Dar es Salaam. Katika kipindi hiki ambacho dunia inabadilika kwa kasi kubwa ya kiteknolojia na kiuchumi, suala la malezi limebeba uzito mpya.
Wazazi hawapaswi tena kujiuliza tu kama watoto wao wanafanya vizuri darasani, bali pia kama wanajengewa misingi imara itakayowawezesha kusimama wenyewe katika soko la ajira lenye ushindani mkali.
Malezi bora si suala la chakula, mavazi na ada za shule pekee; ni mchakato wa makusudi wa kumjenga kijana kuwa mtu anayejitambua, anayewajibika na mwenye uwezo wa kuzalisha thamani katika jamii.
Kwa muda mrefu, wazazi wengi hupima mafanikio ya watoto wao katika ufaulu wa mitihani na kupata ajira rasmi.
Hata hivyo, hali halisi inaonyesha kuwa ajira za kuajiriwa serikalini au katika taasisi kubwa hazitoshelezi idadi ya wahitimu wanaomaliza masomo kila mwaka.
Hivyo, malezi bora yanapaswa kumwandaa kijana si tu kuomba kazi, bali pia kufikiria kwa ubunifu, kujiajiri na hata kuajiri wengine.
Msingi wa kwanza wa malezi bora ni kumjenga mtoto katika maadili. Uadilifu, nidhamu, uwajibikaji na kuheshimu muda, ni sifa zinazotafutwa katika kila eneo la kazi.
Maadili haya hujengwa tangu utotoni kupitia majukumu madogo ya nyumbani, kufuata taratibu na kuwajibika kwa makosa.
Niliwahi kuambiwa na wataalamu wa makuzi na malezi ya watoto kwamba, mtoto anayejifunza kutimiza wajibu wake mapema, hukua akiwa mtu anayeweza kuaminiwa, jambo ambalo ni mtaji mkubwa katika ajira.
Pili, walisema wazazi wanapaswa kutambua na kukuza vipaji vya watoto wao. Walisema hivyo kwa sababu kila mtoto ana upekee wake, wapo wenye uwezo wa sayansi, sanaa, michezo au uongozi.
Hivyo, malezi bora yanahitaji mzazi kuwa karibu na mtoto wake, kusikiliza ndoto zake na kumsaidia kuzifanyia kazi. Kulazimisha taaluma isiyoendana na uwezo au shauku ya mtoto kunaweza kuzima matarajio au ndoto zake na kuathiri mafanikio yake ya baadaye.
Aidha, vijana wa leo wanahitaji stadi za maisha zaidi ya elimu ya darasani. Uwezo wa kuwasiliana kwa ufasaha, kufanya kazi kwa ushirikiano, kutatua matatizo na kufanya uamuzi sahihi, ni nguzo muhimu katika soko la ajira ambayo mzazi anapaswa kulitambua hilo mapema sana.
Hivyo, wazazi wanaweza kuchangia kwa kuwahusisha watoto katika mijadala ya kifamilia, kuwapa nafasi ya kutoa maoni na kuwafundisha namna ya kukabiliana na changamoto bila kukata tamaa.
Katika enzi hii ya teknolojia, malezi bora pia yanahusisha mwongozo sahihi wa matumizi ya vifaa vya kidijitali.
Badala ya kuacha watoto watumie teknolojia bila mwelekeo, wazazi wanapaswa kuwahamasisha kuitumia kama chombo cha kujifunza na kutafuta fursa.
Ujuzi wa kidijitali umegeuka kuwa hitaji la msingi katika sekta nyingi, hivyo maandalizi haya ni sehemu ya kuwajenga vijana imara.
Vilevile, kuwafundisha watoto thamani ya kazi ni sehemu muhimu ya malezi. Mtoto anapojifunza kuwa mafanikio yanatokana na juhudi na si njia za mkato, hujengeka katika misingi ya uvumilivu na bidii. Mzazi anaweza kuhamasisha moyo wa kujitegemea kwa kuwapa watoto fursa za kushiriki katika shughuli ndogondogo za uzalishaji au miradi ya ubunifu inayowajengea uzoefu.
Hata hivyo, malezi haya hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano kati ya familia, shule na jamii. Shule hutoa maarifa na mwelekeo wa kitaaluma, lakini familia hutoa maadili na msingi wa tabia.
Jamii nayo inachangia kwa kuunda mazingira salama na yenye kuhamasisha juhudi. Ushirikiano huu wa pande zote huimarisha maandalizi ya kijana kwa maisha ya kazi.
Kwa maana nyingine, malezi bora ndiyo nguzo ya vijana imara kwa soko la ajira. Wazazi wanapochukua jukumu la makusudi la kujenga maadili, kukuza vipaji, kufundisha stadi za maisha na kuelekeza matumizi sahihi ya teknolojia, wanawaandaa watoto wao kukabiliana na changamoto za dunia ya kazi.
Vijana waliolelewa katika misingi hiyo si tu wataweza kupata ajira, bali pia watakuwa wabunifu na wachangiaji wa maendeleo ya taifa.
