Samia: Tulimhitaji Lukuvi wakati huu wa migongano duniani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Taifa limepata pigo kwa kumpoteza William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) katika wakati nyeti, akieleza kuwa pengo lake litaonekana kutokana na mchango wake katika masuala ya uongozi na ushauri wa kitaifa.

Amesema uzoefu na umahiri wa Lukuvi vilihitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia migongano ya kimataifa, hali inayoweza kuathiri mwelekeo wa bei za bidhaa, huku akisisitiza kuwa alikuwa miongoni mwa viongozi waliosaidia Taifa kuelewa na kuchukua hatua sahihi kukabiliana na changamoto hizo.

Rais Samia amesema hayo leo, Machi 28, 2026 wakati akitoa salamu za rambirambi katika hafla ya kuaga mwili wa Lukuvi, jijini Dar es Salaam.

Lukuvi (70), alifariki dunia asubuhi ya Machi 25, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

Lukuvi alikuwa miongoni mwa wabunge waandamizi bungeni ambaye amekuwa mbunge wa Ismani, Mkoa wa Iringa kuanzia mwaka 1995 hadi sasa akihudumu kwa zaidi ya miaka 30. Mwili wake utazikwa Jumanne kijijini kwao Idodi, Iringa Vijijini.

Rais Samia amesema katika kipindi hiki ambacho dunia imejaa migongano na machafuko, walihitajika zaidi viongozi wenye uzoefu wa muda mrefu na waliowahi kufanya kazi katika maeneo mbalimbali, ndani ya Serikali na katika siasa.

“Tulihitaji tuendelee na mawazo na ushauri wa viongozi wa aina hii. Tulimuhitaji ndugu Lukuvi sasa kuliko jana, lakini kama nilivyosema Mungu alimpenda zaidi,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na wenye Ulemavu), William Lukuvi, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Amesema dunia imejaa misuguano na machafuko ambayo kwa vyovyote vile yatapandisha gharama za maisha, si kwa Tanzania tu bali hata duniani.

“Tayari kumeanza kushuhudiwa kupanda kwa bei za mafuta, na vivyo hivyo tutashuhudia kupanda kwa bei za bidhaa. Pia, kama vita hii itaendelea, tunategemea kuwa na mdororo wa uchumi duniani.

“Mambo haya yanahitaji umakini katika kufanya maamuzi ya uongozi wa nchi yetu. Tumwombe Mwenyezi Mungu haya yamalizike ili tuende vizuri, lakini kwa uzoefu aliokuwa nao mheshimiwa Lukuvi, tulimhitaji zaidi sasa kuliko wakati wowote,”amesema na kuongeza;

“Tulimhitaji ndugu yetu huyu kwa sababu tunamkumbuka kwa moyo wake wa upendo na mahusiano mazuri aliyojenga katika jamii, pamoja na utayari wake wa kushirikiana na kushauriana na makundi mbalimbali.

Rais Samia amesema hayo ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa vita katika ukanda wa Mashariki ya Kati, vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambavyo vinatishia hatari ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari ya kukumbwa na athari hiyo, kwani baadhi ya nchi zilizoathiriwa ndizo chanzo kikuu cha mafuta yanayoagizwa nchini.

Amesema ili kuendeleza mazuri aliyoyafanya, ni vyema kutambua kuwa uongozi ni dhamana na ni wajibu wa utumishi wa umma kwa uaminifu na moyo wa kujitolea.

“Huo ndiyo urithi aliotuachia mpendwa wetu marehemu Lukuvi, na kama alivyosema baba paroko kwamba katika utendaji wa Serikali nafasi hii lazima izibwe na si mbadala. Mbadala ni pale unaposema huyu aondoke badala yake akae huyu. Lakini kilichotokea hapa ni paukwa pakawa,” amesema.

Marehemu Lukuvi alikuwa mwenyekiti wa viongozi waliotumikia Taifa kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM), Serikali na Bunge, kama wasifu wake ulivyoelezwa.

Amesema katika nafasi zote za utumishi alizowahi kushika, alijipatia uzoefu na aliacha alama ya utendaji bora na uwajibikaji, na kwa uzoefu wake hakuwa mchoyo wa maarifa.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema marehemu alifanya kazi kwa ushirikiano na viongozi mbalimbali katika nafasi tofauti alizowahi kuzishika, na alikuwa mzalendo aliyejitolea kwa dhati kulitumikia Taifa kwa moyo, akiweka mbele maslahi ya nchi.

“Kwa hakika, namna bora zaidi ya kumuenzi mpendwa wetu marehemu William Lukuvi ni kuendeleza maono yake na kuiga mfano wake bora wa kuchapa kazi kwa bidii, uadilifu na kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa uzalendo,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema alimfahamu Lukuvi alipoingia bungeni mwaka 2020, na tangu hapo walifanya kazi pamoja kama mawaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wataendelea kumkumbuka kutokana na utendaji wake uliokuwa na umahiri mkubwa wa uwajibikaji na uzalendo.

