Dar es Salaam. Serikali imetangaza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha maeneo maalumu ya kiuchumi kwa ajili ya viwanda vya dawa, huku zaidi ya wawekezaji 50 tayari wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo.
inayochukuliwa kuwa miongoni mwa vipaumbele vipya vya kimkakati nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, amesema Serikali imekamilisha maandalizi ya kuanzisha eneo la kwanza la viwanda la Mloganzila lenye ukubwa wa ekari 600, huku eneo lingine la ekari 100 likiwa Bagamoyo, mkoani Pwani, na kufanya jumla ya ekari 700 kutengwa kwa ajili ya uwekezaji huo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, Tayari anasema, “Kwa sasa tupo hatua za mwisho kabisa za kuanzisha Mloganzila Pharmaceutical and Medical Special Economic Zone.
“Hii ni hatua kubwa sana, lakini pia tuna eneo lingine Bagamoyo ambalo nalo liko katika hatua za mwisho. Kwa ujumla tuna ekari 700 ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya dawa.”
Anabainisha kuwa tangu Desemba mwaka jana Serikali ilipoanza rasmi kupokea maombi ya wawekezaji, zaidi ya maombi 50 yamepokelewa na yanaendelea kufanyiwa tathmini, huku jitihada zaidi zikiendelea kuvutia wawekezaji wapya kutoka ndani na nje ya nchi.
Tayari anasema uwekezaji katika viwanda vya dawa nchini unaweza kufikia kati ya Dola bilioni 5 za Marekani (sawa na Sh12.8 trilioni) hadi Dola bilioni 10 za Marekani (Sh25.6 trilioni), jambo linaloonesha fursa kubwa ya kiuchumi kwa Taifa.
“Tuna Watanzania wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha, lakini wengi wao wanawekeza kwenye magari ya thamani kubwa. Tunawaomba waone fursa hii na kuwekeza katika viwanda vya dawa, hata kwa ubia na wawekezaji hawa 50 waliojitokeza.
“Wanapaswa kuchukua nafasi hii kwa kushirikiana na wawekezaji hao kupitia miradi ya ubia, ili baadaye kuhakikisha wanamiliki sehemu ya sekta hii muhimu. Serikali haitaki kuunda watu maskini, bali inataka wananchi wake wafanikiwe, wawe wamiliki wa biashara kubwa,” anafafanua.
Soko la ndani, kimataifa lalengwa
Kwa mujibu wa Tayari, mkakati huo hauishii katika kukidhi mahitaji ya ndani pekee, bali unalenga pia soko la kikanda na kimataifa, hususan nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Anasema Tanzania inaangalia uwezekano wa kushiriki kikamilifu katika mfumo wa pamoja wa ununuzi wa dawa wa SADC (pooled procurement), hatua itakayoongeza nguvu ya majadiliano ya bei na kushusha gharama za dawa.
“Unapokwenda kununua dawa kwa wingi mkubwa, uwezo wa kubargain bei unakuwa mkubwa zaidi. Kupitia mfumo huu, tunaamini tutashusha gharama za dawa, lakini pia tutafungua soko kwa viwanda vyetu vya ndani kuuza bidhaa nje,” anasema.
Anasisitiza kuwa ili kufanikisha hilo, Serikali inaweka mkazo katika ubora wa bidhaa kwa kuhakikisha viwanda vyote vinavyokuja vinafikia viwango vya kimataifa vya GMP (Good Manufacturing Practice) na WHO Prequalification (WHO PQ).
Miundombinu na nishati kupunguza gharama
Moja ya changamoto kubwa katika uzalishaji wa dawa ni gharama kubwa za uzalishaji. Tayari anasema Serikali imejipanga kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na miundombinu ya kisasa, ikiwemo barabara, umeme wa uhakika na upatikanaji wa gesi.
“Tunajenga miundombinu yote muhimu, ikiwemo umeme wa uhakika na hata kuzungumza na TPDC ili kuhakikisha gesi inapatikana. Hizi zote ni mbinu za kushusha gharama za uzalishaji na kuvutia wawekezaji,” anafafanua.
Aidha, anasema Serikali imepanga kuwekeza Dola milioni 10 za Marekani kujenga maabara ya kisasa ya bioequivalence studies Mloganzila, ambayo itasaidia kupima ubora wa dawa na kukuza tafiti za kisayansi.
“Gharama kubwa katika dawa siyo viwanda pekee, bali tafiti na maendeleo ya bidhaa. Maabara hii itasaidia kupunguza gharama hizo na kurahisisha ubunifu wa dawa mpya hapa nchini,” anasema.
