Geita. Wakati taharuki na mijadala ikiendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu madai ya kuwepo kwa vifo na majeruhi kufuatia kutitia kwa baadhi ya maduara katika mgodi wa Msasa mkoani Geita, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo imethibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini imekanusha kuwepo kwa maafa.
Mgodi wa Msasa uliopo Kata ya Runzewe, wilayani Bukombe mkoani humo, unatajwa kuwa miongoni mwa migodi yenye idadi kubwa ya wachimbaji, ukikadiriwa kuwa na zaidi ya watu 20,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Machi 30, 2026, na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Keneth Mwakisitu amesema taarifa zinazosambazwa mitandaoni si za kweli na zinalenga kuzua taharuki kwa umma.
Amesema operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea kufanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Madini, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Aidha, juhudi zinaelekezwa katika kuokoa mali zilizofukiwa na kifusi pamoja na kuweka miundombinu itakayowezesha kufikia maeneo ya chini ya maduara.
Hadi kufikia mchana wa leo, Mwakisitu amesema vifaa vilivyookolewa ni pamoja na jenereta na winchi inayotumika kuvuta kamba. Amesisitiza kuwa hakuna uthibitisho wa vifo wala majeruhi kama inavyodaiwa.
“Wapo wanaojulikana kama ‘manyani’ au wavamizi wasiokuwa na vibali rasmi. Hao ndio tunaoweza kuwa na wasiwasi nao huenda walikuwepo eneo hilo. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya mtu kupotea au ndugu kuripoti kutokuwepo kwa jamaa yake,” amesema.
Kwa upande wake, Chifu Inspekta wa mgodi wa Msasa, James Nkamba, amesema kabla ya tukio hilo walibaini nyufa katika eneo husika wakati wa ukaguzi wa kawaida na kuchukua hatua ya kuwaondoa watu wote.
“Baada ya kuwaondoa, takribani dakika 15 baadaye eneo hilo likatitia. Wakati huo tayari halikuwa na watu kwani lilikuwa limesimamishwa kwa muda wa siku mbili kwa ajili ya ukarabati,” amesema Nkamba.
Naye fundi mchimba mgodi, Shukuru Kapera, amesema alibaini uwepo wa nyufa hatarishi siku mbili kabla ya tukio na kutoa taarifa kwa uongozi, hatua iliyosaidia kuokoa maisha ya watu.
“Niliona nyufa na kutoa taarifa kuwa eneo si salama. Uongozi ulichukua hatua na watu wakaondolewa. Hivyo, taarifa za vifo ni uzushi tu,” amesema.
George Mwikazi kutoka kitengo maalum cha ukaguzi wa usalama amesema hakuna mwili wowote uliopatikana hadi sasa, akibainisha kuwa eneo hilo lilikuwa limefungwa na kuwekwa alama za tahadhari.
“Maduara yale yalikuwa chini ya ukarabati na tayari yalikuwa yamewekewa alama za hatari. Tukio lilianza kwa ishara za nyufa, na baada ya muda mfupi ndipo kutitia kulipotokea. Hakukuwa na mtu yeyote eneo hilo,” amesema.
“Kitu cha kwanza tulichokifikia, zilisikika sauti za ‘bam bam’, baadaye tukakuta jenereta, ikafuatiwa na pikipiki iliyokuwa kwenye winchi. Hadi sasa tunaendelea na uokoaji, lakini hatujapata kitu chochote kinachoashiria hata shati la mtu au mwili wowote,” amesema.