BAADA ya kusajiliwa na Riga FC ya Latvia, kiungo mshambuliaji Abdu Mandeke amesema malengo yake yametimia kutua barani Ulaya, lakini anatamani kucheza na kuonyesha kiwango bora ili kimfungulie njia zaidi.
Mandeke ambaye amejiunga na timu hiyo akitokea Grassrunners Academy ya Nigeria, amesema kuwa kujiunga na Riga FC ni hatua kubwa katika maisha yake ya soka na anapambana kuhakikisha anaitumia fursa hiyo vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mandeke amesema anatambua ushindani uliopo ndani ya kikosi hicho, lakini yupo tayari kujituma kwa bidii ili kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
“Ndoto yangu kubwa ni kucheza na kufanya vizuri. Najua haitakuwa rahisi, lakini niko tayari kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yangu,” amesema Mandeke
“Naamini kama nitaendelea kuapata nafasi mara kwa mara inaweza kunisiadia kupandisha kiwango changu na kuendelea kuaminiwa naamini nitafika mbali zaidi.”
Baada ya kujiunga na timu hiyo tayari amecheza mechi mbili, akifunga bao moja na kutoa asisti moja, kitu ambacho kinachoonyesha uwezo wake mkubwa wa kushambulia.
Timu hiyo ambayo ilianzishwa 2014 imefanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Latvia mara nne na mataji mawili ya Kombe la FA.
