Hatari iliyojificha wanaofanya biashara juu ya bomba la Tazama, Dar- 1

Dar es Salaam. Je, unafahamu kuwa kuna maeneo matatu jijini Dar es Salaam yanayotajwa kuwa katika hatari kubwa kwa maisha ya binadamu?

Je, unatambua kuwa bado kuna mianya ya uzembe, huku baadhi ya wahusika wakishindwa kutimiza wajibu wao wa msingi wa kulinda usalama wa watu na mali zao?

Maeneo hayo ni Zakheim (Mbagala, wilayani Temeke), Gongo la Mboto na Pugu, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, ambako hali ya usalama inaelezwa kuwa tete kiasi cha kuibua hofu ya kutokea kwa majanga wakati wowote.

Wakazi wa maeneo hayo wanaishi katika mazingira yanayotia shaka, bila wao kufahamu au wakipuuza, huku wenye mamlaka hawajachukua hatua.

Uchunguzi maalumu uliofanywa na Gazeti la Mwananchi kwa miezi kadhaa umebaini kuwapo kwa ujenzi holela na shughuli za kibiashara zinazoendelea katika maeneo yenye miundombinu nyeti, hususan kwenye ukanda unaopitiwa na bomba la Tazama, hali inayotajwa kuwa sawa na bomu linalosubiri kulipuka.

Mbali na bomba hilo la mafuta, eneo hilo pia linapitiwa na laini kubwa ya umeme ya Gridi ya Taifa, huku chini yake shughuli za kibinadamu zikiendelea kama kawaida.

Mchanganyiko huo wa miundombinu hatarishi na makazi ya watu unaibua maswali mazito kuhusu usalama wa wananchi na mali zao, huku mamlaka zikiwepo.

Ni kama vile wakazi wa maeneo hayo wameweka maisha na mali zao rehani, wakiendelea na shughuli zao za kila siku juu ya bomba la mafuta, huku juu yao kukiwa na nguzo kubwa zinazobeba nyaya zenye msongo mkubwa wa umeme.

Hali hii inaongeza hofu ya uwezekano wa majanga makubwa kutokea bila tahadhari, jambo linalozidisha shinikizo kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka na madhubuti, ili kuzuia maafa yanayoweza kuepukika.

Nyuma ya uhai huu wote kuna ukweli unaopuuzwa na wengi. Juu na chini ya ardhi inayotumika kusaka riziki, kuna miundombinu nyeti yenye hatari kubwa.

Miongoni mwa miundombinu hiyo ni bomba la mafuta la Tazama (Tanzania–Zambia Mafuta), linalosafirisha mafuta ghafi kutoka Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola nchini Zambia.

Bomba hilo lilijengwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania na Zambia kwa lengo la kupunguza gharama za usafirishaji wa mafuta na kuimarisha usalama wa nishati.

Lina urefu wa zaidi ya kilomita 1,700, likiwa na kipenyo cha inchi 24, pamoja na vituo kadhaa vya kusukuma mafuta na maghala ya kuhifadhia. Mradi huu ulianza mwaka 1968.

Zambia ni nchi isiyo na bandari ya bahari, hivyo hutegemea kwa kiwango kikubwa Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kupitisha mizigo yake ya kimataifa.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Lazaro Twange, alipoulizwa kuhusu uwepo wa nyaya za umeme mkubwa kwenye ukanda wa bomba la Tazama, jibu lake lilikuwa kuwa hawezi kusema chochote.

Gazeti hili, katika uchunguzi wake, lilibaini kuwa licha ya kuwepo kwa alama za tahadhari zinazoonesha kuwa shughuli za kibinadamu hazipaswi kufanyika katika maeneo hayo, wananchi wengi hawazingatii maelekezo hayo.

Mfano halisi ni mama lishe, Asha Munira, anayejulikana kwa kuuza maandazi na chai ya tangawizi katika eneo la Mbagala -Zakheim. Kibanda chake kimejengwa juu ya bomba la Tazama, huku juu yake kukiwa na nyaya za umeme wa msongo mkubwa.

Asha anafahamu uwepo wa bomba hilo, lakini amelichukulia kama sehemu ya maisha yake ya kawaida. Anasema hana mpango wa kuhama eneo hilo licha ya hatari iliyopo, kwa kuwa hana mbadala wa eneo la biashara.

“Ndipo riziki yangu ilipo,” anasema, akieleza kuwa wingi wa wateja katika eneo hilo humwezesha kupata kipato cha kila siku, hali inayomfanya kuendelea kubaki licha ya tahadhari zilizopo.

“Tunajua chini ya ardhi kuna bomba, na tumekuwa tukipewa elimu mara kwa mara. Juu kuna nyaya za umeme mkubwa na matangazo ya tahadhari, hata wateja wanaona. Sasa tufanyeje?” anasema.

Kwa mtazamo wake, eneo hilo halina hatari kubwa, kwa kuwa mikutano mingi ya kisiasa na matamasha ya kidini hufanyika hapo.

