Hisia pekee hazitoshi, jifunze kupenda

Dar es Salaam. Katika jamii ya leo, mapenzi mara nyingi hufafanuliwa kwa hisia kali: msisimko wa kukutana, mapigo ya moyo yanayoongezeka, hamu ya kuwa karibu kila wakati na mtu fulani. 

Hisia hizi zimepewa nafasi kubwa kupitia nyimbo, filamu na mitandao ya kijamii kiasi cha kufanya wengi waamini kuwa mapenzi ni suala la kuhisi tu. 

Hata hivyo, kadiri muda unavyopita, ukweli hujitokeza wazi: hisia pekee hazitoshi. Hisia huja na kuondoka, hupanda na kushuka, lakini kupenda ni jambo linalohitaji kujifunza, kufundishwa na kufanyiwa kazi kila siku.

Waandishi wengi wameandika kwa kina kuhusu tofauti kati ya kuhisi na kupenda. Hisia ni kama cheche inayowasha moto, lakini cheche peke yake haiwezi kuifanya nyumba ipate joto kwa muda mrefu. Kupenda ni kuni, ni uangalizi wa moto usizimike, ni kujua lini uongeze na lini upunguze. 

Katika mtazamo wa kijamii, ndoa na uhusiano mwingi huvunjika si kwa sababu watu hawakuwa na hisia, bali kwa sababu hawakujifunza kupenda baada ya hisia za awali kupungua.

Mchambuzi yeyote wa masuala ya familia atakueleza kuwa migogoro mingi huanza pale mmoja anaposema, “Sihisi tena kama zamani.” 

Kauli hii huonesha imani potofu kuwa mapenzi yanategemea hisia pekee. Ukweli ni kwamba hisia ni hatua ya kwanza tu, lakini kupenda ni uamuzi, ni nidhamu, na ni sanaa inayohitaji kujifunza kwa makusudi.

Somo la kujifunza kupenda

Mwanazuoni na mwanafalsafa wa mapenzi  Erich Fromm, katika kitabu chake maarufu: The Art of Loving, anatoa msingi mzito wa hoja kuwa mapenzi si hisia ya ghafla bali ni ujuzi. Anaandika: “Mapenzi si hisia tu; ni sanaa inayopaswa kujifunza” Fromm anasisitiza kuwa kama ilivyo muziki au uchoraji, kupenda kunahitaji mazoezi, nidhamu na uvumilivu. 

Watu wengi hupenda hisia za kupendwa, lakini hawajifunzi wajibu wa kupenda.

Kwa kumtazama Fromm kwa jicho la uhalisia, anatuambia kuwa tatizo si kukosa mapenzi, bali kukosa elimu ya mapenzi. 

Wengi huingia katika uhusiano wakitarajia kupokea, si kutoa. Hisia zinapopungua, uhusiano hutikisika kwa sababu haukujengwa juu ya ujuzi wa kupenda bali juu ya msisimko wa muda mfupi.

Mwandishi na mshauri wa ndoa Gary Chapman, kupitia kitabu chake:  The Five Love Languages, ameeleza kwa namna ya vitendo kuwa watu hupenda kwa lugha tofauti.

Katika kitabu hicho anaandika: “Mapenzi ni jambo unalofanya kwa ajili ya mtu mwingine, si kwa ajili yako mwenyewe.” Hapa Chapman anavunja dhana ya kuwa mapenzi ni kujisikia vizuri pekee. Kupenda ni kitendo kinachohusisha kujitolea, hata pale hisia zinapokuwa haziko juu.

Kwa mujibu wa Chapman, hisia zinaweza kukuambia unampenda mtu, lakini kujifunza kupenda kunakufundisha jinsi ya kuonyesha upendo kwa namna ambayo mwenzako anaelewa na kuthamini.

 Hii inaonesha wazi kuwa mapenzi yanahitaji maarifa, si msukumo wa moyo pekee.

Mwandishi mwingine mashuhuri, Paulo Coelho, naye ameandika kwa mtazamo wa kifalsafa kuhusu mapenzi na uwajibikaji. 

Katika  kitabu: By the River Piedra I Sat Down and Wept, anaandika: “Mapenzi si mazoea, si ahadi, wala si deni. Si kama nyimbo za kimapenzi zinavyotuambia. Mapenzi yapo tu.” 

Ingawa kauli hii inaonekana kuipa nafasi hisia, ndani yake Coelho anasisitiza uhalisia: mapenzi hayalazimishwi, lakini yanahitaji uwepo wa dhati. 

Uwepo huu hauji kwa hisia pekee, bali kwa ufahamu wa kina wa nafs yako na ya mwenzako.

Chinua Achebe katika maandiko yake kuhusu jamii na uhusiano, aligusia mara kadhaa umuhimu wa wajibu kuliko hisia. Ingawa hakutunga kitabu mahsusi cha mapenzi, katika kitabu chake maarufu:  Things Fall Apart kuna wazo linaloweza kutafsiriwa katika uhusiano wa kimapenzi, pale anapodokeza kuwa maisha hujengwa juu ya majukumu, si hisia za muda mfupi.

Ana kauli yake maarufu  kuwa mtu anayepuuza wajibu wa kupenda, hujiumiza yeye mwenyewe na mwenzake. 

“Mtu anayewasababishia wengine matatizo, pia anajisababishia matatizo mwenyewe, anaongeza kusema.

Ndani ya mapenzi, kutotaka kujifunza kupenda ni chanzo cha maumivu kwa pande zote.

Kwa kuangalia waandishi hawa, ujumbe wao unakutana katika hoja moja kuu: hisia ni muhimu, lakini hazitoshi. Kupenda ni jambo linalojengwa juu ya ufahamu, uamuzi na matendo ya kila siku.

Uhalisia wa maisha ya leo

Katika maisha ya sasa, changamoto za mapenzi zimekuwa nyingi zaidi. Kasi ya maisha, shinikizo la kiuchumi na mitazamo mipya ya kijamii vimefanya uhusiano uwe mgumu zaidi. 

Watu wanapochoka au kukerwa, kauli ya kwanza huwa, “Sihisi tena mapenzi.” Kauli hii imekuwa kama hukumu ya mwisho, badala ya kuwa mwanzo wa kujifunza upya kupenda.

Kujifunza kupenda kunamaanisha kujifunza kusikiliza, kuelewa, kusamehe na wakati mwingine kuvumilia. Haya yote si hisia, bali ni uamuzi.

Ni rahisi kupenda mtu anapokufurahisha, lakini kupenda kwa dhati huonekana pale unapochagua kubaki hata wakati hisia zimepungua.

Hisia ni kama hali ya hewa, hubadilika bila kuuliza. Kupenda ni kama nyumba, inajengwa kwa misingi imara.

Bila kujifunza kupenda, hisia zinapopotea, nyumba hubomoka. Ndiyo maana waandishi kama Fromm walisisitiza elimu ya mapenzi kama hitaji la msingi katika jamii.

Hisia ni mwanzo mzuri, lakini mwisho wa safari ni upendo unaochaguliwa kila siku. 

Kupenda ni kujifunza, na kujifunza kupenda ni uwekezaji wa maisha yote. Pale jamii itakapokubali ukweli huu, uhusiano mwingi utaacha kutegemea msisimko wa muda mfupi na kuanza kujengwa juu ya misingi ya uelewa, uwajibikaji na upendo wa kweli.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya kimtandao.