Nisre Zouzoua ang’ara, Dar City yaitandika Johannesburg BAL

WAKATI Dar City ikiichapa Johannesburg Giants ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika (BAL) juzi Ijumaa kwa pointi 100-70, Nisre Zouzoua alikuwa mwiba kwa walinzi wa Wasauzi hao.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa SunBet uliopo Pretoria nchini Afrika Kusini, Zouzoua aliongoza kwa kufunga pointi 35 ambazo ni nyingi kuliko wachezaji wote.

Wakati Zouzoua akifanya balaa hilo wachezaji wengine wa Dar City, David Michineau alifuatia na pointi 27, wakati Daniel Utomi akifunga pointi 14, Deng Madut (pointi 10) na Michael Foster (pointi 5) huku pia nyota huyo akiongoza kwa kudaka mipira ya kurudi (rebound) akifanya hivyo mara 7, huku David Benoit akitoa assisti tisa wakati upande wa uzuiaji (Blocks), Hasheem Thabeet alizuia mara mbili.

Upande wa Johannesburg Giants, Jakobi Terrel alifunga pointi 26, akifuatiwa na Arinze Nino (pointi 13), Pieter Prinsloo (pointi 7) na David Lee Craing (pointi 7).

Dar City inayoshiriki mashi ndano hayo kwa mara ya kwanza, katika mchezo huo iliongoza robo tatu za kwanza kwa pointi 31-12, 26-18, 24-20, kabla ya ile ya mwisho kupoteza kwa pointi 19-20.

Jana, Dar City ilikuwa na mchezo wa pili ambapo ilicheza dhidi ya Nairobi City Thunder kutoka Kenya. Baada ya hapo, Machi 31 itacheza dhidi ya Al Ahly Ly ya Libya, kisha Aprili 3 ni dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, itamaliza Aprili 5 kukabiliana na RSSB Tigers Rwanda.

Katika ufunguzi wa mashindano hayo juzi Ijumaa, mechi ya mapema ilishuhudiwa timu ya RSB Tigers kutoka Rwanda, ilifungua dimba kwa kuichapa Al Ahly Ly ya Libya pointi 103-95.

Timu zinazoshiriki kundi hilo la Kalahari Conference ni Al Ahly Ly (Libya), Dar City (Tanzania), Johannesburg Giants (Afrika Kusini), Nairobi City Thunder (Kenya), Petro de Luanda (Angola) na RSSB Tigers (Rwanda) ambapo mechi zake zilianza Machi 27, 2026 na zinatarajiwa kumalizika Aprili 5 mwaka huu.

Kundi lingine la Sahara Conference ni Fus de Rabat (Morocco), Al Ahly (Misri), ASC Ville de Dakar (Senegal), Club African (Tunisia), JCA Kings (Ivory Coast) na Maktown Flyers (Nigeria). Michezo za kundi hili itachezwa kuanzia Aprili 24 hadi Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Ndani wa Prince Moulay Abdellah huko Rabat nchini Morocco.