Rungu la Diarra ni la kumi na tano Ligi Kuu

DJIGUI Diarra jana alitangazwa kufungiwa michezo mitatu na Bodi ya Ligi baada ya kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar akiwa ni mchezaji wa 15 kukutana na rungu hilo msimu huu.

Kanuni za msimu huu za Ligi Kuu Bara zimeonekana kuwa kali huku wachezaji kadhaa wakikutana na rungu la kufungiwa na kupigwa faini ya viwango vikubwa vya fedha lakini timu kubwa za Simba na Yanga ndiyo zimeonekana kuumia zaidi.

Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) iliyokutana Machi 26, ndio imeshuha adhabu hiyo kwa Diarra kufungiwa michezo hiyo kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wa mchezo kati ya Mtibwa dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mbali na kufungiwa kipa huyo namba moja wa Yanga pia alitozwa faini ya Sh2 milioni lakini akakumbana na adhabu nyingine ya kutozwa fedha kama hizo kufuatia kosa la kuonesha kidole cha kati wakati akitoka uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Adhabu hiyo sasa itamfanya Diarra kuzikosa mechi mbili za ligi za timu yake dhidi ya Prisons nyumbani Aprili 4 na ile ya ugenini dhidi ya Pamba Jiji Aprili 8, lakini atamaliza adhabu yake kwenye mchezo wa Kombe la CRDB dhidi ya TMA Stars, Aprili 11.

Katika orodha ya jumla hadi sasa wachezaji sita walikumbana na rungu la kufungiwa mechi tano. Miongoni mwao ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga, aliyeadhibiwa kufuatia kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Mbeya City, Ibrahim Ame.

Mohamed Bakari wa JKT Tanzania alifungiwa kwa kosa la kumkanyaga beki wa Azam, Lusajo Mwaikenda huku Gabriel Mwaipola wa Mbeya City akipata adhabu sawa kufuatia kumpiga kiwiko Rajabu Mfuko wa Namungo.

Vitalis Mayanga alikumbana na adhabu ya mechi mitano kwa kosa la kumpiga kiwiko beki wa Simba, Anthony Mligo na faini ya Sh. 1 milioni.

Nahodha wa Singida Black Stars, Khalid Aucho, alifungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Sh. 1 milioni kwa kosa la kumpiga na kumsukuma Adam Adam wa TRA United.

Wachezaji wengine waliokabiliwa na adhabu ya mechi tano ni Jonathan Sowah wa Simba, aliyeadhibiwa kwa kumpiga kiwiko Himid Mao wa Azam na Allasane Kante pia wa Simba, aliyeadhibiwa kwa kumpiga teke mchezaji Feisal Salum wa Azam, kila mmoja kutozwa faini ya Sh. 1 milioni.

Kwa upande mwingine, wachezaji waliokumbana na adhabu ya mechi tatu ni Seleman Mwalimu na Abdi Banda wa Dodoma Jiji, kila mmoja akiwa na faini ya Sh. 1 milioni, Mwalimu kwa kosa la kumpiga mtu kiwiko huku Banda akiadhibiwa kwa kujirusha kutoka kwenye machela.

Mchezaji David Kameta ‘Duchu’ alikumbana na adhabu ya faini ya Sh. 1 milioni kufuatia kitendo cha kuonyesha tabia zisizokubalika uwanjani, kinachotafsiriwa kama ishara za imani za kishirikina.

Wachezaji wengine walilimwa faini kwa kutosalimia wenzao kabla ya mechi kuanza ni Andy Lobuka Bikoko (TRA), Muhsini Malima (Dodoma Jiji) na Mzamiru Yassin (TRA). Hata hivyo, asilimia kubwa ya wachezaji waliokumbana na adhabu wamekwisha maliza adhabu zao.