Baada ya kuiongoza Taifa Stars katika mechi tano zilizopita bila ya ushindi sawa na dakika 450, hatimaye kocha, Miguel Gamondi ameonja ushindi wake wa kwanza katika mechi ya kimataifa dhidi ya Macau katika michuano ya FIFA Series huko Kigali, Rwanda.
Licha ya kufanya mabadiliko ya wachezaji 10 katika kikosi cha kwanza kilichoanza katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo ambayo Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Liechtenstein, Stars ilionekana kutawala mchezo huo na kuibuka na ushindi wa mabao 6-0, ikiwa ni rekodi kwa Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni.
Mabao ya Stars katika mchezo huo, yalifungwa na Amancio (alijifunga) dakika ya 16, Bakari Mwamnyeto dakika ya 26 na Mudathir Yahya dakika ya 45 katika kipindi cha kwanza ambapo vijana hao wa Gamondi walipiga mashuti 11, huku matano yakilenga lango.
Mabao mengine yalifungwa kipindi cha pili na Paul Peter katika dakika ya 56 na Novatus Dismas katika dakika ya 74 na Allarakhia katika dakika ya 87. Katika kipindi hicho, Stars ilifanya mabadiliko ya wachezaji wote ambao walianza kipindi cha kwanza kwa nyakati tofauti.
Katika mchezo huo, Charles M’Mombwa alihusika na mabao matatu ya Stars kati ya sita kuanzia la kwanza ambalo Amancio alijifunga huku akitoa asisti za mabao ya Mudathir na Peter kwa dakika 56 ambazo alicheza.
Gamondi aliiogoza Stars kwa mara ya kwanza Morocco katika fainali za mataifa ya Afrika ambako alikuwa kocha wa muda akichukua mikoba ya Hemed Suleiman, licha ya kikosi chake kutoshinda mechi hata moja kiliweka historia ya kutinga hatua ya 16 bora na pointi mbili.
Stars ilitinga hatua hiyo baada ya kuwa kati ya timu nne ambazo zilikuwa na pointi nyingi na zilimaliza katika nafasi ya tatu. Katika fainali hizo ambapo Stars ilikuwa kundi C ilianza kwa kufungwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria huku ikikusanya pointi mbili muhimu kwa kutoa sare bao 1-1 katika kila mechi dhidi ya Uganda na Tunisia.
Katika mechi ya hatua ya 16 bora, Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa fainali hizo, hivyo kurejea nyumbani kifua mbele kwani kutinga hatua hiyo ilikuwa ni historia kwa Tanzania.
Kwa Gamondi mechi dhidi ya Macau ni mechi ya sita huku ikiwa ya pili ya kirafiki katika kalenda ya FIFA na kocha huyo katika uchaguzi wake wa kikosi hicho, alisema anataka kujenga kikosi cha ushindi kuelekea fainali zijazo za mataifa ya Afrika 2027 ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki.
Lakini pia huo ulikuwa ushindi wa pili tangu Stars ianze kushiriki michuano ya FIFA Series, mara ya kwanza ikicheza michuano hiyo ilikuwa Azerbaijan waliichapa Mongolia nayo ya Asia baada ya kufungwa mechi ya kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria.
Katika mechi hizo, Novatus ndiye mchezaji wa Stars mwenye mabao mengi zaidi (2), alifunga pia katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mongolia kabla ya kufunga tena, jana dhidi ya Macau.
