Dar es Salaam. Wakati malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa dawa yakiendelea kusikika katika baadhi ya vituo vya afya nchini, imebainika sehemu ya changamoto hiyo inatokana na wagonjwa kuhitaji dawa ambazo hazijapangwa kwa ajili ya ngazi ya huduma wanazozifuata.
Hali hiyo inaonekana zaidi kwa wagonjwa wanaopata matibabu katika hospitali za juu kama za rufaa za mikoa au kitaifa, wanaporudi katika vituo vya chini kama zahanati au vituo vya afya, wanatarajia kuendelea kupata dawa zilezile walizoandikiwa, jambo ambalo mara nyingi haliwezekani.
Katika sehemu ya pili ya mahojiano maalumu yaliyofanyika Dodoma hivi karibuni, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi anasema mwongozo wa matibabu unapanga aina ya dawa kulingana na ngazi ya kituo cha huduma na huo ndio mfumo wa utoaji dawa nchini.
Anasema mwongozo huo umeainisha aina 382 za dawa na bidhaa za afya zinazotumika nchini, lakini si zote zinapatikana katika kila ngazi ya huduma.
“Kwa mfano, zahanati tunazipima kwa dawa 101, vituo vya afya 186, halmashauri 202, hospitali za rufaa za mikoa 236 na hospitali za kanda na taifa dawa hadi 290.
Taasisi maalumu kama Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Kibong’oto zinafikia hadi dawa 382 kwa sababu ya huduma maalumu wanazotoa,” anafafanua.
Anasema kutokana na mpangilio huo, si sahihi kwa mgonjwa kutarajia kupata dawa ya kiwango cha juu, kama ya saratani au baadhi ya dawa za presha, katika zahanati.
“Unakuta mtu ameandikiwa dawa ya saratani Ocean Road, halafu anatarajia dawa hiyo aipate kwenye zahanati ya kijiji. Au mgonjwa wa presha amepewa dawa katika hospitali ya rufaa, anapofika kituo cha chini anaanza kulalamika hakuna dawa,” anasema.
Kwa mujibu wa Msasi, hali hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa dawa, ilhali mfumo umezingatia usalama wa mgonjwa na utaalamu unaohitajika katika utoaji wa dawa hizo.
Anasisitiza baadhi ya dawa, hasa za magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari, zinahitaji uangalizi maalumu wa kitabibu, hivyo hutolewa katika ngazi maalumu za huduma.
“Dawa za presha ni nyeti sana. Daktari akikosea kidogo tu, inaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa. Ndiyo maana utoaji wake unaendana na kiwango cha utaalamu wa kituo,” anasema.
Pamoja na changamoto hizo, Msasi anasema hali ya upatikanaji wa dawa nchini inaendelea kuimarika, ambapo kwa wastani imefikia asilimia 88.8 Februari mwaka huu.
Anasema katika ngazi ya halmashauri upatikanaji ni asilimia 89.5, vituo vya afya 88.7 na zahanati asilimia 79, huku hospitali za kanda, taifa na maalumu zikifikia zaidi ya asilimia 93, baadhi zikiwa hadi asilimia 99.
Hata hivyo, anakiri kuwa bado kuna changamoto katika ngazi za chini, hasa zahanati, ambazo zinakabiliwa na upungufu wa dawa.
“Tunapopata malalamiko tunafuatilia kujua chanzo. Mara nyingi unakuta changamoto ipo kwenye mnyororo wa ugavi au utaratibu wa ununuzi wa dawa,” anasema.
Anaeleza Bohari ya Dawa (MSD) ndiyo mhimili mkuu wa usambazaji wa dawa nchini, lakini bado inakabiliwa na changamoto za kuwa na upatikanaji wa bidhaa kwa takribani asilimia 73 badala ya lengo la asilimia 93.
Kutokana na hali hiyo, vituo hulazimika kununua dawa nje ya MSD, jambo ambalo linaweza kusababisha ucheleweshaji hasa katika ngazi za chini zinazohitaji idhini ya mamlaka za juu.
Msasi anasema Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh200 bilioni mwaka 2023 hadi kufikia Sh398 bilioni sasa, ingawa mahitaji halisi yanafikia takribani Sh600 bilioni kwa mwaka.
Anasema pamoja na juhudi hizo, vituo vya afya pia vinachangia kupitia mapato yao ya ndani, lakini bado kuna pengo la rasilimali.
“Tunafanya jitihada kuhakikisha MSD inakuwa na dawa za kutosha muda wote, lakini pia tunaimarisha mifumo ya maoteo na ufuatiliaji ili kujua mahitaji halisi ya dawa nchi nzima,” anasema.
Anaongeza kuwa Serikali imeweka mfumo wa usambazaji unaowezesha dawa kufikishwa katika vituo kila baada ya miezi miwili, lakini ucheleweshaji wa maombi au makadirio yasiyo sahihi unaweza kuathiri upatikanaji.
Ingawa malalamiko ya ukosefu wa dawa bado yapo, Msasi anasema yamepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili hadi mitatu iliyopita, kutokana na maboresho ya mifumo ya upimaji na ufuatiliaji.
Anasema malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara, hasa ni kuhusu dawa za presha, kisukari na kwa kiwango kidogo dawa za saratani.
Anasema dawa za magonjwa ya kuambukiza kwa ujumla zinapatikana muda wote.
Katika tahadhari kwa wananchi na wataalamu, Msasi anawataka wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na kuepuka kununua dawa bila ushauri sahihi, akionya kuwa matumizi holela yanaweza kusababisha usugu wa dawa na madhara mengine ya kiafya.
“Ni muhimu mgonjwa kufika kituo cha afya, kupata uchunguzi na kupewa dawa sahihi kulingana na hali yake. Pia afuate kikamilifu maelekezo ya matumizi ya dawa,” anasema.
Aidha, anawahimiza wananchi kutoa taarifa wanapopata madhara au kutopona baada ya kutumia dawa, ili kusaidia mamlaka kufanya ufuatiliaji.
Kwa upande wa wataalamu wa afya, anasisitiza umuhimu wa kuzingatia mwongozo wa matibabu katika kuandika dawa, akieleza kuwa kuandika dawa nje ya mwongozo kunachangia wagonjwa kukosa dawa na pia kuongeza hatari ya usugu wa vimelea.
Katika hatua nyingine, Msasi anatoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika viwanda vya dawa ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Anasema kwa sasa uzalishaji wa ndani bado uko chini, hali inayoweza kuathiri upatikanaji wake, hasa kunapotokea changamoto za kimataifa kama ilivyokuwa wakati wa Uviko-19.
Msasi katika hatua nyingine, anasema mkakati wa Serikali wa bima ya afya kwa wote utasaidia kuongeza upatikanaji wa dawa kwa wananchi kwa kupunguza vikwazo vya kifedha na hivyo itamwezesha mwananchi kupata dawa kwa urahisi katika vituo vya huduma bila kujali uwezo wake wa kifedha.
Licha ya changamoto zilizopo, anasisitiza kuwa mfumo wa ugavi wa dawa nchini unaendelea kuimarika na unalingana vizuri na mifumo ya ukanda wa Afrika Mashariki, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wananchi.