Rais Samia Atoa Funzo la Uongozi Akimuenzi Lukuvi (Picha +Video)

Global Publishers
March 28, 2026
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Hayati William Vangimembe Lukuvi, akisisitiza kuwa taifa limepoteza kiongozi mzalendo, mwadilifu na mwenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza leo Machi 28, 2026 katika viwanja vya Karimjee Hall jijini Dar es Salaam, Rais Samia alimwelezea Hayati Lukuvi kama kiongozi aliyekuwa tayari kushirikisha uzoefu wake bila ubinafsi.

Alisema Lukuvi hakuwa mchoyo wa maarifa, na viongozi wengi waliopata nafasi ya kufanya naye kazi walijifunza mambo makubwa yaliyowajengea uwezo wa kiuongozi.

“Alikuwa Darasa kwa Viongozi” Rais Samia alisisitiza kuwa katika nafasi zote alizowahi kushika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikalini na Bungeni, Hayati Lukuvi ameacha alama ya utendaji bora ambayo itaendelea kuwa rejea kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Ndugu zangu, msiba huu si wa familia pekee bali ni wetu sote Watanzania. Wengi tulimfahamu, wengine tulibahatika kufanya kazi naye, na muhimu zaidi wengi waliguswa na mchango wake kupitia uongozi na utumishi wake wa muda mrefu,” alisema Rais Samia.

Kifo cha Lukuvi kimeacha pengo kubwa ndani ya serikali na siasa za Tanzania, hasa kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika utumishi wa umma.

Watanzania kutoka kada mbalimbali wameendelea kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho, wakikumbuka mchango wake katika kuimarisha utawala na maendeleo ya taifa.