CAG ataja sababu baadhi hoja zake kutotekelezwa

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji katika taasisi za Serikali, kunasababisha baadhi ya hoja zake kutotekelezwa kwa muda mrefu.

Kauli hiyo inatokana na kile alichosema, katika mapendekezo 38,181 yaliyotolewa na ofisi hiyo miaka ya nyuma hadi sasa ni asilimia 36.7 pekee ndiyo yametekelezwa, asilimia 43.5 yakiwa katika utekelezaji na 7.5 hayajatekelezwa kabisa.

Kichere, amekwenda mbali zaidi na kueleza kumekuwepo na mapendekezo yasiyotekelezwa kwa miaka saba hadi 20, jambo linaloonyesha changamoto ya kudumu katika ufuatiliaji wa utekelezaji na kushindwa kushughulikia vyanzo vya matatizo.

Hoja ya kutotekelezwa kwa mapendekezo ya ripoti za CAG imewahi kuibuliwa na vyama mbalimbali vya siasa vikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT Wazalendo, vilivyowahi kusema mwenendo huo unaonyesha ombwe la uwajibikaji kwa taasisi za umma.

CAG ameeleza hayo leo, Jumatatu Machi 30, 2026 aliposoma muhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi inayoanzia Juni mwaka 2024 hadi Julai mwaka 2025, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema mwenendo huo ni ishara kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi unahitaji kuimarishwa zaidi ili kuhakikisha matokeo ya ukaguzi yanakuwa nyenzo muhimu katika utendaji serikalini.

“Changamoto hizo zinatokana na kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji katika taasisi za Serikali kwa ajili ya kuratibu ufuatiliaji wa hoja za CAG na utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kutoka kwa Charles Kichere, leo Machi 30, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, amesema mfumo uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) umeanza kuonyesha ufanisi na anapendekeza utumike na taasisi zote ili kuhakikisha mapendekezo yanatekelezwa.

“Hali hii inaendelea kuhatarisha upotevu wa rasilimali za umma na kudhoofisha ufanisi wa taasisi,” amesema.

Ametaja baadhi ya taasisi zenye hoja za muda mrefu ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yenye madeni ya kodi yaliyofikia Sh7.24 bilioni yameendelea bila kukusanywa kwa zaidi ya miaka 17.

Nyingine ni Mamlaka ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo ya Hifadhi ina madeni ya Sh658 milioni yanayodaiwa na jamii ya Mafia hayajalipwa kwa zaidi ya miaka 15.

Pia, Bodi ya Korosho ina mali na viwanja vyenye thamani ya Sh3.28 bilioni bado havijapatiwa hati miliki kwa zaidi ya miaka 13 jambo linalohatarisha umiliki wake.

“Utekelezaji wa mapendekezo mengine hauhitaji rasilimali, taratibu tu za kufuta hasara kwa mujibu wa sheria, lakini taratibu hizo za kisheria zinachukua muda mrefu na kuacha hoja zikiendelea kuwepo kwenye orodha ya mapendekezo ambayo hayajatekelezwa,” amesema.