Dar es Salaam. Wakati mwaka jana mvua zilionekana kusababisha zaidi uharibifu wa miundombinu, mwaka huu zimegeuka tishio kwa maisha ya watu, zikisababisha vifo vya zaidi ya watu 38 nchini hadi sasa.
Mbali na idadi hiyo ya watu kupoteza maisha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu (sawa na siku 90), mvua hizo zimekuwa chanzo cha kukosekana kwa mawasiliano ya barabara, mfano Ifakara-Mlimba, huku makazi ya watu yakijaa maji.
Hii ni tofauti na mwaka jana ambapo kwa kiwango kikubwa mvua hizo zilisababisha barabara kufungwa, gharama za usafiri kupanda, foleni, huku mazao ya mashambani yakiharibika katika baadhi ya maeneo.
Machi 21, 2026, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitoa angalizo la mvua kubwa kwa mikoa kadhaa, ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na hali ya hewa mbaya.
Taarifa hiyo ilieleza uwezekano wa kutokea madhara makubwa, ikibainisha athari mbaya zinazoweza kutokea ni mafuriko katika baadhi ya maeneo na kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi.
Ili kuepukana na vifo vitokanavyo na hali mbaya ya hewa, wataalamu wametahadharisha wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kama mabondeni, kando ya mito na maeneo ya miteremko kuchukua tahadhari za haraka, ikiwemo kuhamia sehemu salama pindi mvua inapozidi au dalili za mafuriko zinapoanza kuonekana.
Wamesema wananchi wanapaswa kuepuka kuvuka mito au maji yanayotiririka kwa nguvu, kwani hali hiyo imechangia ajali nyingi na vifo.
Vilevile, wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini zaidi na watoto, ambao mara nyingi huwa waathirika wakubwa katika matukio ya mafuriko.
Askali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wakitafuta mwili wa mtoto chini ya daraja linalounganisha Tabata Mwananchi na Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam ambapo mtoto huyo alitumbukia katika mto huo uliokuwa umejaa maji kutokana na mvua iliyonyesha juzi. Picha na Michael Matemanga
Mtaalamu wa Mazingira, Rahel Elibariki, anasema ili kuepukana na athari za mvua, watu wanaoishi maeneo hatarishi waondoke kwa muda.
“Kama unajua upo sehemu ya hatari ni muhimu kuondoka kwa muda ili uepukane na madhara. Pia tuifuatilie taarifa za hali ya hewa tusizipuuze; kama umesikia hali ya hewa ni mbaya au una safari siku hiyo, ni bora uache usafiri wakati mwingine,” anasema.
Mchambuzi wa hali ya hewa kutoka TMA, Ramadhani Omary, anataja mambo manne ambayo wananchi wanaweza kuyafanya ili kuepusha majanga yanayotokea kutokana na mafuriko au upepo mkali.
“TMA tumekuwa tukitoa taarifa za utabiri mara kwa mara, na kuna kipindi tunaeleza uwepo wa mvua kubwa, upepo mkali na matukio kama hayo. Wananchi wazipe kipaumbele taarifa hizi na kuchukua hatua,” anasema.
Anasema pia wajiepushe kuishi kwenye maeneo hatarishi ikiwamo mabondeni na kwenye kingo za mito.
Maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha na kusababisha maafa ya vifo vya watu 18 katika Kata ya Nkunga, Lupepo, Kawetele na Ikuti wilayani Rungwe.
Anafafanua kuwa pia kuna utaratibu usio mzuri wa baadhi ya watu kutupa taka kwenye mitaro na mifereji ya maji na kusababisha kuziba.
“Wananchi wawe na utaratibu wa kusafisha mifereji na mitaro ili maji yaweze kutembea, na maeneo ambayo hayana mitaro au mifereji yawekwe,” anasema.
Omary anasema changamoto nyingine ni ujenzi holela kwenye njia za asili za maji. Hivyo, inapotokea mvua kubwa, maji yanatafuta njia na kusambaa na kusababisha mafuriko.
“Wananchi wawe na utaratibu wa kuheshimu njia za asili za maji; hii ni changamoto nyingine ambayo inasababisha mafuriko na mengine kupelekea maafa,” anasema.
Anasema ushauri wa wataalamu wa maafa na mazingira pia unapaswa kuzingatiwa katika nyakati ambazo TMA imetoa tahadhari ya hali ya hewa.
