Mwanza. Serikali imekamilisha utafiti wa vitendo wa Usalama na Ujumuishaji Shuleni (SIAR) uliotekelezwa kupitia programu ya Shule Bora, kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza, ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto nchini.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa, licha ya uwepo wa sera, mifumo na miongozo ya usalama na ujumuishaji, bado kuna changamoto katika utekelezaji wake kutokana na kutokulingana kwa mila, desturi na mitazamo ya jamii.
Aidha, utafiti umebaini uwepo wa utamaduni wa ukimya unaochangiwa na aibu, staha pamoja na hofu ya kuharibu heshima ya familia, hali inayozuia utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Vilevile, unyanyapaa na imani potofu kuhusu ulemavu zimeendelea kuwa kikwazo katika ujumuishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu, huku ushiriki mdogo wa jamii ukidhoofisha juhudi za kulinda usalama wa mtoto.
Akifunga warsha ya siku tatu ya wadau wa elimu kuhusu utekelezaji wa mikakati ya ulinzi, usalama wa mtoto na ujumuishaji wa elimu leo Jumamosi, Machi 28, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Fatuma Nassoro, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha watoto wanakuwa salama ili watimize ndoto zao.
Baadhi ya wadau wa elimu wakiwa kwenye warsha ya kujadili masuala mbalimbali juu ya usalama wa mtoto kuanzia shuleni hadi kwenye jamii. Picha na Saada Amir
Amesema miongozo ya usimamizi, usalama na ulinzi wa mtoto imetolewa katika shule za msingi na sekondari, sambamba na utekelezaji wa programu zinazolenga kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapokwenda na kurudi shuleni.
“Tumeandaa utaratibu wa mapito salama kwa watoto kwa kushirikisha jamii. Maeneo yenye vichaka husafishwa ili kuhakikisha watoto wanapita katika mazingira salama,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inashirikiana na jamii pamoja na maofisa maendeleo ya jamii katika kuimarisha ulinzi wa mtoto, huku kila shule ikiwa na walimu wa unasihi wa kike na wa kiume wanaosaidia kuwajengea wanafunzi ujasiri na kuwapatia elimu ya kujilinda.
Kupitia programu hiyo, wanafunzi pia hufundishwa namna ya kuripoti matukio hatarishi wanayokutana nayo shuleni au njiani, pamoja na kuelekezwa ni kwa nani wanapaswa kutoa taarifa na kwa utaratibu gani.
Mafunzo hayo pia yametolewa kwa watendaji wa kata, wenyeviti wa bodi na kamati za shule, ili kuhakikisha ulinzi wa mtoto unaimarishwa ndani na nje ya shule.
Naibu Kiongozi wa Programu ya Shule Bora, Benjamin Oganga, amesema utafiti huo umeweka msingi muhimu wa kupata suluhisho zinazozingatia mazingira halisi ya jamii.
Ameeleza kuwa jamii ina nafasi kubwa katika kulinda watoto, hivyo ni muhimu kuwashirikisha viongozi wa dini, wazee wa mila na wanawake vinara katika utekelezaji wa mikakati hiyo.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Muungano mkoani Pwani, Vivian Nnko, ameshauri kuboreshwa kwa mchakato wa utambuzi wa watoto wenye mahitaji maalumu ili ufanyike mwaka mzima, badala ya miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia watoto wengi zaidi kupata haki zao za msingi.
Mapendekezo ya utafiti huo yanazitaka Serikali na wadau kutumia lugha na mbinu zinazoendana na tamaduni za jamii, kuimarisha mifumo ya kuripoti matukio ya ukatili, pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa jamii kupitia majukwaa yasiyo rasmi kama masoko na nyumba za ibada.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kujenga mazingira salama na jumuishi kwa wanafunzi, kuongeza ujasiri wa kuripoti matukio hatarishi na kupunguza unyanyapaa, jambo litakalochangia kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuanzishwa kwa Siku ya Kitaifa ya Elimu Jumuishi na Usalama wa Mtoto, pamoja na kurekebisha miongozo ili iendane na mazingira halisi ya jamii.
Utafiti huo ulizinduliwa Machi 2025 na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, na kutekelezwa katika mikoa ya Pwani, Mara, Kigoma na Rukwa, ukihusisha Halmashauri za Kibaha, Butiama, Kasulu na Sumbawanga.
