ZFF yaleta neema kwa waamuzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limesema lina mpango wa kuboresha maslahi ya waamuzi ili kuongeza ubora wa usimamizi wa michezo ya soka visiwani hapa.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha (ZFF), Awadh Maulid Mwita wakati akizungumza na waamuzi kwenye Ofisi za Shirikisho hilo zilizopo Mbuyu Mnene, Unguja.

Mwenyekiti huyo, alisema sababu za kufanya hivyo ni kuongeza hadhi kwa waamuzi na ili kufanya kazi yao kwa weledi na umakini wanapokuwa uwanjani.

“ZFF imejipanga kuweka mikakati maalumu ya kuboresha mazingira na maslahi ya waamuzi ili kuongeza ubora wa usimamizi wa michezo ya soka Zanzibar,” alisema.

Pia mwenyekiti huyo, alisema kamati imefanya hivyo kwa lengo la kuwafanya waamuzi hao kuifanya kazi yao vizuri bila ya upendeleo wa aina wowote.

Alifafanua kwamba, pia kamati hiyo inapanga kuboresha mavazi ya waamuzi kwa kiwango kikubwa, hatua itakayosaidia kuongeza hadhi na kuimarisha taaluma ya uamuzi katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na ZFF.

Alisema, kamati itahakikisha kila kinachopatikana kinaongezwa mara mbili katika kipindi kijacho na iwapo hilo halitawezekana angalau kiwango hicho kitaongezwa ili kuendelea kuimarisha ustawi wa waamuzi.

Mwita amewataka waamuzi kushirikiana kwa pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwa lengo la kulinda heshima ya soka la Zanzibar.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo alitangaza kuwa, ZFF itaweka utaratibu wa kutoa tuzo kwa waamuzi wanaofanya vizuri kila mwezi.

Alisema mwamuzi atakayesimamia mchezo kwa weledi wa hali ya juu atalipwa Sh200,000, huku mwamuzi mwenye nidhamu bora akizawadiwa kiasi kama hicho.

Alisisitiza kwamba tuzo hizo zitatolewa kila mwezi kwa lengo la kuwahamasisha waamuzi kufanya kazi kwa kiwango cha kitaalamu zaidi na kuimarisha ushindani chanya miongoni mwao. Ikumbukwe kuwa, kwasasa mwamuzi anayechezesha mechi ya Ligi Kuu Zanzibar analipwa kati ya Sh20,000 hadi 30,000 kwa kila mchezo mmoja.