Hasara yazidi kuziandama ATCL, TRC

Dar es Salaam. Mashirika mawili ya kimkakati kwenye usafirishaji – Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Reli Tanzania (TRA) yameendelea kupata hasara, licha ya kupewa ruzuku ya uendeshaji na mishahara kutoka serikalini.

Mashirika hayo, yamekuwa katika orodha ya yanayopata hasara katika ripoti mbalimbali za Madhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hali inayoibua hoja katika ufanisi wa usimamizi wake.

Mathalan, katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2022/23, shirika la ATCL ilifikisha jumla ya hasara ya Sh580.18 bilioni tangu lilipofufuliwa mwaka 2015.

Kwa upande wa TRC, kwa ripoti ya mwaka wa fedha 2023/24, lilipata hasara ya Sh224 bilioni ikilinganishwa na Sh102 bilioni ya mwaka uliotangulia wa fedha.

CAG ameeleza hayo leo, Jumatatu Machi 30, 2026 aliposoma muhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi inayoanzia Juni mwaka 2024 hadi Julai mwaka 2025, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kichere, amesema Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa mwaka wa fedha 2024/25 lilipata hasara ya Sh191.19 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 108.

“Hii inafanya kufikisha jumla ya hasara tangu lianzishwe ya Sh748 bilioni, licha ya kuendelea kupokea ruzuku ya Serikali kwa ajili ya mishahara na gharama za uendeshaji,” amesema.

Amesema hasara hiyo imechangiwa na ongezeko la gharama za uendeshaji zilizofikia Sh675 bilioni zinazozidi kiwango cha mapato. Hilo ni sawa na ongezeko la Sh134 bilioni.

Ameeleza shirika hilo lilifanya safari chini ya matarajio na njia 87 za safari zilikuwa na wastani wa ujazo wa abiria asilimia 57 pekee.

Pia, amesema amebaini ndege ya mizigo ya Boeing 767-300F ilitumika kinyume na matumizi yake yaliyokusudiwa na kufanya asilimia 94 ya safari kuwa za masafa mafupi na kati, badala ya safari ndefu zenye mapato makubwa.

Aidha, amesema ndege hiyo ilifanya safari nyingi chini ya uwezo wake wa kubeba na hatimaye ilisimamishwa, huku ikiendelea kugharimu shirika takriban Sh3.54 bilioni kwa ukodishaji na bima bila kuzalisha mapato.

“Hali hii inaonyesha changamoto za kimuundo na utendaji zinazoendelea kuathiri ufanisi wa kifedha katika shirika hili,” amesema.

Pia, Kichere amesema udhaifu wa mifumo ya udhibiti umesababisha malipo ya Sh20.61 bilioni kwa mawakala bila kuthibitishwa kuwafikia abiria, pamoja na marejesho ya nauli za abiria kutokana na kuahirishwa kwa safari Sh310.47 milioni yaliyofanyika bila uthibitisho wa nyaraka.

Amependekeza Serikali iboreshe ufanisi wa shughuli za ATCL kwa kupitia upya faida za njia za safari na matumizi ya ndege na kuandaa mkakati maalumu ya kuongeza ufanisi wa ndege ya mizigo, kuunganisha mifumo ya Tehama ili kuboresha ubadilishanaji wa data na kupunguza michakato nje ya mfumo.

Pia, ameshauri kuimarisha udhibiti wa marejesho ya fedha kutoka kwa mawakala ili kulinda mapato ya kampuni.

Kwa upande wa TRC, Kichere amesema linaendelea kukabiliwa na changamoto za kiutendaji zinazoathiri utendaji wake wa kifedha hasa katika Reli ya MGR ambapo kiwango cha mizigo kimepungua.

Hatua hiyo, amesema imesababisha kushuka kwa mapato na kuongezeka kwa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini, licha ya kuongezeka kwa mapato kulikotokana na Treni za Umeme.

Kichere, amesema shirika hilo limepata hasara kutokana na ajali za treni zilizofikia 328 na kusababisha upotevu wa Sh3.06 bilioni kutokana na uharibifu wa miundombinu na upotevu wa mapato.

Amependekeza shirika hilo, kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya reli kwa kuhakikisha ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara yanafanyika.

Ameshauri pia kutekelezwa kwa mfumo madhubuti wa bima kwa mali zote ikiwemo mabehewa.

Katika ripoti yake, Kichere amesema utendaji wa kifedha wa mashirika ya kifedha, unaonyesha kupungua kwa hasara kutoka Sh412.31 bilioni hadi Sh307.1 bilioni.

Hata hivyo, amesema upungufu huo haujachangiwa na ufanisi wa utendaji, bali umechangiwa na ruzuku za matumizi ya kawaida kwa ajili ya mishahara, gharama za uendeshaji wa taasisi zenye thamani ya Sh105.21 bilioni.

“Jambo hili linaashiria hasara zimehamishiwa kwa Serikali badala ya kupungua kiuhalisia,” amesema.

Licha ya Serikali kutoa ruzuku ya maendeleo ya Sh159.61 bilioni kwa ajili ya uwekezaji, amesema taasisi 22 zimeendelea kupata hasara kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mitatu.

Hali hiyo, amesema inaoinyesha changamoto endelevu ya ufanisi, ongezeko la gharama za uendeshaji na udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani.