiwa katika viwanja vya Bunge, Dodoma wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi.

Katika kusisitiza hilo, Mdee amesema: “Hivi unakuwa na waziri, anachukua mapendekezo yetu (ya upinzani) na kuyafanyia kazi, sasa unaanzaje kuipinga bajeti yake? Na unajua tangu ameondoka, sijaona waziri aliyevaa viatu vyake. Sasa wengine waige mfano wake.”

Mdee amesema hata akiwa mnadhimu wa Bunge aliitendea haki nafasi hiyo, kwani alikuwa anaangalia hoja za pande zote za Serikali na za upinzani na kushauri, japo si kwa kiwango kikubwa.

 “Lakini alihakikisha anasimama katikati akiamini wote ni wawakilishi wa wananchi,” amsema

Mbunge wa Nzenga (CCM) Mjini Hussein Bashe amesema kilichokuwa kikimsaidia Lukuvi hata bajeti zake kupita bila kupingwa ni kwa sababu ya heshima aliyokuwa amejijengea kwenye mhimili.

Bashe amesema Lukuvi alikuwa amejijengea mahusiano mazuri pia hata kwa wabunge vijana ambao walikuwa na mihemko lakini alikuwa karibu nao na hivyo wakajenga heshima kwake.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ametaja kilichombeba hata kuwa mtuliza joto bungeni ni kwamba aliipenda kazi yake na kuijua na ndiyo maana alifanikiwa kwa kila jambo alilolifanya bungeni.

Kwa upande wake Mbunge wa Mtama Nape Nnauye amesema Marehemu Lukuvi alikuwa mfano mzuri kwa viongozi vijana kutokana na heshima aliyokuwa amejiwekea ya kufanya kazi kwa bidii kwani hakuwa mbovu.

Nape amesema kitendo hicho kilipelekea kuaminiwa bungeni na kila alilolokuwa akilisema lilikuwa lazima liungwe mkono na wabunge wote wakiwemo wa upinzani.

Leo Machi 27, 2026 Muhimili wa Bunge umeuaga mwili wa Lukuvi ambaye hadi anafariki dunia, ndiye alikuwa mbunge mkongwe kuliko wote, akiwa amehudumu chini ya maspika Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anne Makinda, Job Ndugai, Dk Tuli Ackson na Mussa Zungu.

Shughuli ya kuaga mwili wake iliyofanyika baada ya misa, iliongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambapo zilitolewa hotuba mbalimbali kuhusu maisha na utumishi wake.

Pamoja na wote waliozungumza, mwakilishi wa familia, Mosi Lukuvi ambaye ni mdogo wa marehemu amemwombea msamaha na upatanisho kwa watu wote ambao huenda aliwahi kukwaruzana nao wakati wa uhai wake, akisisitiza alikuwa binadamu mwenye upungufu kama wengine.

Mosi amesema licha ya mengi mazuri yanayosemwa baada ya kifo, ni muhimu kukumbuka marehemu pia alipitia changamoto mbalimbali katika utumishi wake, hasa katika uwanja wa siasa.

“Mwanadamu akifariki, mengi mazuri husemwa. Hata hivyo, tukumbuke kwamba alikuwa binadamu; kuna wakati katika utumishi wake alikwaruzana na wenzake kazini na tunatambua kwamba siasa ni mchezo wa aina yake.

“Hivyo, bila shaka, katika kipindi cha utumishi wake aliwahi kukwaruzana kwa namna moja au nyingine…huenda ameondoka bila kupata nafasi ya kuomba msamaha kwa wale aliowakosea. Sisi kama familia, kwa niaba yake, tunaomba msamaha na upatanisho kwa wote ambao aliwahi kuwakosea katika harakati zake za kisiasa na maisha yake kwa ujumla. Vilevile, kwa wale ambao waliwahi kumkosea, sisi kama familia tunawasamehe kwa niaba yake,” amesema.

Aidha, Mosi amesema kaka yake hakuamini katika siasa za upendeleo au kuwa na mbuyu, bali alisisitiza mafanikio yanatokana na juhudi binafsi.

