Kahama. Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amekabidhi vitendea kazi kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha changamoto za wateja zinatatuliwa kwa haraka zaidi.
Vifaa hivyo vya usafiri ni pamoja na magari manne, Bajaj moja na pikipiki nne.
Akizungumza Ijumaa Machi 27, 2026, katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Makamba amesema hatua hiyo inatekeleza maono ya Rais, Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kutaka kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika na wa haraka.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba akiwa juu ya moja ya pikipiki alizokabidhi kwa Tanesco Shinyanga.
Amesema vitendea kazi hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi kwa watumishi wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga na kuwawezesha kufika kwa wakati katika maeneo yenye changamoto za umeme ili kuzitatua bila kuchelewa.
“Vyombo hivi vya usafiri vitasaidia kuleta mabadiliko katika kumfikia mteja kwa haraka na kumhudumia ipasavyo. Niwaombe visitumike kikamilifu kutatua changamoto za wananchi kwa wakati,” amesema Makamba.
Aidha, amewataka wakazi wa Manispaa ya Kahama kuchangamkia matumizi ya nishati safi ya umeme kwa kupikia, akieleza kuwa ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.
“Niwaombe wakina mama wa Kahama tutumie nishati safi ya umeme kupikia. Tanesco wameleta majiko ya umeme ambayo ni rahisi na ya haraka kutumia,” amesema.
Pia ameeleza kuwa Serikali kupitia Tanesco inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Manispaa ya Kahama kutokana na ukuaji wa kasi wa mji huo, ambapo zaidi ya Sh600 milioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa laini mpya ya umeme itakayoboresha huduma kwa wakazi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Benson Mbigili amesema shirika limepokea vitendea kazi hivyo na vitasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuwafikia wateja kwa haraka, hususan katika maeneo magumu kufikika.
Ameongeza kuwa Tanesco Mkoa wa Shinyanga inaendelea pia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu manufaa ya nishati hiyo kwa afya na mazingira.
