Rais CAF aitaja Yanga, ishu ya Senegal 

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe amekumbushia bao walilofunga Yanga kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi wakati akitangaza mabadiliko na maboresho katika Katiba na Kanuni zake yatakayoongeza imani na uwazi kwa waamuzi, wasimamizi wa VAR pamoja na vyombo vya kimaamuzi vya shirikisho hilo.

Motsepe amewataja mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara katika hotuba yake wakati akitoa ufafanuzi wake huko Cairo, Misri katika mkutano maalumu na waandishi wa habari uliofanyika Misri

Tukio ambalo Motsepe aliligusia ni bao la Yanga ambalo lilikataliwa mwaka 2024 katika mechi ya robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns na kufanya mechi hiyo kumalizika suluhu hivyo, Wananchi kutupwa nje kwa mikwaju ya penalti 3-2.

“Kama ulitazama kwenye TV wakati ule Yanga inacheza na Mamelodi lile lilikuwa ni bao halali na nimekuwa nikisema hivyo mara nyingi, kumekuwa na juhudi nyingi kuhakikisha tunatoka huko na ndicho hiki tunachofanya sasa,” alisema na kuongeza.

“CAF kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa katika Katiba na Kanuni zake ambayo yataongeza imani kwa waamuzi wa CAF, waendeshaji wa VAR, makamishna wa mechi pamoja na Bodi ya Nidhamu na Rufaa ya CAF. Maboresho haya pia yatahakikisha kuwa matukio yasiyokubalika yaliyojitokeza katika AFCON Morocco 2025 hayatatokea tena,” alisema rais huyo.

Aliongeza kuwa CAF imepata ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalamu bora wa sheria za soka kutoka Afrika na kimataifa ili kuhakikisha kuwa kanuni zake zinaendana na viwango bora vya soka duniani, ndani na nje ya uwanja.

Katika maboresho hayo, CAF imeeleza kuwa itaendelea na utaratibu wa kuteua majaji na wanasheria bora kutoka barani Afrika ili kuunda Bodi ya Nidhamu na Bodi ya Rufaa ya shirikisho hilo.

Majaji na wanasheria hawa huteuliwa na Kamati ya Utendaji ya CAF pamoja na Mkutano Mkuu wa CAF, kutokana na majina yanayopendekezwa na vyama wanachama 54 na mashirikisho ya kanda huku ikielezwa kuwa Uhuru na kutokuwa na upendeleo kwa vyombo vya kimahakama vya CAF ni jambo la lazima.

CAF pia imesisitiza msimamo wake wa kutovumilia rushwa na tabia zisizofaa, pamoja na kuhakikisha kuwa vyama vyote wanachama vinatendewa kwa usawa bila upendeleo wowote.

Azungumzia ubingwa wa Senegal

 Motsepe amesema mechi ya fainali kati ya Morocco na Senegal siyo jambo muhimu sana kuendelea kulijadili na wapo tayari kuheshimu mifumo ya kisheria.

Hivi karibuni CAF iliipoka ubingwa wa AFCON Senegal ambo iliopata baada ya kuichapa Morocco mabao kwenye mchezo wa fainali, hata hivyo bosi huyo wa zamani wa Mamelodi amesema siyo jambo la kujadiliwa kwa sasa.

‘‘Mechi ya fainali kati ya Senegal na Morocco, si jambo muhimu sana kuendelea kulijadili. Tunachotaka kusisitiza ni kwamba suala hilo tayari liko mbele ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ambayo ni chombo cha juu cha maamuzi katika masuala ya michezo duniani, na sisi tutaheshimu na kutekeleza uamuzi wowote utakaochukuliwa na CAS”.

Ameeleza kuwa CAF haioni umuhimu wa kuendelea kujadili suala hilo hadharani, bali inaelekeza nguvu katika kuheshimu taratibu na mifumo ya kisheria ya michezo.