Orkeeswa yajifua Zanzibar kusaka uzoefu wa kimataifa

KOCHA Mkuu wa timu ya kikapu kwa wanawake ya Orkeeswa kutoka Arusha, Benjamin John amesema ushiriki wao katika mashindano ya Asma Mwinyi Next Generation ni sehemu ya maandalizi ya kikosi hicho kuelekea mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Asma Mwinyi Next Generation yaliyoanza Machi 28, 2026 na kutarajiwa kutamatika leo, Jumatatu, kocha huyo amesema wamejipanga kutoa ushindani kwa lengo la kujitathmini.

“Tumekuja katika mashindano haya tukiwa  na lengo ya kuwapa wachezaji wetu nafasi ya kupata uzoefu na mazoezi zaidi kwa kukutana na timu mbalimbali zenye viwango tofauti,” amesema.

Aliongezea kuwa kukutana na timu hizo kutawasaidia wachezaji kuongeza uwezo wa kiufundi na kujiandaa vyema kwa mashindano ya Afrika na kwamba kikosi chake kimefanya maandalizi.

Benjamin amesema timu hiyo imewahi kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, ikiwemo kushika nafasi ya pili katika moja ya mashindano ya Afrika Mashariki pamoja na kuwa miongoni mwa timu saba bora katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Misri.

Kwa upande wake, mchezaji wa timu hiyo, Namnyaki Isaya amesema wachezaji wamejipanga kuitumikia vyema timu yao na kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Amesema ushindani unaotarajiwa katika mashindano ya Asma Mwinyi Next Generation utawasaidia kuongeza uzoefu na kuimarisha kiwango chao kabla ya kushiriki mashindano ya Afrika.