Pia, kuna stendi ya daladala, na wafanyabiashara wengi wanaendelea na shughuli zao. “Kama kungekuwa na hatari, Serikali ingetuondoa,” anasema Asha.

Kando kidogo ya Asha, yupo muuza matunda, Juma Sedeki, anayesukuma toroli lililosheheni matunda kama vile maembe, mapapai na ndizi, akipita chini ya minara mirefu ya umeme wa gridi ya Taifa, huku nyaya zikining’inia juu.

Wakati mwingine huinua macho na kuziangalia, akifikiria hatari iliyopo, lakini mawazo hayo huyapuuza. “Njaa haisubiri,” anasema huku akitabasamu kwa mteja wake wa kwanza wa siku.

“Biashara yangu ni ya kuzunguka eneo hili. Wateja ni wengi iwe asubuhi, mchana au usiku, mwingiliano wa watu ni mkubwa, na wanahitaji matunda,” anasema.

Katika eneo hilo hilo, kuna mama Subira anayemiliki baa ya pombe za kienyeji na vinywaji vikali. Anasema anafahamu hatari iliyopo, lakini hana sehemu nyingine ya kufanyia shughuli zake.

“Ni kweli kuna hatari, lakini nitaenda kufanya biashara wapi? Kila sehemu imejaa. Hapa wateja ni wengi muda wote, napata riziki na kusomesha watoto wangu watatu,” anasema.

Abdul Razaki, dereva wa bodaboda katika kituo kipya cha Gongo la Mboto, anasema wanafahamu hatari iliyopo, lakini eneo hilo ndilo lenye shughuli nyingi zaidi.

“Eneo hili limechangamka, watu ni wengi. Wapo wanaokuja kununua bidhaa na wanaohitaji usafiri wa bodaboda na bajaji. Ndiyo maana unaona msururu mkubwa, biashara ipo,” anasema.

Anasema muda wote aliokuwapo hapo hajawahi kushuhudia tukio lolote la hatari, jambo linalowapa imani kuwa ni sehemu salama.

“Hata hatari ikitokea, ni mipango ya Mungu. Kufa ni kufa, wengine hufa kwa ajali za barabarani, wengine kwa moto au ajali za anga. Kila mtu ana hatima yake,” anasema.

Abdallah Sebo, mfanyabiashara wa kuchoma na kuuza samaki, anasema amefanya biashara kwa muda mrefu bila kushuhudia tukio lolote la hatari.

“Nimekuwa hapa muda mrefu, hakuna tatizo lililowahi kutokea. Ingawa tunasikia kuna bomba la mafuta, hatuna sehemu nyingine ya kufanya biashara, na Serikali yetu inatutoza ushuru,” anasema.

Kwa upande wake, Richard Steven, mmiliki wa banda la kuangalia mpira, sinema na mchezo wa pool table, anasema wafanyabiashara hupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuheshimu miundombinu hiyo.

“Hili ni eneo la wazi lenye watu wengi. Hufanyika mikutano ya kisiasa, kidini na matamasha ya muziki, hivyo biashara zinaendelea,” anasema.

Kwa upande wake, Mariam Amis, mfanyabiashara mpya wa vinywaji baridi katika kituo kipya cha Gongo la Mboto, anasema hakuwa na ufahamu kuwa eneo hilo ni hatarishi.

“Nimenunua banda hili kwa mfanyabiashara mwingine. Hata mwezi mmoja sijamaliza hapa, na sijawahi kupewa elimu kuhusu hatari hii, lakini mamlaka zinapita kukusanya ushuru,” anasema.

Kauli ya kiongozi wa mtaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani, Jabiri Mohamed, anasema uongozi unatambua uwepo wa miundombinu hiyo nyeti, lakini wanapata ugumu kuwaondoa wananchi wanaotegemea eneo hilo kwa kipato.

“Tunatoa elimu kwa kushirikiana na mamlaka ili wananchi wafahamu hatari na wafanye shughuli zao pembeni, lakini kuwafukuza kunaweza kuleta taharuki,” anasema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gongo la Mboto, Seleman Mwaruko, anasema wafanyabiashara waliopo katika hifadhi ya bomba la Tazama ni wavamizi, na wala hawatozi ushuru wowote katika maeneo hayo.

“Sheria iko wazi, mita 15 kila upande wa bomba ni marufuku kufanya shughuli yoyote. Tumeendelea kutoa elimu, lakini bado kuna ukaidi,” anasema.

Meneja Uendeshaji Kanda ya Tanzania wa Tazama, Saimon Salu, anasema maeneo ya Zakheim, Kituo kipya Gongo la Mboto na Pugu ni sehemu ya hifadhi ya bomba, na kinachoendelea ni uvamizi.

Anasema changamoto katika miundombinu yao imekuwa mtihani kwa taasisi hiyo, kwani inaongezeka kadri miji inavyoendelea kukua, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo mipaka yake ilikuwa ikiheshimiwa.

Salu anasema licha ya kutoa elimu, imefikia hatua wanazidiwa na wanasiasa, hususan katika ngazi za serikali za mitaa. Licha ya kuweka alama maalumu (mikuza) zilizoandikwa jina la Tazama kuonesha mipaka ya hifadhi ya bomba hilo, bado haiheshimiwi.