“Nilipoingia bungeni mwaka 2000, kwa miaka 20 tokea wakati huo hadi nilipokwenda Zanzibara mwaka 2020 tulikuwa pamoja kama mawaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya mzee hayati Mkapa, mzee Kikwete na hayati mzee Magufuli.

“Yeye aliendelea kuwa katika baraza la mawaziri hadi awamu hii ya Rais Samia kutokana na utendaji wake wa kazi ambao ulikuwa na umahiri mkubwa, uwajibikaji na uzalendo. Hivyo tutaendelea kumkumbuka kwa ushirikiano wake katika kazi na kama rafiki wa karibu,” amesema.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Lukuvi alifikwa na umauti akiwa kazini.

“Siku mauti ilipomfika, tayari alikuwa na ratiba nyingine za kazi, ikiwemo kukutana na Kamati ya Bunge na kikao kazi ambacho alikuwa ameandaa mwenyewe cha kukutana na wakuu wa mikoa,” amesema.

Familia ya William Lukuvi imesema msiba huo si tu wa kumpoteza kiongozi wa umma, bali pia ni pigo kubwa la kumpoteza nguzo kuu ya familia.

Hayo yamesemwa na mtoto wa marehemu, Nobert Lukuvi, wakati akisoma salamu za familia kwa waombolezaji waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Nobert, ambaye ni mmoja wa watoto watatu wa Lukuvi, amesema kwa wengi marehemu alijulikana kama waziri, mbunge na mshauri mahiri wa masuala ya kijamii na kisiasa, lakini kwao alikuwa zaidi ya hayo, alikuwa baba, mume, babu na mlezi aliyewaunganisha wote.

“Kwetu sisi, baba alikuwa moyo wa familia. Alikuwa nguzo tuliyotegemea na chanzo cha mshikamano wetu. Leo hii tunaposema mbuyu umeanguka, tunaeleza kwa undani kabisa jinsi pengo lake lilivyo kubwa,” amesema.

Amesema kama watoto wanakumbuka malezi waliyopewa na baba yao, malezi yaliyojengwa juu ya nidhamu, bidii na kuthamini elimu.

Nobert amesema marehemu alikuwa mtu aliyesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa uaminifu na kujituma, akiamini kuwa juhudi za kweli ndizo zinazofungua milango ya mafanikio.

“Baba alikuwa akituambia tusichoke kujifunza na tusione aibu kuuliza pale tusipoelewa. Alitujengea tabia ya kufanya mambo kwa umakini na si kwa kukurupuka, hakikisha unafanya utafiti, uliza maswali yote utakayoweza kabla hujafanya maamuzi.

Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakiwa kwenye misa takatifu ya kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na wenye Ulemavu), William Lukuvi katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Nakumbuka kama ulikuwa na jambo ukimfuata baba kumshirikisha, lazima uwe umejipanga kweli kweli, maana atakupiga maswali kushoto, kulia, juu, chini hadi unajiuliza haya yote yametokea wapi,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amesema marehemu Lukuvi alianza siasa akiwa kijana mdogo na hadi sasa mchango wake katika chama na nchi ni mkubwa kwa zaidi ya miaka 40 aliyokitumikia chama.

“Kwa kweli, ingawa wananchi walisema walimpata Pacome kama mbadala, sisi tunapata changamoto ya kupata mbadala kwa sababu mtu aliyeandaliwa na kuongoza kwa zaidi ya miaka 30 si rahisi kumpata. Ni sawa na madaktari kupoteza daktari bingwa ambaye inachukua miaka mingi kumsomesha,” amesema.

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema alifanya kazi na Lukuvi kwa muda mrefu tangu wakiwa Umoja wa Vijana wa CCM, baadaye bungeni na hatimaye serikalini.

“Amenisaidia katika nafasi mbalimbali, kuwa mkuu wa mkoa, waziri ameisaidia sana nchi. Alikuwa mtu anayependa kufanya kazi. Ukimwagiza kitu, anajisikia vizuri kwamba ameagizwa na pia anafurahia kutoa taarifa ya kazi aliyotumwa ameifanya vizuri,” amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo, hakushangaa kuona Rais akimteua kuwa mshauri wake na baadaye kuwa waziri.

“Kwa hiyo Taifa limepoteza mmoja wa watu wake mahiri, wazalendo wa kweli, waliojitolea kwa ajili ya nchi yetu na maendeleo ya watu wake. Kitaifa tumepoteza mmoja wa viongozi mahiri,” amesema.