Kwa nini mbio za urais 2030 zimeanza mapema?

Dar es Salaam. Kwa nini mapema? Ni swali linaloakisi harakati, vikumbo na hekaheka zilizoanza kushuhudiwa kwa miongoni mwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakijisafishia njia ya kupenya na hatimaye kuupata urais mwaka 2030.

Ni mapema, kwa sababu miezi minne tu imepita, tangu Rais Samia Suluhu Hassan, aapishwe kuiongoza nchi kwa muhula wa pili, nafasi atakayohudumu kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2030 kwa mujibu wa Katiba.

Imechukua muda mchache baada ya Serikali mpya kuingia madarakani, kuibuka harakati, pilika na mipango ya watu kuutaka urais mwaka 2030, jambo lililowaibua viongozi wa Serikali na hata chama hicho tawala, wakionya mienendo hiyo.

Machi 27, mwaka huu, Makamu Mwenyekiki wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, aliwaonya makada wa chama hicho waache harakati za mapema za kujipanga kwa urais mwaka 2030.

“Unazungumziaje urais 2030 leo, wakati hata hujui kama utakuwepo. Hiyo ni kama kumjaribu Mungu. Wakati huu tunapaswa kujikita kwenye kazi za kujenga chama na nchi,” alisema.

Siku mbili kabla ya kauli ya Wasira, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, akiwa mkoani Arusha, Machi 25, aliwaambia wanaojipanga kwa urais mwaka 2030, hawatafanikiwa katika mbio hizo.

“Ukiona hao viongozi wanataka kujitenganisha, hii ni Serikali yeye akae pembeni awe sehemu ya wakosoaji wanaoikosoa Serikali. Watu wote wanaojipanga hawa hawawezi kushika hata urais, 2030 hawapati,” alisema.

Kauli kuhusu kuwepo vikumbo vya urais 2030, ilitolewa pia hata na Rais Samia mwenyewe, alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam, Desemba 2, mwaka jana. Aliwatahadharisha wateule wake wenye nia ya urais 2030, waachie nafasi alizowapa, ili wafanye harakati hizo wakiwa nje ya Serikali.

“Nimesema kazi yetu sasa ni kutibu majeraha na hapa nataka nizungumze na watoto wangu, vijana wanaoangalia mbele hawa wengine waliopo nje. Wanaongalia mbele 2030 safari hiyo isiende kutuvurugia nchi yetu.

“Nilizungumza na mawaziri wangu, nikamwambia namuangalia mmoja mmoja, una masilahi na huko, kaa nje kafanye huko usifanye ndani ya Serikali yangu. Nimekuweka hapo ukatumikie wananchi masilahi yako utayakuta mbele, Mungu ndio anajua nani kiongozi,” amesema.

Wachambuzi wa siasa, wanaona kuanza mapema kwa harakati hizo, kunachochea kupungua kwa ufanisi wa utendaji serikalini, huku wengine wakisema ni jambo zuri kwa kuwa zinaipa siasa uhai.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Anjali Nguyuhambi, amesema inapotokea mkuu wa nchi aliyepo madarakani anamaliza muhula wa mwisho, pilika na kujipitisha hujitokeza mapema.

Inakuwa mapema kutokana na kile alichoeleza, watia nia wanatengeneza mazingira ya kujitambulisha kwa wananchi na mamlaka zitakazowapitisha ili watathminiwe mapema.

“Mara nyingi inafanyika hivi, watia nia wakitaka kujiingiza katika fikra za wananchi na wale watakaowaunga mkono. Ingekuwa Rais aliyepo madarakani naye ni mgombea mtarajiwa hilo usingeliona mapema hasa kwa CCM,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Majjid, anaona harakati hizo kama matokeo ya kutojulikana nani atakuwa mrithi wa nafasi hiyo, ukizingatia aliyepo anamaliza muhula wa mwisho.

“Pale ambapo hakuna mrithi anayejulikana, kila mwenye ndoto huanza mapema kujipanga, ili asije akachelewa wakati wa maamuzi,” amesema.

Ameeleza mkuu wa nchi aliyepo madarakani bado yuko katikati ya safari ya utumishi wake, hivyo hakuna ishara kwamba nani atamrithi atakapomaliza muda wake.

