MENEJA Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Haji Haji, amesema Serikali ina mpango wa kujenga laini maalumu kutoka Mtoni hadi Mji wa Afcon (Afcon City) uliopo Fumba ili kuondosha changamoto ya umeme kwenye mji huo.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya umeme katika maeneo mbalimbali kisiwani hapa ikiwemo ya AFCON City ambayo ni maalum kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2027 nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Amesema, miradi hiyo inatazamiwa kumaliza mianya iliyopo na Serikali inaendelea kuchukua jitihada ikiwemo kuanzisha vyanzo vipya ili kuwa na umeme wa uhakika.
Zanzibar inapokea umeme kupitia waya za baharini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kwa upande wa Unguja zipo waya mbili, moja ya megawati 45 iliyowekwa 1980 na imeshatumika hadi kufikia asilimia 98.8 ya pili ya megawati 100 imeshatumika asilimia 97.3 ambapo waya zote zimeshafikia ukomo wa uwezo wa kusafirisha umeme.
Kutokana na hali hiyo, amesema laini hiyo itajengwa na kampuni kutoka nchini India ambapo itatumika kupeleka umeme kwenye mji huo unaolenga kuifungua Zanzibar kiutalii.
“Laini hiyo itatumia umeme mahsusi ambayo haitatumika sehemu nyingine yoyote zaidi ya Mji huo, lengo ni kufanya kuwa na uhakika wa nishati hiyo,” amesema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya hiyo ikiwa katika sehemu ya maandalizi ya kupokea ugeni wa AFCON 2027 kwani baadhi ya mechi zitachezwa kisiwani hapa kama ilivyokuwa CHAN 2024.
Kuelekea AFCON 2027 itakayochezwa Juni 19, 2027 hadi Julai 18, 2027, Tanzania, Kenya na Uganda zitashirikiana kuandaa fainali hizo ambapo kwa Tanzania, mechi zitachezwa Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema Serikali imejiandaa kujenga mji huo wenye thamani ya dola za marekani milioni 150 sawa na Sh388.8 bilioni.
Waziri huyo amesema mradi huo upo katika hatua ya ujenzi wa muundo mkuu ikijumuisha uwekaji wa nondo, ujenzi wa beam, kumwaga zege na ujenzi wa kuta.
“Hadi kufikia sasa mradi huo umefikia asilimia 35, na hiyo inadhihirisha namna ambavyo Serikali imejipanga kupokea ugeni huo,” amesema Pembe.
Pia, amesema kwa timu ambazo zitachaguliwa kucheza kisiwani hapa zitafanya mazoezi katika viwanja vya New Amaan Complex na Suluhu Academy.
