Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ametoa onyo kali kwa Marekani akisema majeshi ya nchi yake yako tayari kukabiliana na wanajeshi wa Marekani iwapo wataingia katika ardhi ya Iran.
Akizungumza kupitia vyombo vya habari vya serikali, Ghalibaf alisema Iran iko tayari dhidi ya vikosi vya Marekani, akidai kuwa kuna dalili za njama za uvamizi wa ardhini licha ya ishara za mazungumzo zinazoonekana hadharani.

Kauli hiyo inakuja wakati Marekani ikiendelea kuongeza nguvu zake za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, ambapo wanajeshi wapatao 3,500 wamewasili hivi karibuni. Kwa mujibu wa US Central Command, wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi kinachoongozwa na meli ya kivita USS Tripoli, ambayo ina uwezo wa kushambulia na kusafirisha wanajeshi.
Ripoti kutoka gazeti la The Washington Post zinaeleza kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inaandaa uwezekano wa operesheni za ardhini dhidi ya Iran, ingawa hakuna uthibitisho rasmi uliotolewa kuhusu kupelekwa kwa vikosi hivyo.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump ametoa kauli zinazokinzana kuhusu mustakabali wa vita hiyo. Wakati mwingine amesema vita iko karibu kuisha, lakini pia amedokeza uwezekano wa hatua zaidi, ikiwemo mashambulizi dhidi ya sekta ya nishati ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa licha ya uwezekano wa kufanikisha malengo ya vita bila vikosi vya ardhini, Marekani inapaswa kuwa tayari kwa hali mbalimbali.
Wakati huo huo, juhudi za kidiplomasia zinaendelea kugubikwa na sintofahamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amekiri kuwa kumekuwepo mawasiliano kupitia wapatanishi, lakini akasisitiza kuwa hayo si mazungumzo rasmi.
Hata hivyo, Trump amedai kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri, akiongeza kuwa Iran inaogopa kukiri hilo hadharani.
Ripoti zinaeleza kuwa Marekani imewasilisha mpango wa vipengele 15 unaolenga kumaliza mgogoro huo, ukiwemo sharti la Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia. Iran nayo imeweka masharti yake, ikiwemo kutambuliwa kwa udhibiti wake wa Mlango wa Hormuz, fidia ya uharibifu wa vita, na kuondolewa kwa kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.
Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari, viongozi kadhaa wa juu wa Iran wameuawa, akiwemo Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na mamia ya raia kupoteza maisha kutokana na mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran yamelenga Israel na kambi za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati, hali iliyosababisha kuvurugika kwa usafiri wa anga na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Hali hiyo inaendelea kuongeza hofu ya kuongezeka kwa vita hiyo na athari zake kwa usalama wa kimataifa.