TRA YATOA WITO KWA WALIPAKODI KUFANYA MAKADIRIO KWA WAKATI

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka walipakodi ambao bado hawajafanyiwa makadirio ya kodi kwa nchi nzima kutumia siku mbili zilizosalia kufanya makadirio yao kabla ya kufika kwa muda wa mwisho wa kufanya makadirio ambao ni Machi 31, 2026.

Akizungumza na baadhi ya walipakodi pamoja na waandishi wa habari alipofanya ziara katika kituo cha kodi cha Buguruni kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam tarehe 29.03.2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema ni vema walipakodi wakautumia muda uliosalia kwenda kufanyiwa makadirio ya kodi.

Amesema TRA imefungua ofisi zake kwa siku za Jumamosi na Jumapili kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mmoja mwenye kutakiwa kufanya makadirio anatekeleza wajibu wake kikamilifu.

Anasema makadirio yanafanywa kwa wale wanaoanza biashara na kwa wale ambao walishaanza biashara huku akiwataka walipakodi kuhakikisha wanafanyiwa makadirio kutokana na aina ya biashara wanayoifanya wanazofanya.

“Moja ya haki ya wanaokadiriwa kulipa kodi ni kwenda kwa maafisa wa TRA ili waweze kukadiriwa, kama wataona kiasi walichokadiriwa ni kidogo wanayo haki ya kuwaeleza maafisa wetu, lakini pia kama wakiona kiasi walichokadiriwa ni kikubwa pia wanayo haki pia ya kuwambiwa maafisa yetu ili wafanyiwe upya makadirio” amesema Mwenda

Kwa Upande wake Meneja wa Kituo Cha Huduma za Kodi Cha Buguruni Mamika Nyika amewataka wafanyabiashara na watoa huduma wote kuhakikisha wanatumia kikamilifu siku tatu zilizobaki ili kujiepusha na adhabu na kusisitiza kuwa milango ya Ofisi hiyo ipo wazi kwa ajili ya kuwahudumia

Naye mmoja wa walipakodi katika kituo hicho Bw. Masoud Kumbakumba mbali na kutoa rai kwa wafanyabiashara wenzie kutumia muda uliobaki kujitokeza kulipa Kodi, amesema tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa TRA imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara jambo linalowavutia kujitokeza kulipa Kodi.

Amesema Kipindi cha nyuma ilikuwa ngumu kuwaona wafanyabiashara wakienda kwa hiari katika Ofisi za TRA hali iliyotokana na uwepo wa hofu miongoni mwao, ila kwa sasa hakuna hali kama hiyo jambo linaloongeza wigo wa ulipaji wa Kodi kwa hiari.