Watafiti waiomba Serikali kurekebisha sera zinazonufaisha wachache

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kutunga na kutekeleza sera mbalimbali za maendeleo, wadau wa utafiti na sera wameitaka kuhakikisha sera hizo zinawanufaisha wananchi wengi zaidi badala ya kundi dogo la watu, wakisisitiza umuhimu wa maendeleo jumuishi kwa ustawi wa jamii.

Wito huo umetolewa Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam na watafiti na wadau wa maendeleo wakati wa mhadhara wa wazi ulioongozwa na Profesa Vishantie Sewpaul kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal) cha Afrika Kusini (UKZN).

Akizungumza katika mhadhara huo uliokuwa na mada “Politicization of the Self: Personal Mastery for Professional Capabilities and Transformative Societies,” mtafiti mwandamizi wa  Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Hubert Shija, amesema baadhi ya sera zilizopo zinawanufaisha watu wachache huku jamii kubwa ikikosa fursa.

Dk Shija amesema kuna haja ya kufanya maboresho ya sera ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na rasilimali na fursa za maendeleo.

“Baadhi ya sera tulizonazo sasa ni ngumu kubadilika na mara nyingi zinanufaisha watu wachache pekee. Mara nyingine hata zinadumisha mitazamo ya zamani inayoweka majukumu fulani kwa wanawake na mengine kwa wanaume,” amesema.

Ameongeza kuwa sera hizo zilitungwa na jamii yenyewe hivyo kuna uwezekano wa kuzibadilisha ili ziendane na mahitaji ya sasa ya maendeleo jumuishi.

“Tunapaswa kufanya mageuzi ya sera ili kufungua fursa kwa kila mtu na kuhakikisha jamii nzima inanufaika. Kumaliza ubinafsi katika jamii huanza na mtu mmoja mmoja lakini pia kunahitaji sera zinazotoa fursa sawa kwa wote,” amesema.

Kwa upande wake, Profesa Vishantie amesema ili kufanikisha mabadiliko ya kweli katika jamii, ni lazima mataifa yajifunze kutokana na historia na kuepuka kurudia mifumo ya zamani iliyosababisha ukosefu wa usawa.

Amesema baadhi ya mifumo ya kijamii na kiuchumi iliyoachwa na wakoloni bado inaathiri namna maendeleo yanavyogawanywa katika jamii.

“Hatupaswi kurudia makosa yaliyofanywa na wakoloni. Mabadiliko ya kweli yanahitaji kuthubutu kuhoji mifumo ya zamani na kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha watu wote, si kundi dogo la walio na nafasi au mamlaka,” amesema.

Ametoa mfano wa migogoro ya muda mrefu duniani, ikiwemo mvutano kati ya Iran na Israel, akieleza kuwa kushikilia misimamo migumu ya kihistoria kunaweza kuendeleza mgawanyiko na migogoro inayodumu kwa muda mrefu.

Naye mwanzilishi mwenza wa Utu Africa, Wilma Mallya, amesema maendeleo endelevu yanawezekana pale jamii inapojenga utamaduni wa kuheshimiana na kusaidiana.

Amesema jamii inapaswa kujenga mazingira ya amani na mshikamano ili kuwezesha maendeleo jumuishi.

“Ni muhimu kuishi katika mazingira yenye utulivu na amani. Maendeleo endelevu na ukuaji jumuishi vinawezekana pale jamii inapothamini utu wa kila mmoja na kushirikiana kutatua changamoto,” amesema.