Mirerani. Watu 1,163 walioathirika na mafuriko katika Tarafa ya Moipo, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamepatiwa msaada wa vyakula na mahitaji mengine muhimu wenye thamani ya Sh20 milioni, uliotolewa na kampuni ya uchimbaji madini ya Permanent Mineral Ltd.
Msaada huo umetolewa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha zilizosababisha nyumba za wakazi wengi kuingiliwa na maji, huku ekari 5,429 za mashamba ya maharage na mahindi zikisombwa na maji.
Akizungumza leo Machi 29, 2026 wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba ya waathirika, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandana, ameishukuru kampuni hiyo kwa kujitolea kuwasaidia wananchi waliokumbwa na maafa hayo.
Lulandana amesema mafuriko hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa kaya nyingi katika tarafa ya Moipo, hali iliyosababisha uharibifu wa mali na mazao.
Amefafanua kuwa kati ya waathirika hao, 233 ni kutoka kata ya Endiamtu na ekari 1,570 za mashamba zimeharibiwa, Mirerani watu 409 (ekari 249), Shambarai watu 461 (ekari 1,600) na Naisinyai watu 60 (ekari 2,010).
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Permanent Mineral Ltd, Elisha Mnyawi, amesema msaada huo umetolewa kwa niaba ya mkurugenzi wa kampuni hiyo, God Mwanga, ikiwa ni sehemu ya kuwafariji waathirika hao.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Lulandana (kushoto) akiwashukuru viongozi wa kampuni ya Permanent Mineral Ltd waliotoa misaada kwa waathirika 1,163 wa mafuriko wa tarafa ya Moipo wa vyakula na vifaa wa Sh20 milioni. Picha na Joseph Lyimo
Ametaja msaada uliotolewa kuwa ni pamoja na magunia 100 ya mahindi, madumu 318 ya mafuta ya kupikia, mashuka 100, kilo 500 za mchele, sabuni 400, katoni 20 za mafuta ya kujipaka na vyandarua 100.
Vifaa vingine vilivyotolewa ni madaftari 100, kalamu 200, penseli 200, kompasi 100, katoni sita za malapa na katoni sita za chumvi.
Naye Katibu wa Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, Frank Oleleshwa, amesema mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ametuma salamu za pole kwa wananchi walioathirika.
Amesema mbunge huyo yupo Malabo nchini Equatorial Guinea, kwa majukumu ya kikazi pamoja na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, lakini anaendelea kufuatilia kwa karibu athari za mafuriko hayo.
“Pamoja na kuwa nje ya nchi, Mheshimiwa Mbunge anaendelea kufuatilia hali ya waathirika na anatoa pole kwa wakazi wa Moipo pamoja na tarafa za Terrat, Emboreet na Msitu wa Tembo,” amesema Oleleshwa.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani, Hans Nkya, ameungana na wengine kutoa pole kwa waathirika na kuziomba taasisi, kampuni na watu binafsi kujitokeza kusaidia.
Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Mnyawi, amesema wananchi wa vitongoji vitano wameathirika, huku baadhi ya nyumba zikizungukwa na maji.
Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha miundombinu ya bwawa la Kidawashi ili litumike kwa kilimo cha umwagiliaji na uvuvi wa kisasa.
Naye Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian, amesema mafuriko hayo yalipitia kata za Shambarai, Endiamtu, Mirerani na Naisinyai kabla ya kuelekea bwawa la Nyumba ya Mungu.
Baadhi ya viongozi na waathirika wa mafuriko wa tarafa ya Moipo, wakimsikiliza Mkuu wa wilayani Simanjiro mkoani Manyara Fakii Lulandana. Picha na Joseph Lyimo
Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Lemboi, amesema vijiji vya Shambarai, Kilombero, Orbili na Kandasikira vimeathirika kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa waathirika, Asha Said, mkazi wa kata ya Endiamtu, ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada waliotoa katika kipindi kigumu.
Amesema mafuriko hayo yamesababisha familia yake kukosa makazi baada ya nyumba yao kuzungukwa na maji katika kitongoji cha Tupendane.
