Fei Toto awaacha mbali Pacome, Chama

KIWANGO kizuri kinachoonyeshwa msimu huu na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kimemfanya kuwapiga bao nyota mbalimbali wakiwemo Pacome Zouzoua wa Yanga na mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama ‘Triple C’ wa Simba.

Fei Toto, ndiye mchezaji aliyechangia mabao mengi ya Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026, baada ya nyota huyo kuchangia 11, akifunga sita na kutoa assisti tano, akiwapiku Pacome Zouzoua na Clatous Chama, ambao wote wamekuwa wakisuasua.

Bao moja aliloifungia Azam FC katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0, dhidi ya Dodoma Jiji, Machi 11, 2026, limemfanya nyota huyo kufikisha mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu, huku akiivuka rekodi ya msimu uliopita aliofunga mabao manne tu.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Fei Toto, alifunga bao hilo la dakika ya 11, huku akichangia pia lingine moja la, Zidane Sereri, aliyefunga mawili dakika ya 5 na 70, akiwaadhibu waajiri wake wa zamani.

Baada ya Fei Toto kuchangia mabao mawili kati ya matatu dhidi ya Dodoma Jiji, nyota huyo kwa sasa amefikisha mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu, akiivuka rekodi ya msimu uliopita, huku akifikisha assisti tano, ambapo kwa sasa anadaiwa nane.

Msimu wa 2024-2025, Fei Toto, alichangia mabao 17, ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga manne na kuasisti 13, akiwa ndiye aliyeongoza kwa assisti nyingi, ingawa, kwa msimu huu, tayari amechangia 11, kufuatia kufunga sita na kuasisti matano.

Kwa upande wa Pacome wa Yanga, msimu huu amechangia mabao 6, ya Ligi Kuu Bara baada ya kufunga manne na kuasisti mawili, huku msimu wa 2024-2025, alichangia mabao 21, akifunga 12 na kuasisti tisa, akionyesha kiwango kizuri na kikosi hicho.

Pacome, aliyejiunga na Yanga, Julai 19, 2023, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, msimu wa kwanza na kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani wa 2023-2024, alichangia mabao 11, ya Ligi Kuu, baada ya kufunga saba na kuasisti manne.

Kwa upande wa Clatous Chama, anayeichezea Simba kwa misimu mitatu tofauti sasa, msimu huu amechangia mabao matatu tu ya Ligi Kuu, baada ya kufunga mawili ambayo yote aliifungia Singida Black Stars, huku assisti moja akiitoa akiwa na Simba.

Chama aliyejiunga na Simba dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Singida Black Stars, kwa msimu wa 2024-2025, alikuwa Yanga, ambapo alichangia mabao tisa, baada ya kufunga sita na kuasisti matatu, huku akiipa timu hiyo taji la Ligi Kuu.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba kwa mara ya kwanza, Julai 1, 2018, akitokea Lusaka Dynamos FC ya kwao Zambia, msimu wake wa kwanza wa 2018-2019, akiwa na kikosi hicho, alichangia mabao 16, ya Ligi Kuu, baada ya kufunga saba na kuasisti tisa.

Rekodi nzuri zaidi kwake akiichezea Simba, ni za msimu wa 2020-2021, alipochangia mabao 23, ya Ligi Kuu Bara, akifunga manane na kuasisti 15, huku msimu wa 2022-2023, kiungo huyo alichangia mabao 18, baada ya kufunga manne na kuasisti 14.

Misimu ambayo namba za Chama katika Ligi Kuu zilikuwa chini zaidi ni za msimu wa 2021-2022, aliporejea tena akitokea RS Berkane ya Morocco, kwani alifunga mabao matatu na ule wa 2019-2020, alipofunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho 10.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, Jean Charles Ahoua, aliyekuwa Simba na kuifungia timu hiyo mabao 16, kabla ya kuachana na kikosi hicho, Januari 22, 2026, alikuwa amechangia mabao mawili, baada ya kufunga moja na kuasisti moja.Ahoua aliibuka kinara wa mabao ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu hapa nchini, tangu alipojiunga na kikosi hicho, Julai 3, 2024, akitokea Stella Club d’Adjame ya kwao Ivory Coast, ambapo aliibuka Mchezaji Bora (MVP), kwa msimu wa 2023-2024.

Nyota huyo aliyewahi kuzitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kabla ya kukipiga Stella, alikuwa mchezaji bora wa Ligi ya Ivory Coast, msimu wa 2023-2024, baada ya kuhusika na mabao 21, ya kikosi hicho, akifunga 12 na kuasisti tisa.

Msimu wa 2024-2025, Ahoua alichangia mabao 25 Ligi Kuu akiwa na Simba baada ya kufunga 16 na kuasisti tisa, huku  2025-2026 alichangia mawili akifunga moja na kutoa asisiti moja, kisha kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria.

Licha ya ubora wa viungo mbalimbali ambao wamekuwa na namba nzuri katika Ligi Kuu, ila Fei Toto, ameonyesha kiwango cha kuvutia, kilichowafanya mabosi wa Al Ahli Tripoli ya Libya kumwekea Sh4.5 bilioni, ingawa Azam iliweka ngumu kumwachia.

Msimu wa 2024-2025, Fei Toto, alichangia mabao 17 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga manne na kuasisti 13, akiwa ndiye aliyeongoza kwa assisti nyingi, ingawa, kwa msimu huu, tayari amechangia 11, kufuatia kufunga sita na kuasisti matano.

Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimzidi, Stephane Aziz KI, aliyekuwa Yanga, ambaye alichangia 21, akifunga 12 na kuasisti pia tisa.

Mwaka 2024, Fei Toto aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi, akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad SC ya Libya, ambapo hadi anaondoka alichangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa.

Kiwango bora cha Fei Toto, kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI, aliyekuwa Yanga, aliyefunga mabao 21.

Pia, alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2023-2024, kwa kuifikisha Azam fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5, baada ya suluhu (0-0) ya dakika 120, Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.