“Wakati mwingine kwenye siasa kuna lugha kwamba wengine wana mibuyu, lakini Mheshimiwa William hakuwa na mbuyu. Alikuwa akisema ‘Godfather’ ni wewe mwenyewe na kazi zako,” amesema Mosi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Tulia amesema Lukuvi hakuwa na choyo cha maarifa na hakuwa mtu wa kufurahia baya limpate mwingine na kwamba kila mmoja achukue yale aliyojifunza kwake na aangalie namna atakavyomuenzi.

“Mengi yamesemwa hapa, mimi nitasema moja tu kwamba hakuwa na choyo cha maarifa katika maeneo yote. Ukitaka maarifa ya namna ya kufanya siasa safi utayapata kwake, ukitaka maarifa ya namna ya kutokuwa mwizi utajifunza kwake.

Ukitaka kuwa mbunge bora utajifunza kwake, na ukitaka kuwa mbunge wa muda mrefu kama yeye alivyokuwa utajifunza kwake. Hakuwa na choyo, kwa maana kwamba katika hayo maeneo machache niliyoyataja angeweza kukueleza kama ungetaka,” amesema Dk Tulia.

Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, amesema atamkumbuka Lukuvi kama kiongozi mwema na mshauri wa kweli huku akikumbushia kauli yake pindi hali ilipokuwa ngumu yeye akiwa Waziri wa Fedha.

“Alikuwa nguzo kubwa katika kunieleza taratibu za Serikali ndani ya Bunge. Nakumbuka siku moja tulikutana akaniambia, ‘Mdogo wangu, tangu Uhuru hajawahi kupatikana Waziri wa Fedha bahili kama wewe.’ Kwa kweli, sijasahau maneno hayo hadi leo. Alifanya kazi yangu kuwa nyepesi kwa kushauri kwa upendo na hekima,” amesema Dk Mpango.

Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Lukuvi alikuwa mtendaji halisi wa Serikali aliyetumia maono yake na busara zake kikamilifu.

“Kwa ufupi nakiri marehemu alikuwa kiongozi aliyebeba maono mapana, busara za hali ya juu na moyo wa dhati katika kulitumikia taifa lake katika utumishi wake na nikiri kusema Mheshimiwa Lukuvi alikuwa mserekali par excellence…” amesema Zungu.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema somo la kifo cha Lukuvi limekumbusha binadamu wote kuwa wanyenyekevu na kuwa mwenye masahihisho ni Mungu peke yake.

“Lakini mtandaoni wapo wengine wakiandika ukimuangalia mtu anayeeandika hivyo, mara nyingi ameshadhulumu, si msafi, ana madeni kibao na utapeli mwingi. Somo la leo limetusaidia kuona sisi ni binadamu na safari yetu ni moja.

Mwenye masahihisho ni Mungu peke yake; Mungu ndiye anaweza kuamua nani anastahiki, wa kuweza kujua nani ananuka ni Mungu mwenyewe,” amesema Dk Mwigulu, huku akisisitiza umuhimu wa matumizi bora ya mitandao ya kijamii.

Akisoma wasifu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi amesema Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955 katika kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa Vijijini.

Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri aliyeshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na alijulikana kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi, uzalendo, pamoja na uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi.

Aliweka masilahi ya Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Dk Yonazi amesema Lukuvi alijulikana kwa mtindo wake wa kazi wa kutembelea maeneo ya miradi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Katika kudhihirisha uchapakazi wake, siku moja kabla ya umauti kumkuta, alihudhuria na kuratibu shughuli za Serikali katika vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali.

Kuhusu elimu, Dk Yonazi amesema alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970.

Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) kuanzia mwaka 1974 hadi 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa cheti cha ualimu.

Mwaka 1982–1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa (Advanced Diploma in Political Science).

Alipata Shahada ya Masuala ya Kimataifa na Diplomasia (Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy) kutoka Washington International University kuanzia mwaka 1999 hadi 2001. Baadaye alijiendeleza katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa mwaka 2008–2011.

Amesema Lukuvi alifunga ndoa Julai 28, 1990 na Germina Lukuvi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Dar es Salaam, na kujaliwa watoto watatu: Nobert, Brown na Anifisye Vanessa. Ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwaye Donovan.