Dk Mwinyi: Mfumo huduma za afya kidijitali umeanza kuleta matokeo Zanzibar

Unguja.  Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya baada ya kuachana na mifumo ya matumizi ya karatasi na kuanza kutumia mifumo ya kidijitali, hatua ambayo tayari imeanza kuleta ufanisi katika utoaji huduma.

Dk Mwinyi amesema Serikali imejizatiti kujenga mifumo ya afya ya kidijitali iliyo salama, yenye ubora na inayozingatia mahitaji ya wananchi.

Amesema hayo leo Machi 30, 2026, alipowakilishwa na Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya, katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa afya kidijitali Zanzibar unaolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia sekta ya afya.

Amesema mkutano huo unahamasisha matumizi ya teknolojia kama tiba kwa njia ya mtandao, akili mnemba (AI) na rekodi za afya za kielektroniki ili kuboresha huduma.

“Tayari tumeanza kuona matokeo; ufanisi umeongezeka, muda wa kusubiri umepungua na usahihi wa tiba umeimarika,” amesema.

Ameongeza kuwa mifumo hiyo imepunguza muda wa watumishi kujaza makaratasi na kuongeza muda wa kutoa huduma.

Hata hivyo, amesisitiza huduma za afya ya msingi ndizo msingi wa mfumo, hivyo mageuzi ya kidijitali yafike hadi zahanati na vituo vya afya Unguja na Pemba.

Kaimu Waziri wa Afya ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Dk Saada Mkuya akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Zanzibar Digital Health alipomwakilisha Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi

Amesema afya kidijitali si hiari bali ni lazima, na inahitaji uwekezaji katika miundombinu, mifumo na ujuzi kwa watumishi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Miraji Mzee, amesema awali kulikuwa na mifumo zaidi ya 42 isiyounganishwa, lakini sasa imeanza kuunganishwa na kuboresha huduma.

“Leo tuna mfumo mmoja wa utambulisho wa mgonjwa na mifumo inayowasiliana, hali iliyoboreshwa huduma na usimamizi wa data,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Fatma Mbarouk Khamis, amesema mageuzi ya kidijitali ni msingi wa maendeleo, yakihusisha miundombinu, ulinzi wa data na teknolojia mpya.

Mwakilishi wa JSI Tanzania, Dk Jema Bisimba, amesema mifumo hiyo inaongeza ufanisi, uwazi na usahihi katika usimamizi wa huduma na rasilimali.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Maour Suleiman, amesema licha ya mafanikio, bado kuna changamoto za usawa wa huduma na matumizi ya data katika maamuzi.

Amesisitiza ushirikiano wa wadau ni muhimu kufanikisha lengo la huduma bora za afya kwa wote.