Dar es Salaam. Taasisi za kifedha na benki nchini zimetakiwa kuzingatia waraka wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba unaohusu uwiano wa kijinsia.
Waraka huo wa mwaka jana 2025 unataka hadi ifikapo Juni mwaka 2028 kuwe na asilimia 30 ya wanawake katika nafasi za uongozi ikiwemo menejimenti na wajumbe wa bodi.
Hayo yamebainishwa leo Machi 30, 2026 kwenye mkutano wa pili uliowakutanisha viongozi wa benki na taasisi za kifedha, unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya fedha na shughuli za kiuchumi ulilofanyikia makao makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Akifafanua jambo kwenye mkutano huo, Gavana Tutuba amesema mkutano wa kwanza ulifanyika Machi 2025 na uliazimia benki zote angalau ziwe na uwiano hadi ifikapo 2028 kuwe na asilimia 30 kwenye bodi na menejimenti zao.
“Nashukuru hadi sasa benki 22 kati ya 42 wameshafikia uwiano wa asilimia 30 kwenye uongozi wao. Nimewaomba na benki nyingine kwa sababu mchakato wa kuwapata viongozi hao huwa unategemea uwepo wao na wanawake wenye sifa,” amesema.
Amesema waendelee kuweka mikakati na kutafuta fursa mbalimbali zitakazofanya kuwezesha wanawake kiuchumi na kushiriki shughuli za maendeleo.
“Nitaendelea kufuatilia na nataka taasisi ziendelee kuweka mikakati na kutafuta fursa mbalimbali zitakazofanya kuwezesha wanawake kiuchumi na kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo kuwawezesha kifedha na kielimu,”‘ amesema.
Kwa upande wake, Naibu Gavana uthabiti na usimamizi wa sekta ya fedha wa BoT, Sauda Msemo amesema juhudi mbalimbali zimeshafanyika katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye meza za maamuzi ya kibenki.
“Tumeona bidhaa mbalimbali zenye mrengo wa kijinsia ili kuhakikisha mahitaji maalumu yanafikiwa na kuwafanya washiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ikiwemo kupata mikopo,” amebainisha.
Msemo amesema mkutano wa leo umewaleta pamoja pia kuangazia hatua na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa kwanza.
“Kuna juhudi kubwa zimefanyika kwa sababu benki zimetekeleza kuongeza ushiriki wa wanawake katika meza ya uamuzi,” amesema.
Ameongeza kwamba ujumuishwaji wa wanawake katika sekta ya fedha si suala la kijamii bali ni muhimu, hasa kiuchumi kwa sababu uwepo wao unaongeza kasi katika shughuli za kiuchumi na ukuaji kiujumla.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi, amesema uongozi wa benki nchini hasa ngazi ya bodi tayari benki nyingi zimefikia kiwango akisema ni jambo la kujivunia katika safari ya uwiano wa kijinsia.
“Benki zina sera maalumu ya kuwasaidia wanawake kufikia ngazi za juu na bidhaa zinazohusu jinsia. Wanawake kupata mikopo na uongozi. Nashukuru Benki Kuu, wizara ya fedha na Serikali kwa ujumla,” amesema.
Aidha Sabi amebainisha maeneo ya kipaumbele ambayo ni kupanua bidhaa za kifedha zinazozingatia jinsia, kuimarisha uelewa wa kifedha na usaidizi wa ujasiriamali kwa wanawake na kuimarisha mifumo shirikishi ya udhibiti.
