LICHA ya KVZ kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mafunzo katika mwendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar, lakini ofisa habari wa timu hiyo, Abduljalil Mohamed amekiri kikosi chao hakikucheza vizuri ingawa kimeondoka na pointi tatu.
Ofisa huyo amesema, kutokana na ugumu wa ratiba ulivyo, hawaangalii kucheza vizuri bali wanachotafuta ni pointi tatu na wameshukuru kuzipata.
Mechi hiyo ya raundi ya 21, ilichezwa Jumamosi Machi 28, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja ambapo mabao ya KVZ yalifungwa na Bilali Amiri dakika ya tano, Mussa Jeba (dk 46) na Michael Joseph (dk 67).
Akizungumza baada ya kumaliza kwa mechi hiyo, Ofisa Habari wa KVZ, Abduljalil Mohamed amesema timu hiyo haikucheza mpira wa kuvutia lakini wanachofurahi wamepata matokeo mazuri.
Amesema, mashabiki wanapaswa kutambua kwamba timu hiyo inacheza kutafuta matokeo na sio kusifiwa, hivyo wakubaliane na hali hiyo.
“Hatuhitaji kucheza mpira mzuri kwa sasa kwani tulishacheza huko nyuma bila ya mafanikio, timu imejipanga kucheza mpira na kupata matokeo mazuri ambayo yatafanya kushinda mataiji mengi msimu huu,” amesema.
Amesema, timu ina ratiba ngumu hasa kipindi hiki kwani wana mechi za Ligi Kuu Zanzibar, Kombe la Muungano na Kombe la FA Cup, hivyo ndio maana wanacheza kwa tahadhari kubwa kusaka ushindi.
Hii ni mara ya pili msimu huu kwa Mafunzo kupoteza alama tatu mbele ya KVZ, baada kufungwa mabao 3-1 walipokutana kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu.
Ushindi huo, umeifanya KVZ kufikisha pointi 40 na kupanda hadi nafasi ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kabla ya mechi moja ya jana ambapo Zimamoto iliyokuwa nafasi ya tatu ikikusanya pointi 38, ilicheza dhidi ya Kipanga iliyokuwa nafasi ya sita na pointi 34.