“Tuna sheria inayotamka wazi mipaka ya miundombinu yetu. Tunaweka alama za mikuza kwa umbali wa mita 30 kila upande, yaani mita 15 kila upande, na eneo hilo linapaswa kuheshimiwa bila uvamizi wowote,” anasema.

Anasema imefikia hatua hadi wameajiri walinzi wanaotembea hadi kilomita 10 kila siku katika maeneo yaliyotengwa kuimarisha ulinzi, lakini bado ni changamoto, mathalani Zakheim na Kituo kipya Gongo la Mboto.

Anasema imekuwa changamoto kuanzia kwa wananchi hadi baadhi ya viongozi wao, ikiwemo madiwani, ambao wamekuwa wakiomba hata kuruhusiwa kupitisha barabara ndani ya hifadhi ya bomba, huku wakiahidi zitakuwa za muda mfupi na za vumbi.

Anatolea mfano wa eneo la Mbagala, Salu anasema Tazama iliwahi kuingia katika migogoro mikubwa hadi na madiwani baada ya kuchukua hatua za kuzuia shughuli za kijamii kufanyika ndani ya hifadhi ya bomba hilo.

“Tulizidiwa na wanasiasa haohao, tunawatoa leo, kesho wanarudi. Kuna kikao tulifanya Januari mwishoni kuueleza uongozi wa mkoa, na waliahidi watashughulikia. Tatizo ni kubwa,” anasema.

Anasema imekuwa changamoto kwani baadhi ya halmashauri zimekuwa zikikusanya ushuru katika maeneo yaliyovamiwa, hali iliyowalazimu kufanya kikao na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwaeleza changamoto hiyo.

“Uvamizi umefika maeneo mengi. Hapo Zakheim, ukirudi nyuma kidogo, wamejenga hadi soko, jambo ambalo halipaswi kuwepo kutokana na hatari ya mafuta yanayosafirishwa kwenye bomba hilo,” anasema.

Anasema, ingawa hawajawahi kufanya sensa kujua idadi ya watu wanaovamia kiholela miundombinu yao, wamekuwa wakiongezeka kila uchao, wakivutiwa na wenzao wanaofanya shughuli zao bila bugudha yoyote.

“Dar es Salaam, bomba hili limechukua kilomita 70 kuanzia Kigamboni hadi Kibaha (Mkoa wa Pwani). Wengi wamejenga mabanda ya biashara. Kuna kesi moja Kigamboni ambapo baadhi wameenda hadi kuzika katika eneo la hifadhi ya bomba,” anasema.

Akizungumzia athari, anasema bomba hilo lina presha kubwa ya mafuta, likipasuka, linaweza kusababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa wa mali. Pia, hata waliojenga karibu na miundombinu hiyo, mafuta yatamwagikia katika makazi yao.

“Msukumo wa mafuta ni mkubwa, zaidi ya mara tano ya presha ya mzunguko wa tairi la gari. Likipasuka, madhara yake ni makubwa,” anasema.

Anaongeza kuwa uvujaji wa mafuta unaweza kuathiri makazi ya watu kutokana na mipango duni ya miji, na pia kusababisha hasara kubwa kiuchumi kwa kampuni, ikiwemo kupoteza mapato.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio, kuhusu hali ya uvamizi wa miundombinu hiyo, alijibu kuwa mamlaka itafanya ziara ya ukaguzi ili kubaini hali halisi na kuchukua hatua stahiki kuondoa tatizo hilo.

“Pia, Tazama kuna wakaguzi wao watakaofuatilia na kutathmini hali iliyopo ili kutafuta ufumbuzi,” anasema Dk Mataragio.

Hata hivyo, Mwananchi ilizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhite, kutaka kujua iwapo anafahamu changamoto hiyo na hatari inayowakabili wanaofanya biashara katika maeneo hayo, naye anasema, “Nitafuatilia na kujua namna ya kufanya kazi.”

Pia, Mwananchi iliwatafuta viongozi wengine kwa nyakati tofauti, wote walikiri kufahamu hali hiyo na kueleza wanachukua hatua, ikiwemo kuandaa maeneo mengine ili wafanyabiashara hao wakafanye kazi katika mazingira salama.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, Sixtus Mapunda, anakiri kuwa eneo la Zakheim, pamoja na kwamba shughuli za kibiashara na kijamii zinazofanyika, ni hatari kwa usalama wao.

“Kwa kushirikiana na halmashauri, tumeanza mipango ya kujenga masoko ya maghorofa Mbagala ili kuwahamisha wafanyabiashara hao na kuwapeleka maeneo rasmi wafanye shughuli zao kwa usalama zaidi,” anasema.

Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal ‘Shetta’, anasema anafahamu jambo hilo, isipokuwa wanalishughulikia, ikiwemo kutafuta maeneo yanayofaa wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao.

“Jambo hili tunalifuatilia na kulishughulikia kwa kuwatafutia maeneo sahihi wanayoweza kufanya shughuli zao kwa usalama,” anasema.