Tayari anataja taasisi za utafiti kama NIMR na Ifakara Health Institute kuwa zina mchango mkubwa katika sekta ya dawa, lakini changamoto imekuwa ni ukosefu wa mifumo ya kibiashara (commercialization).
Anasema uwekezaji katika maabara hiyo mpya utasaidia tafiti zinazofanyika nchini kubaki hapa na kuleta matokeo ya moja kwa moja katika maendeleo ya dawa.
“Kwa sasa watafiti wengi hulazimika kupeleka sampuli nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi. Tukipata maabara yetu, tafiti zote zitafanyika hapa na matokeo yatatumika moja kwa moja katika uzalishaji wa dawa,” anasema.
Katika kukabiliana na tatizo la dawa bandia, Tayari anasema uwepo wa viwanda vya ndani utarahisisha udhibiti wa ubora wa dawa ukilinganisha na utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
“Ni rahisi kukagua kiwanda kilichopo nchini mara kwa mara kuliko kufuatilia bidhaa zinazotoka nje. Hii itasaidia sana kupunguza dawa bandia na kuhakikisha usalama wa wagonjwa,” anasema.
Anaongeza kuwa sekta hiyo pia itachangia kuongeza ajira kwa maelfu ya Watanzania na kujenga wataalamu wabobezi katika masuala ya dawa na udhibiti wa ubora.
Soko la dola bilioni moja kwa mwaka
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, Tanzania kwa sasa inaagiza dawa kutoka nje zenye thamani ya kati ya Dola milioni 800 hadi bilioni moja, sawa na Sh2.5 trilioni kwa mwaka, huku uwezo wa uzalishaji wa ndani ukiwa ni takribani asilimia 10 tu ya mahitaji.
Tayari anasema hali hiyo inaonesha wazi fursa kubwa iliyopo kwa wawekezaji wa ndani na nje.
“Kwa sasa asilimia 90 ya dawa tunategemea kutoka nje. Hii ni fursa kubwa kwa uwekezaji wa ndani. Tunataka kufikia angalau asilimia 80 ya uzalishaji wa ndani ndani ya miaka mitano,” anasema.
Anaongeza kuwa kuanza kwa bima ya afya kwa wote kutachochea zaidi mahitaji ya dawa, na hivyo kuongeza ukubwa wa soko hilo.
Utashi wa kisiasa na dira ya Taifa
Tayari anasisitiza kuwa mafanikio ya mkakati huo yanatokana na utashi mkubwa wa kisiasa uliopo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya sekta ya viwanda vya dawa kuwa ajenda ya kitaifa.
“Utashi wa kisiasa ni muhimu. Rais ameonesha dhamira ya dhati na ametupa maelekezo ya kuhakikisha sekta hii inakua kwa kasi,” anasema.
Anabainisha kuwa hata kuundwa kwa kikosi kazi maalumu (Pharmaceutical Acceleration Task Force), kinachojumuisha taasisi mbalimbali, ni sehemu ya juhudi za kurahisisha uwekezaji na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo awali.
Fursa kwa wataalamu na diaspora
Katika kuhakikisha sekta hiyo inapata utaalamu wa hali ya juu, Tayari anasema ameunda mtandao wa wataalamu wa Kitanzania waliopo nje ya nchi (diaspora), wanaoshirikiana kutoa ushauri wa kitaalamu.
“Tunao Watanzania zaidi ya 50 walioko kwenye nafasi za juu duniani katika sekta ya dawa. Wanatusaidia kwa ushauri na uzoefu wao ili kuhakikisha tunajenga sekta imara,” anasema.
Anaongeza kuwa sekta hiyo itatoa nafasi kubwa kwa wahitimu wa fani za famasia, kemia na uhandisi, ambao kwa sasa wengi wao hawapati nafasi za kutumia ujuzi wao ipasavyo.
Hatua kuelekea kuwa kitovu cha Afrika
Kwa mtazamo wa muda mrefu, Tayari anasema Tanzania inalenga kuwa siyo tu kitovu cha dawa kwa ndani, bali kwa Afrika nzima.
“Hili siyo suala la Tanzania pekee, tunataka kuwa kitovu cha Afrika. Tunataka kuzalisha dawa zenye ubora, bei nafuu na zinazokubalika kimataifa,” anasema.
Anasisitiza kuwa mafanikio ya mkakati huo yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, kuanzia Serikali, sekta binafsi hadi wananchi kwa ujumla.
“Kilichobaki sasa ni Watanzania kuunga mkono ajenda hii, kuizungumza vizuri na kuchangamkia fursa zilizopo. Hii ni nafasi ya kipekee ambayo hatupaswi kuikosa,” anasema.
