Rais Samia Atoa Heshima za Mwisho kwa Hayati Lukuvi Karimjee, Dar (Picha +Video)

Global Publishers
March 28, 2026
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na wenye Ulemavu), Hayati William Vangimembe Lukuvi, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 28 Machi, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Machi 28, 2026 ameongoza mamia ya viongozi na maelfu ya wananchi kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Wenye Ulemavu), Hayati William Vangimembe Lukuvi, katika hafla ya kitaifa iliyofanyika viwanja vya Karimjee Hall jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo lililogubikwa na huzuni, Rais Samia alionekana akitoa heshima za mwisho kwa unyenyekevu mkubwa mbele ya jeneza lililobeba mwili wa marehemu Lukuvi, huku viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na wananchi wakifuatilia kwa makini.

Waombolezaji waliojitokeza walionyesha masikitiko yao, wakikumbuka mchango mkubwa wa Lukuvi katika uongozi na utumishi wa umma kwa miongo kadhaa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alimwelezea Lukuvi kama kiongozi aliyekuwa nguzo muhimu katika serikali na chama, akisisitiza kuwa alikuwa tayari kushirikisha maarifa yake kwa wengine.

“Tumempoteza kiongozi mzalendo, mwalimu wa wengi na mtu aliyekuwa tayari kuwaongoza na kuwainua wengine,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa katika nafasi zote alizowahi kushika, ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lukuvi aliacha alama ya utendaji bora na mfano wa kuigwa kwa viongozi wa sasa na vijavyo.

Rais Samia akiwafariji wafiwa mara baada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na wenye Ulemavu), Hayati William Vangimembe Lukuvi, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 28 Machi, 2026.