Fadlu amkomalia beki Yanga | Mwanaspoti

RAJA Athletic haijakata tamaa bado inaipigania saini ya beki mmoja wa Yanga ambapo sasa imempa ofa kubwa huku ikimtaka mwenyewe kufanya uamuzi kama abaki klabuni kwake au akavae jezi za kijani na nyeupe za Waarabu hao.

Raja imerudi tena kwa Chadrack Boka ambaye ni beki wa kushoto wa Yanga ikimtaka Mkongomani huyo kwenda kuungana na kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, ambaye alikuwa kocha wa Simba msimu uliopita akimaliza nafasi ya pili kwenye ligi.

Mara ya kwanza Raja ilitua Yanga wakati wa usajili wa Januari ikituma ofa ambayo hata hivyo mabosi wa timu hiyo waliigomea wakiwajibu waarabu kwamba beki huyo hayupo sokoni.

Raja imerudi tena kwa Boka ikimsisitiza kwamba bado anahitajika kwenye kikosi chao ambapo kama Mkongomani huyo yuko tayari anaweza kufanya maamuzi juu ya kumalizana na klabu yake kisha fasta watamchukua.

“Hakuna nafasi ya sisi kufanya biashara kirahisi na Yanga, tulishawatafuta viongozi wao lakini walikuwa wagumu sana na hata namna tulivyongea nao hatukufurahi sana, sasa hapa wa kumaliza hilo ni mchezaji mweyewe,”amesema bosi huyo wa Raja.

“Tunajua kwamba kwasasa hapati nafasi sana (Boka) lakini bado idara ya ufundi inamtaka huyo beki,huku tunataka sana beki mwenye kasi na urefu mzuri ambavyo anavyo vyote, hatuoni kama wenzetu (Yanga) kama wako tayari kukaa mezani na sisi kumaliza hiyo biashara.

Boka kwasasa yuko majeruhi akiuguza kifundo cha mguu wake lakini kabla ya hapo amekuwa na muda mchache wa kucheza, ukipunguzwa na ujio wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye  anapata nafasi zaidi ya kuanza.

Beki huyo wa zamani wa TP Mazembe na FC Lupopo akimaliza msimu huu, atabakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa miaka mitatu wa Yanga ambapo kama atataka kuondoka lazima ake mezani na mabosi wa klabu yake kuridhia.

Awali Yanga ilishindwa kufanya uamuzi wa kumuuza Boka ikidai endapo ingefanya hivyo kikosi hicho kingesalia na beki mmoja pekee wa kushoto, Tshabalala, na kugoma kukaa mezani na Waarabu hao.

“Nikweli ilikuja hiyo ofa tuliwahi kuijadili kwenye vikao lakini wakati ambao hii ofa ilikuja haukuwa rafiki, unajua kule kushoto tuna Boka na Tshabalala pekee ukimuodoa mmoja hapo lazima uanze kuishin maisha ya shida, tukasema tuachane nayo.”amesema bosi mmoja wa Yanga.

“Hatuna shida kumuachia mchezaji lakini wakati mzuri ni mwisho wa msimu ambapo unaweza kufanya hesabu za kuchukua nani aje azibe nafasi yake, wakati kama huu ambao tunakumbana na presha ya majeruhi wengi ni vigumu.”