CRDB yapata tuzo benki bora ya uwezeshaji wa biashara Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetunukiwa na Shirika la Fedha Duniani (IFC), tuzo ya kimataifa ya ‘Benki Bora ya Uwezeshaji wa Biashara Afrika Mashariki 2026’.

Tuzo hiyo ni kutambua mchango wake katika kukuza huduma za fedha za biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Tuzo hiyo ilitolewa katika mkutano wa tisa wa Kimataifa wa Washirika wa Biashara (GTPM) uliofanyika Lisbon, Ureno, ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya fedha na biashara duniani.

Lengo la mkutano lilikuwa kujadili changamoto na fursa za biashara ya kimataifa, ikiwemo upatikanaji wa mitaji na uimara wa minyororo ya usambazaji.

Tuzo hiyo ilipokewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, aliyesema huo ni uthibitisho wa dhamira ya benki katika kukuza biashara na uchumi wa ukanda.

Alieleza mafanikio hayo yanaonyesha imani ya wateja na washirika pamoja na uwekezaji unaoendelea katika suluhisho bunifu za fedha za biashara.

Aidha, alisema utambuzi huo unaendana na malengo ya IFC ya kukuza biashara katika nchi zinazoendelea na kuwezesha SMEs kupitia mifumo jumuishi ya kifedha.

Mafanikio hayo yanakuja wakati CRDB ikiendelea kuimarisha nafasi yake kama mwezeshaji mkuu wa biashara kikanda.

Kupitia ushirikiano na taasisi za kimataifa, benki imepanua huduma za fedha za biashara, kuboresha mifumo ya kugawana hatari na kuvutia mitaji ya kimataifa katika masoko ya ndani.

Katika mkutano huo, benki pia iliwasilisha mafanikio yake katika ufadhili wa biashara na miundombinu, ikiwa imewezesha zaidi ya dola za Marekani 1 bilioni katika uwekezaji kwenye sekta muhimu kama kilimo, nishati na miundombinu.

Mtendaji Mkuu wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa mwelekeo sahihi wa kimkakati wa benki na mchango wake katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania na ukanda kwa ujumla.

Kwa upande wa ubunifu, benki imeanzisha huduma za ufadhili wa mnyororo wa thamani, zilizorahisisha upatikanaji wa ukwasi kwa biashara, kuimarisha uhusiano wa wasambazaji na kuongeza ushindani.

Pia, imeendelea kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu, jambo linaloimarisha nafasi yake kama mshirika wa maendeleo ya taifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Neema Mori alisema tuzo hiyo inaakisi uimara wa utawala bora, maono ya muda mrefu na uwezo wa benki kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo.

Alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa utaendelea kusaidia kukuza ujumuishaji wa uchumi wa Afrika.

Aliongeza kuwa CRDB inaendelea kutumia fursa za Mpango wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) kukuza biashara za ndani ya bara, kuimarisha minyororo ya thamani na kuongeza ushindani wa Afrika duniani.

Kwa ujumla, tuzo hii inaimarisha hadhi ya CRDB kama taasisi inayoongoza kwa ubunifu, uendelevu na mchango mkubwa katika kukuza uchumi jumuishi barani Afrika na kufungua masoko ya kimataifa kwa wafanyabiashara wa Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.