Lissu aja kivingine, mawakili wafungua shauri la kikatiba

Dodoma. Mawakili watatu wamefungua shauri la Kikatiba wakipinga vikwazo wanavyowekewa na Mkuu wa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, kila wanapokwenda gerezani kuzungumza na mteja wao, Tundu Lissu.

Katika shauri hilo namba 7300 la 2026 lililofunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma na mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri 17 dhidi ya walalamikiwa.

Mawakili hao wamefungua shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), Mkuu wa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na Lissu mwenyewe ambaye ni mshitakiwa katika kesi ya uhaini.

Shauri hilo la Kikatiba limepangwa kutajwa Aprili 14 mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Amir Mruma, Dk Angelo Rumisha na Evaristo Longopa, wakati usikilizwaji wa kesi ya Lissu ukiwa umesimama.

Mara kadhaa, Lissu amekuwa akilalamika mahakamani juu ya mawakili wake, ndugu, jamaa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho yeye ni mwenyekiti, kunyimwa fursa ya kumuona na kuzungumza naye.

Safari suala hilo halijaishia kwa Lissu kulalamika mahakamani, mawakili hao wamefungua shauri la kikatiba na moja ya amri wanazoomba ni wajibu maombi kuwaruhusu mawakili kuzungumza na Lissu kwa faragha.

Kwa nini wamefungua shauri

Walalamikaji wanaowakilishwa na Wakili John Seka wamefungua shauri hilo kutafuta uamuzi wa kimahakama kuhusu uhalali wa matendo ya mjibu maombi wa tatu (mkuu wa Gereza) kutokana na kushindwa kutekeleza kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza.

Kwa mujibu wa walalamikaji hao, kanuni hiyo inahakikisha haki ya washauri wa kisheria kufanya mashauriano ya siri na wateja wao, ikihakikisha kwamba ushauri wa kitaalamu wa kisheria unaweza kutolewa na kupokewa bila kuingiliwa.

Mawakili hao wanaiomba mahakama itoe tamko kuhusu utangamano wa kutotekelezwa huko na haki za msingi zilizohakikishwa chini ya ibara za 13(1), 13(3), 13(6)(a), 15, 16(1), 22, 26(1) na 29(2) za Katiba ya Tanzania ya 1977.

Wanaeleza kuwa mleta shauri wa kwanza, Wakili Maduhu ni mmoja wa mawakili na mshauri wa sheria wa Lissu, ambaye yuko mahabusu tangu Aprili 2025, akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi dhidi yake.

Kwamba mara nyingi kati ya Septemba 2025 na Machi 2026, mleta shauri huyo wa kwanza amekuwa akienda Gereza la Ukonga kwa ajili ya kumpa ushauri Lissu.

“Malengo yake ya msingi (Wakili Maduhu) katika ziara hizi yalikuwa kutoa hati zenye udharura za kesi na misimamo ya kisheria (case law) na kujadili mikakati muhimu ya kesi ambayo ilihitaji majadiliano ya siri ya ana kwa ana,” wanaeleza.

Mara ya kwanza ilikuwa Januari 20, 2026, ambapo mleta shauri huyo wa kwanza alijulishwa na maofisa wa Gereza la Ukonga wakati wa kuingia, kwamba hataruhusiwa kuonana wala kuzungumza na mjibu maombi wa 4, Tundu Lissu.

“Siku hiyo, mleta shauri wa kwanza aliomba kuonana na mkuu wa gereza la Ukonga, ambaye alimthibitishia kuwa amekuwa akitekeleza maagizo na maelekezo yanayotolewa na mjibu maombi wa pili (Kamishna Mkuu wa Magereza,” wanadai.

Kwa mujibu wa walalamikaji hao, tukio lingine ni la Machi 11, 2026 ambapo mleta shauri huyo wa kwanza alikwenda tena katika gereza hilo akiwa na nyaraka muhimu na za haraka kwa ajili ya Lissu, lakini alikataliwa kuzungumza naye.

“Maafisa wa zamu hawakuweza au hawakutaka kutoa maelezo yoyote ya kwa nini wanakataa kuniruhusu isipokuwa kwamba wanafuata maagizo na maelekezo ya mjibu maombi wa 2 (kamishna mkuu) na wa 3 ambaye ni mkuu wa gereza,” wanalalamika.

Kwa mujibu wa hati za shauri hilo, hali hiyo ilimkumba tena mleta maombi wa kwanza Septemba 30, 2025 na Oktoba 28, 2025. Vilevile mleta shauri wa pili, Wakili Nashon Nkungu katika tarehe tofauti tofauti naye alikutana na vikwazo kama hivyo.

Wanadai kuwa katika tarehe hizo ambazo mleta shauri wa pili alimtembelea Lissu gerezani kwa ajili ya ushauri wa kisheria, mazungumza yao hayakuwa ya faragha kwani maofisa wanne wa magereza walibakia umbali wanaoweza kusikia kila kitu wanachozungumza.

