Iringa. Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, umewasili mkoani Iringa tayari kwa mazishi yatakayofanyika Jumanne, Machi 31, 2026.
Jeneza lenye mwili wa marehemu limewasili katika Uwanja wa Ndege wa Nduli saa 10:45 jioni na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James.
Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, ukiwasili mkoani Iringa tayari kwa mazishi yatakayofanyika Jumanne, Machi 31, 2026.
Baada ya mapokezi hayo, msafara wa kuupeleka mwili ulianza kuelekea nyumbani kwa marehemu, Gangilonga, mtaa wa Kinondoni, ambako uliwasili saa 12:10 jioni, ukipokewa kwa vilio na majonzi kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wakiusubiri.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, kesho Jumatatu mwili huo utatolewa nyumbani na kupelekwa katika Kanisa Katoliki Kihesa, Manispaa ya Iringa, kwa ibada ya kuaga itakayoanza saa 3:00 asubuhi.
Baada ya ibada hiyo, mwili utasafirishwa kuelekea Kijiji cha Idodi, Wilaya ya Iringa, kwa ajili ya maandalizi ya mazishi yatakayofanyika siku inayofuata.
Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, ukiwasili mkoani Iringa tayari kwa mazishi yatakayofanyika Jumanne, Machi 31, 2026.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, James, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha taratibu zote zinafanyika kwa utulivu na heshima stahiki.
“Baada ya ibada ya kuaga, safari kuelekea Kijiji cha Idodi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mazishi itaanza,” amesema.
Ameongeza kuwa mazishi hayo yataongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, huku yakitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi.
Aidha, amesema hatua za ulinzi na usalama zimeimarishwa ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa utaratibu.
Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, ukiwasili mkoani Iringa tayari kwa mazishi yatakayofanyika Jumanne, Machi 31, 2026.
Awali, mwili wa marehemu uliagwa jijini Dodoma Machi 27, 2026, kabla ya kusafirishwa hadi Dar es Salaam ambako uliagwa kitaifa Machi 28, 2026.
William Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.