Hali hiyo, inaibua kile alichokiita uwanja wa wazi wa mapambano kwa kuwa kila mtu anaona nafasi ipo wazi kwa ajili ya kushindania.

“Ndani ya CCM, utaratibu wa kumpata mgombea unategemea vikao na ushawishi wa ndani, hivyo watu wanaona kuanza mapema ni silaha muhimu,” amesema.

Dk Nguyuhambi,ameeleza joto hilo la mapema lina madhara kwa sababu linaathiri mwenendo wa utendaji wa wanaotajwa kwani baadhi yao ni sehemu ya Serikali.

“Wanaotajwa ni viongozi wakubwa serikalini na unakuta utendaji wao unalegalega kwa sababu hawajielekezi kutimiza wajibu wa uongozi, bali wanajionyesha ili kupata uungwaji mkono,” amesema.

Kwa aina hiyo ya utendaji, amesema watu hao mara nyingi wanaishia kujitangaza wenyewe badala ya kutangaza chama au kutekeleza yale ambayo yanapaswa kutekelezwa kwa wakati husika.

“Si kitu kizuri kuanza mapema kiutendaji na kwa maslahi ya chama husika, lakini kwa wagombea, tutarajie kuona hilo likiendelea kujitokeza sana,” amesema.

Kwa upande wa Majjid, anaona harakati za mapema ni hatari kwa kudhoofisha utendaji wa Serikali, kwani inawafanya viongozi wafikirie uongozi wa baadaye badala ya utendaji wa sasa.

“Wakati viongozi wanaanza kufikiria uchaguzi unaofuata mapema, wanapunguza muda wa kufikiria utendaji wa sasa,” amefafanua.

Ameijenga hoja yake hiyo, akirejea ripoti ya Utawala na Usimamizi wa Sekta ya Umma ya Benki ya Dunia, inayoonyesha katika nchi zinazoendelea, kuanza mapema kwa siasa za uchaguzi kunapunguza ufanisi wa taasisi za umma kati ya asilimia 20 hadi 30.

“Viongozi wanaweza kuanza kufanya maamuzi ya kisiasa badala ya kitaalamu, kuweka mbele umaarufu badala ya utendaji wa sasa,” amesema.

Ameeleza hilo pia, linahatarisha kutokea kwa mgawanyiko ndani ya Serikali na chama husika, kwa kuwa watia nia watakuwa wanashindana kujenga umaarufu wakiwa serikalini.

“Badala ya kuzingatia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, viongozi wanaanza kujijenga kisiasa, hii inaathiri huduma kwa wananchi,” amesema.

Ingawa watu wanatazama vibaya kuhusu hilo, kwa Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa, Balozi Benson Bana, amesema ni jambo zuri na linaipa siasa uhai wakati wote.

Katika siasa, mwanazuoni huyo amesema mwisho wa uchaguzi ni mwanzo wa mwingine, hivyo vikumbo, harakati, pilika na kujipitisha ni vitu ambavyo vinapaswa kutarajiwa, kwani vinaiweka siasa hai muda wote.

“Sioni ubaya kwa hilo. Watu kuanza vuguvugu la urais sasa wala sio mbaya. Watu wanapaswa waone hilo kama uhai wa kisiasa,” amesema Balozi Bana, aliyewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Nigeria.

Amesema watiania wakijipitisha, kufanya harakati na hata kujitangaza mapema inatoa nafasi kwa wapiga kura kumchunguza, kumtathmini na kumpima kama anawafaa ili wamchague wakati utakapofika au wamtose.

“Najua kwa sasa hakuna mtu aliyejitangaza, lakini watu kuanza kuunda vikambi imeanza na sio mbaya. Isipokuwa hilo lisidumaze utekelezaji wa yale ambayo yanapaswa kutekelezwa sasa,” amesema.

Ametaka watu waachwe wajitokeze kabisa, kwa sababu wapigakura ndilo chujio la mwisho kwa anayestahili urais na yule asiyestahili.

Pamoja na yote hayo, Dk Bana amesema vyama vya siasa, vina haki ya kuweka miiko na taratibu zao katika kujitokeza huko, kulingana na masilahi yao.