MSHAMBULIAJI Mtanzania Said Khamis Said Jr anayekipiga katika timu ya Imigresen ya Ligi Kuu Malaysia ameamua kupigania kiatu cha dhahabu katika mashindano hayo akimkimbiza polepole anayeongoza kwenye msimamo wa wafungaji bora hadi sasa.
Nyota huyo wa zamani wa Hatta Club ya Ligi Daraja la Kwanza Dubai na Bani Yas ya Falme za Kiarabu, msimu huu katika mechi 21 amefunga mabao 16 na kutoa asisti nne, rekodi zinazomuweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania ufungaji bora.
Kuhusu ushindani amesema: “Naona nafasi ya kuwa mfungaji bora ipo. Tofauti siyo kubwa. Nahitaji kuongeza juhudi kidogo tu kwa sababu anayeongoza (ufungaji bora) anayo 21, nafasi ya pili ana mabao 17 ninayefuata ni mimi.”
Huu ni msimu wake wa kwanza katika ligi hiyo, lakini ameonyesha kuzoea haraka mazingira mapya. Klabu anayiitumikia ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, lakini bado wana mechi saba mkononi.
Akizungumzia ligi hiyo, amesema imesimama kwa muda hadi Juni, mwaka huu ili kupisha mashindano ya timu za taifa.
Said aliliambia Mwanaspoti kwamba, katika kipindi hiki cha mapumziko ya miezi mitatu anaendelea na programu maalumu ili kuuweka mwili sawa kabla ya kurejea kwa mashindano hayo.
Amesema, “nimeanza vizuri hapa Malaysia, lakini bado nina malengo makubwa zaidi na ninaona bado nina kazi ya kufanya.”
