‘Bwege’ Afariki Dunia Akiwa Hospitalini Kigamboni

Bakari Mahundu
March 30, 2026
0 Comments

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Seleman Bungara maarufu kwa jina la ‘Bwege’ amefariki dunia mchana wa leo, Machi 30, 2026, katika hospitali binafsi iliyopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na kaka wa marehemu, Abbas S.A. Bungara, ambaye amesema kuwa ndugu yake alifariki akiwa hospitalini hapo akipatiwa huduma ya kusafisha damu (dialysis), huduma ambayo alikuwa akiipata mara kwa mara kutokana na hali yake ya kiafya.

Amesema kuwa marehemu alifikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu kama ilivyokuwa kawaida, lakini hali yake ilibadilika ghafla na hatimaye kupoteza maisha.

Kwa sasa, familia inaendelea na maandalizi ya mazishi, huku taarifa zaidi kuhusu ratiba na taratibu za mazishi zikitarajiwa kutolewa baadaye. Msiba upo nyumbani kwa Abbas Bungara, eneo la Temeke, Dar es Salaam, ambako ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kufika kutoa pole.

Enzi za uhai wake, Bungara alihudumu katika vyama mbalimbali vya siasa ikiwemo CUF na ACT-Wazalendo, na hivi karibuni alitangaza kujiunga na CHADEMA, ingawa mchakato wa kukabidhiwa rasmi kadi ya chama hicho ulikuwa bado haujakamilika.