Naye Joel Ulome, mchambuzi wa masuala ya maendeleo, anasema jamii na mamlaka za mitaa kuna haja ya kuchukua hatua za pamoja za kupunguza madhara.
Hatua hizo ni kusafisha mifereji ya maji, kuzuia ujenzi holela katika maeneo hatarishi, na kutoa elimu ya mara kwa mara kuhusu tahadhari za majanga.
“Kwa mtazamo wa kitaalamu, mabadiliko ya tabianchi yanaongeza uwezekano wa matukio haya kujirudia, hivyo maandalizi ya muda mrefu yanahitajika ili kulinda maisha ya watu na mali zao,” anasema.
Mkoani Mbeya, wilayani Rungwe, kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha mkoani humo kuanzia Machi 25, 2026, ikiambatana na upepo mkali uliyosababisha maporomoko ya udongo, watu 20 walifariki dunia.
Hali ilivyokuwa katika Barabara ya kwenda Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam, baada ya mvua kubwa kunyesha mchana wa Jumamosi Machi 28, 2026.
Taarifa ya vifo vya watu hao ilitolewa Machi 26, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, akisema maporomoko hayo yalisababisha uharibifu wa nyumba.
Vifo vingine vilivyotokana na hali mbaya ya hewa, vilidhibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Machi 18, 2026.
Tukio la radi ndilo alilotaja kamanda huyo akieleza lilisababisha vifo vya wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Msongola, iliyopo Kivule, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.
Mbali na hayo, Machi 11 mwaka huu, mkoani Dodoma, mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 9, 2026 iliripotiwa kusababisha vifo vya watu watano katika wilaya za Kondoa, Chemba, na Bahi.
Nako mkoani Morogoro, Februari 23, 2026, ilielezwa mvua zilisababisha watu wawili kupoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa kwa kupigwa na radi, Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro.
Taarifa hiyo ilitolewa na siku hiyo na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, akisema tukio hilo lilitokea usiku wa Februari 23, 2026, katika kitongoji cha Mbesi, kijiji cha Utengule, Halmashauri ya Mlimba, wakati watu hao wakiwa njiani wakitoka matembezini.
Kamanda Mkama ambaye kwa sasa ni Kamishna wa Polisi Jamii kuanzia Machi 26, 2026 alisema radi hiyo iliwapiga ghafla wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha, hali iliyosababisha vifo vya watu wawili papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa.
Februari 22, 2026, mkazi wa Kitongoji cha Kambeni, Kata ya Myamba, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Stephano Zawadi (43), alifariki dunia kwa kupigwa na radi wakati alipokuwa akimfuata mkewe shambani aliyekuwa akizuia tumbili wasile mahindi.
Imeelezwa mwanaume huyo baada ya kurudi ibadani jioni ya Februari 22, alimfuata mke wake shambani alikokuwa akilinda tumbili wasile mazao yao, na akiwa njiani alipigwa na radi na kufariki dunia.
Nako mkoani Songwe, Februari 20, 2026, watu watatu, akiwamo mwanafunzi wa darasa la pili, wamefariki dunia kufuatia mvua zilizonyesha mkoani humo.
Taarifa hiyo ilitolewa na Jeshi la Polisi Februari 21, 2026, mkoani humo, matukio hayo yalitokea maeneo mbalimbali.
Tukio la kwanza lilitokea saa 10 jioni katika Kijiji cha Ssenga, Kata ya Halungu, wilayani Mbozi, ambapo mtu mmoja, Said Kamwela (62), alifariki dunia kwa kuzama kwenye maji.
Lingine lilimuhusisha mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Migombani, Janeth Tarimo, baada ya kuteleza na kutumbukia katika korongo lililokuwa na maji mengi alipokuwa akitoka shuleni kisha kusombwa na maji hayo, saa 10 jioni huko Kaloleni, wilayani Momba.
Pia, imeeleza saa moja usiku, mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake, anayekadiriwa kuwa na miaka 30, alifariki dunia baada ya kuteleza na kutumbukia kwenye korongo lililokuwa likitiririsha maji kutokana na mvua zinazoendelea.
Machi 27, 2026, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Yusuph Mwandami, mke wake, mtoto pamoja na dereva wao, waliripotiwa kufariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika daraja la Mto Mang’onyi, wilayani Ikungi.