Kutokana na mazingira hayo na athari za moja kwa moja, mleta shauri wa pili na mjibu maombi wa nne (Lissu) hawakuweza kufanya mashauriano yao katika hali ya faragha, ambayo ni muhimu kwa kubadilishana taarifa zenye ukweli wa habari.

Kwa upande wake, mleta shauri wa tatu, Wakili Paul Kisabo, inaelezwa kuwa tangu Lissu akamatwe, alitembelea mara kwa mara gereza la Ukonga kwa ajili ya mashauriano na naye, lakini wakati wote wa mazungumzo, maofisa wanne walikuwapo.

Wanaeleza kuwa waleta shauri wote watatu wanadai matendo hayo ni kinyume kabisa na kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza na kwamba kuwanyima kabisa fursa ya kumwakilisha vyema katika shauri la uhaini linalomkabili mahakamani.

Katika shauri hilo, waleta shauri wanadai pamoja na mambo mengine, kitendo cha mawakili wa Lissu kuzuiwa kumuona gerezani ni kinyume cha sheria na kinaingilia haki za mawakili, jambo ambalo ni kinyume na Ibara ya 22 ya Katiba.

Wanalalamika kuwa kitendo cha mkuu wa gereza la Ukonga, kushindwa kusimamia utekelezaji wa Kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza na kumzuia kabisa wakili wa Lissu kushauriana naye, kinakiuka Ibara ya 13(1) ya Katiba.

Halikadhalika kitendo cha kutoruhusu mawakili wa Lissu kuzungumza naye kwa faragha gerezani kama Kanuni ya 13 inavyoelekeza, kunakiuka ibara za 13(1), 13(3) na 16 ya Katiba inayotoa haki ya usawa, usikilizwaji wa haki na wa faragha.

“Kushindwa kutekeleza kanuni ya 13 ni uvunjaji wa Ibara ya 26(1) ya katiba inayoweka wajibu kwa kila mtu na mamlaka kuheshimu, kudumisha na kutekeleza Katiba. Vitendo vyao vinadhoofisha ukuu wa Katiba na utawala wa sheria”

“Kwamba kuzuia mashauriano ya siri na kumnyima kupata mawakili mfungwa na kutendewa udhalilishaji, kunadhoofisha utu wake, na kuzuia haki yake kinyume cha sheria na kinyume na ibara za 15, 29(1) na 29(2) ya Katiba,” wanaeleza.

Katika shauri hilo walalamikaji wanaiomba mahakama itoe maagizo, kwamba wakati shauri hilo linasubiri kusikilizwa na kuamuliwa na mahakama, wapewe haki ya kuongea na kushauriana na mjibu maombi wa nne (Lissu) kwa faragha.

Pia wanaiomba mahakama itamke Kanuni ya 13 ya Kanuni za magereza imetungwa kwa usahihi na inatoa hakikisho la ushauriano wa faragha kati ya mfungwa na mawakili wake na mazungumzo yao yasisikilizwe na maofisa magereza.

Walalamikaji wanaiomba mahakama itamke kuwa matendo ya maofisa magereza katika gereza la Ukonga ya kubakia kusikiliza mazungumzo ya mashauriano ya kisheria kati ya mleta shauri wa 2 na 3 na Lissu ni kinyume cha sheria.

Wanaiomba mahakama itamke kuwa matendo yote hayo yanakiuka Katiba.

Walalamikaji wanaiomba mahakama itoe amri kwa wajibu maombi kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha kuwa mazungumzo ya mashauriano ya kisheria ya wafungwa na mawakili wao yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 13.

Pia wanaiomba mahakama itoe amri ya hakikisho kuwa mashauriano ya kisheria kati ya Lissu na mawakili wake katika gereza la Ukonga au eneo lolote nchini, yanafanyika kwa faragha na bila mawakili kuzuiwa kuwaona wateja wao.

Mbali na ombi hilo, wanaiomba mahakama, kwamba ndani ya siku 90 za kutolewa kwa hukumu na miezi sita baadaye, wajibu maombi wawasilishe taarifa mahakamani ya namna walivyotekeleza kanuni ya 13 na ibara ya 16 ya Katiba.

Mahakama itoe amri kwamba wakati kesi ya jinai inayomkabili Lissu ikiendelea, Lissu atakiwe awe analeta taarifa kortini endapo ataona dalili za uvunjwaji au uingiliwaji wa haki zake za mawasiliano ya faragha na mawakili wake gerezani.

Vilevile wanaomba mahakama itoe ari kuwa kila upande ubebe gharama zake za shauri hilo na itoe nafuu yoyote ambayo itaona inafaa kulingana na mamlaka yake ya kikatiba kupitia ibara ya 26(1) ya Katiba inayokazia kuheshimiwa kwa Katiba.