MCHEZA gofu, Gervas Wilbroad, ameibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya saba ya kimataifa ya Diplomatic Golf mjini hapa baada ya kujikusanyia pointi 43 kwa siku mbili.
Ushindi huo ulimuweka mbele ya wapinzani wake wa karibu, akiwemo Rashid Rashid, aliyeshika nafasi ya pili kwa pointi 42, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Dr. Mosi Makau, aliyepata pointi 34.
Mashindano hayo, yaliyofanyika jana, Machi 29, 2026, katika mashimo 36 ndani ya Viwanja vya Kili Golf vilivyoko eneo la USA, mkoani Arusha, yalikutanisha wachezaji zaidi ya 90 kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuchangisha fedha za kusomesha watoto walio katika familia duni.
Kwa ushindani wa timu, Nathalia Isaya aliiongoza timu yake kuibuka mshindi kwa pointi 46, akishirikiana na William Loderer, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na timu ya Thimea Choggo, aliyepata pointi 45, akishirikiana na Neema Olomi.
Kwa upande wa wanawake, Jackline McCommick aliibuka mshindi kwa pointi 39, akifuatiwa na Loveness Mungure, aliyepata pointi 38, wakati kwa vijana chipukizi Felix Mrema aliibuka kinara kwa pointi 35.
Katika kundi la wachezaji wakongwe, Boudwijn Rip alionesha uzoefu wake kwa kuibuka mshindi akiwa na pointi 33.
Mashindano hayo yalipambwa na vipengele maalumu, ambapo Jan H. Spies alishinda mpigo mrefu zaidi kwa wanaume, huku Loveness Mungure akitwaa ushindi huo kwa upande wa wanawake. Kwa upande wa mpira uliokaribia zaidi shimo, ushindi kwa wanaume ulienda kwa Venance Msebo, na kwa wanawake ukachukuliwa na Neema Olomi.
Mratibu wa mashindano hayo kutoka Taasisi ya Songea Mississippi (SOMI), Reinafrida Rwezaura, amesema katika mashindano hayo wamefanikiwa kukusanya Sh45 milioni kwa ajili ya kusaidia elimu ya wanafunzi 25 walioko mashuleni.
“Tulilenga kukusanya milioni 50, lakini tumepata Sh45 milioni kutoka kwenye ada za wachezaji na sapot ya wadhamini, tunashukuru kwa wote waliofanikisha na tunaahidi tutahakikisha fedha zinaenda kufanya kazi kwa walengwa,” amesema.
Naye mshindi wa watoto, chipukizi Felix Mrema, amesema ushindi huo unampa morali zaidi ya kuhakikisha anazidi kufanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
“Mashindano yalikuwa magumu sana, lakini nimefurahi kuibuka mshindi, natarajia kuanzia sasa kushiriki mashindano mengi zaidi ya ndani na yale ya kimataifa kwa ajili ya kuwakilisha nchi yangu vema na kuitangaza kimataifa.”
Wadhamini wakuu wa mashindano hayo, benki ya NMB, wamesema wamekuwa wakiunga mkono kwa miaka mitano mfululizo kama sehemu ya mchango wa taasisi hiyo katika kukuza michezo nchini na kusaidia jamii.
