BODI ya Ligi Zanzibar (ZLB) imesema imejipanga kuimarisha ulinzi kwa michezo yote iliyosalia ya Ligi Kuu Soka Zanzibar na Ligi Daraja la Kwanza ili kuhakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa utulivu na kufuata sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Issa Kassim wakati akizungumza na Mwanaspoti kwenye Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) zilizopo Mbuyu Mnene.
Amesema, katika tathmini iliyofanywa na Bodi hiyo imebaini kuwa vurugu zinazotokea viwanjani wakati wa mechi zinasababishwa na ubishi wa baadhi ya wadau wa mpira wa miguu ambao hawaelewi sheria za mpira wa miguu.
“Tathmini iliyofanywa imebaini kuwa baadhi ya michezo imekuwa ikikumbwa na matatizo yanayotokana na ubishi wa wadau mbalimbali ambao hawaelewi vizuri vizuri sheria za soka,” amesema.
Kutokana na hilo, Bodi hiyo imejipanga kuimarisha ulinzi kwa michezo yote ndani na nje ya uwanja ili kuhakikisha inamaliza kwa haki na amani.
Alisisitiza kuwa, mara nyingi wadau hao wanawahujumu waamuzi kuwa wanaharibu michezo jambo ambalo sio sahihi na hayo yote yanasababishwa na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria za mpira.
Amesema, baada ya kutokea hayo, wanatumia njia hiyo kuanza kulalamika na kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
Vilevile, amesema, Bodi ya Ligi imeanza kuchukua hatua ya kutoa elimu kwa wadau wa soka, ikiwemo kufanya mikutano na viongozi wa klabu kuwafahamisha kuhusu sheria za mchezo na umuhimu wa kuziheshimu.
Mtendaji huyo, ametoa wito kwa wadau wa michezo kuwa na ushirikiano kwani hilo ni muhimu katika kuhakikisha michezo inachezwa kwa kuzingatia nidhamu.
